Coastal v Yanga vita ipo hapa!

WAGOSI wa Kaya, Coastal Union usiku wa leo watakuwa wenyeji wa Yanga katika mechi ya Ligi Kuu Bara, huku wakiwa na rekodi ya unyonge wa kupasuka mechi nane mfululizo mbele ya watetezi hao tangu 2022, jambo lililowafanya mabosi wa klabu hiyo kushtuka na kuapa leo ni leo.

Coastal inaipokea Yanga kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kuanzia saa 1:15 usiku baada ya Uwanja wa Mkwakwani – Tanga kufungiwa na kuwakosesha mashabiki wa soka wa jijini hilo kuiona Yanga kwa miaka miwili mfululizo.

Kibaya ni kwamba Coastal inakutana na Yanga kwenye Uwanja wa Jamhuri huku ikiwa na rekodi mbaya mbele ya watetezi hao wa Ligi Kuu, kwani mara ya mwisho kushinda tena ikiwa nyumbani ilikuwa Machi 4, 2021 ilipowalaza vijana wa Jangwani kwa bao 1-0.

Baada ya hapo imekuwa ikipasuka kila ikikutana na Yanga nje ndani kwa misimu minne mfululizo na safari hii Wagosi wamekuja na kauli mbiu ya ‘Wanapigika…zamu yao kulia’ wakiamini kwamba leo iwe isiwe ni lazima wageni wao wapasuke Jamhuri kitu ambacho huenda Yanga haitakubali.

Rekodi zinaonyesha kuwa timu hizo zimeshakutana katika mechi 24 za Ligi Kuu Bara tangu 2011, Wagosi wakishinda mechi tatu na kupasuka 16 wakati mechi tano ziliisha kwa sare, huku kwa msimu huu kila moja ikiwa na mwenendo wake, Yanga ikionekana bora kuliko Coastal Union.

Katika mechi tano zilizopita za Ligi Kuu msimu huu Coastal imeshinda moja dhidi ya Mbeya City, ikitoka sare tatu na kupoteza moja tofauti na Yanga iliyocheza pia mechi tano ikishinda nne ikiwamo iliyopita dhidi ya Fountain Gate na kutoka sare moja na haijapoteza mechi yoyote.

Mechi ya leo kila timu inaingia uwanjani ikiwa na hesabu zake, Yanga ikitaka kuthibitisha ubora na kuendelea kukusanya pointi wakati Coastal ikitaka kufuta uteja ilionao mbele ya wapinzani wao wanaoshika nafasi ya tatu kwa sasa wakiwa na pointi 13.

Kwa miaka miwili Yanga haijacheza Mkwakwani kuumana na Coastal kutokana na sababu kadhaa ikiwamo kufungiwa kwa uwanja na matokeo yote ya ugenini iliyapata kwenye viwanja vingine ikiwamo Sheikh Amri Abeid na kuepuka zile aibu ilizokuwa ikikutana nazo Mkwakwani.

Kabla ya Wagosi kugeuka nyanya, Yanga ilikuwa inataabika kila ikiifuata Coastal Mkwakwani na matokeo mazuri kwao ilikuwa sare kabla ya kuinasa ‘code’ 2025 kwa bao la Nadir Haroub ‘Cannavaro’ lililomsababisha nahodha huyo wa zamani wa timu hiyo na Taifa Stars kwenda kulishangilia kwa kumkumbatia askari trafiki na kuzua gumzo kipindi hicho.

Pia, Coastal ni moja ya timu iliyowahi kuitibulia Yanga rekodi ya kucheza mechi 18 mfululizo bila kupoteza kwa kuipasua mabao 2-1 na kumpoza kocha wa kipindi hicho Cedric Kaze kutimuliwa na ndio uliokuwa ushindi wa mwisho kwa Wagosi kwani mechi nane zilizofuata imepasuka zote.

Hata hivyo, ikiwa chini na kocha Mohamed Muya, Coastal imejinasibu leo inataka kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kuifunga Yanga iliyocheza karibu mechi 25 bila kupoteza kwani matra ya mwisho timu hiyo kuonja kipigo ni Novemba 7, 2024 ilicharazwa mabao 3-1 na Tabora United (sasa TRA United) iliyomsababisha kocha Miguel Gamondi kutimuliwa kazini.

Lakini ni Yanga iliyosababisha pia Muya kufutwa kazi enzi akiwa Fountain Gate wakati timu hiyo ya Manyara ilipopasuliwa mabao 5-0 na leo anakutana nao tena akiwa na Wagosi wa Kaya.

Ni mechi ambayo Yanga iliyopo chini ya kocha Pedro Goncalves itaendelea kuwategemea nyota kama Pacome Zouzoua, Prince Dube, Maxi Nzengeli, Duke Abuya, huku Coastal ikitambia kina Maabad Maulid, Athuman Masumbuko, nahodha Bakar Msimu na wengine kuichachafya ngome ya Yanga chini ya kipa Djigui Diarra na mabeki Dickson Job na Bakar Mwamnyeto anayeweza kuanza kukabiliana na waajiri wake wa zamani.

Makocha wa timu hizo wamezungumzia pambano hilo ambalo Kocha Pedro alisema: “Namba za wapinzani wetu hazidanganyi, wameruhusu mabao machache katika mechi walizocheza na kila mara tukikutana nao tunakuwa na mchezo mgumu, hata kesho (leo) tunajua hautakuwa mchezo mrahisi lakini tuna kikosi bora na tutapambana kuhakikisha tunaondoka na pointi tatu.”

“Maandalizi yetu siyo makubwa kuelekea mchezo huu kwa sababu ya muda mchache tuliopata kutokea mchezo wetu uliopita, tuna baadhi ya wachezaji wako sawa na kuna wengine wana uchovu. Lakini kwenye akili zetu tunajua ni nini tunataka na tuko hapa kutafuta ushindi,” alisema Pedro huku  Offen Chikola kwa niaba ya wachezaji wa timu hiyo alisema;  “Tumejiandaa vizuri kuwakabili Coastal Union kesho, ni kweli mechi zetu huwa zinakuwa na ugumu lakini tunajua umuhimu wa mchezo wa kesho na tumejiandaa kuondoka na ushindi.”

Kwa upande wa kocha wa Coastal Mohammed Muya alisema; “Naheshimu sana ubora wa Yanga na ukubwa wao ila mechi ya kesho (leo) tumejipanga kufanya vizuri, Mungu akileta kheri wachezaji wakiamaka vizuri na wafuate maelekezo niliyowapa basi mashabiki wa Coastal Union watafurahi.”

Huku nahodha wa timu hiyo, Bakar Msimu alisema; “Uwanja wa Jamhuri umetupa pointi moja katika michezo miwili tuliyocheza hapa msimu huu, tunajua mechi ya kesho (leo) ni mgumu ila tumejipanga vizuri kupata pointi tatu.” Mbali na mechi hiyo ya Dodoma, mapema saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Simba na Azam zitamalizana katika pambano la Dabi ya Mzizima, Wekundu wakiwa chin ya Kaimu Kocha Mkuu, Seleman Matola na Wanalambalamba wakiwa na Florent Ibenge.

Timu hizo zinakutaka kila moja ikitoka kupata matokeo tofauti ya mechi zilizopita za Ligi, Simba ikitioka kushinda 3-0 mbele ya Mbeya City na Azam kutoka suluhu na Singida Black Stars, lakini hata zilipokutana mara ya mwisho msimu uliopita zilitoka sare ya 2-2.

Soma zaidi uchambuzi wa mechi hiyo ukurasa wa 8&9.