CHAMA la mshambuliaji wa Mtanzania Mgaya Ally (Salalah SC), linaloshiriki Ligi Daraja la Kwanza Oman liko kwenye hali mbaya katika msimamo wa ligi.
Mgaya alijiunga msimu huu kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Coastal Union ya Tanga ambako nako alitumikia nusu msimu.
Hadi sasa ligi hiyo imepigwa mechi 26 na Salalah iko mkiani mwa msimamo wa ligi yenye timu 14, huku kileleni ikiwa Fanja SC yenye pointi 48 sawa na Al Suwaiq iliyopo nafasi ya pili.
Kwenye mechi 26, Salalah imeshinda tatu, sare tano na kupoteza 18 ikifunga mabao 19 na kuruhusu 45 ikikusanya pointi 14.
Inayoshika nafasi ya 13, Sur Club ina pointi 21 kwenye mechi 26 imeshinda tatu sare 12 na kupoteza 11 ikiwa na pointi 21.
Hadi sasa zimesalia mechi mbili kumalizika kwa ligi hiyo na chama la Mtanzania huyo hata likishinda mechi mbili zilizosalia itaendelea kushika nafasi ya mkiani.
Hivyo Salalah inashuka rasmi Ligi Daraja la tatu baada ya kukusanya pointi hizo ambazo hata ikishinda hazitakuwa na maana yeyote.
Akizungumza na Mwanaspoti Mgaya amesema: “Ni matokeo yanayoumiza lakini kama mchezaji nitaangalia ofa zitakazokuja sababu sitaki niendelee kucheza timu za madaraja ya chini.”
Kabla ya Coastal Mgaya aliitumikia Fleetwoods ya Uarabuni misimu miwli akifunga mabao 20, timu hiyo ilikuwa inashiriki ligi daraja la kwanza.
