KIUNGO wa Fountain Gate, Abdallah Kulandana bado anaweweseka na kipigo cha mabao 2-0 ilichopewa timu hiyo na Yanga, huku akilitaja bao la Prince Dube lililotokana na penalti kuwa ndilo lililowatoa mchezoni na kujikuta wakipoteza mechi hiyo inayokuwa ya sita msimu huu.
Kipigo hicho kilichopatikana kwenye Uwanja wa KMC kilikuwa cha pili mfululizo kwa timu hiyo kwa mechi zilizopita, na kuiacha Fountain ikisalia nafasi ya 10 na pointi 10 kutokana na mechi 10, ikiwa na maana imevuna alama moja kwa kila mechi hadi sasa, huku Yanga ikifikisha 13.
Awali, ilipasuka kwa mabao 2-0 pia kutoka kwa maafande wa JKT Tanzania ilipowakaribisha kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa mjini Babati Manyara, lakini Kulandana ameliambia Mwanaspoti kuwa katika mechi dhidi ya Yanga walijipanga kuwabana watetezi hao wa ubingwa wa ligi, lakini bao la Dube likawatibulia.
Kulandana amesema mpango wao ulikuwa ni kucheza kwa kuiheshimu Yanga kwa kujilinda zaidi na kuwaacha wenyeji wacheze na walifanikiwa kwa dakika za mwanzo hadi dakika ya 29 Dube alipofunga kwa penalti na kuwakata stimu.
“Mechi ilikuwa ngumu kwetu tumekutana na timu bora ambayo ina wachezaji wengi bora na wazoefu. Tuliingia kwa kumheshimu mpinzani na mbinu ya kuzuia, tukishambulia kwa kushtukiza tulifanikiwa kufika langoni, lakini umaliziaji ulikuwa mbovu,” amesema Kulandana na kuongeza:
“Hatukuwa vibaya sana kama timu, tulijitahidi kufanya majukumu tuliyopewa. Ubora wa mchezaji mmoja mmoja kwenye kikosi cha Yanga ndio ulituhukumu na kujikuta tunapoteza mchezo na bao la kwanza la penalti lilitunyong’onyesha na kututoa mchezoni.”
Kulandana amesema mara baada ya dakika 45 kuisha na kurudi vyumbani, kocha wa timu hiyo aliwajenga kisaikolojia na kuwaaminisha kuwa bado wana nafasi ya kuwa bora na kupata walau alama moja, lakini mambo yakawa magumu baada ya Yanga kupata bao la pili dakika za jioni.
“Sio nzuri kwetu kupoteza mechi mbili mfululizo, naamini kocha ameona upungufu wetu na anaufanyia kazi ili kurudisha timu kwenye mstari na kuendelea na ushindani. Na sisi kama wachezaji tuna kazi ya kufanya ili kupunguza makosa hasa safu ya ulinzi,” amesema mchezaji huyo.
Bao la pili la Yanga lilifungwa na mtokea benchi, Pacome Zouzoua na kumfanya afikishe mabao mawili msimu huu katika Ligi Kuu huku Yanga ikifikisha mechi ya tano bila kupoteza.
Hata hivyo, rekodi zinaonyesha kuwa Fountain haijawahi kupata ushindi wowote mbele ya Yanga tangu ilipopanda daraja 2022, kwani zimeshakutana mara saba na zote imepasuka, ikifungwa mabao 22 na yenyewe kufunga moja kupitia katika mechi ya Novemba 17, 2022 ilipofungwa 4-1.
