Dar es Salaam. Moja kati ya yaliyovutia katika mahafali ya 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ni wingi wa wahitimu wanawake.
Kwa mfano, katika duru la pili la mahafali hayo yaliyofanyika Novemba 18, 2025, wahitimu 2,742 walitunukiwa Shahada, Stashahada na Astashahada kati yao wanawake walikuwa 1,510 sawa na asilimia 55.4 na wavulana wakiwa 1,232.
Vivyo hivyo, katika duru ya tatu wahitimu 2,452 walitunukiwa shahada za awali na astashahada kati yao wanawake walikuwa 1,386 sawa na asilimia 56.6, huku wanaume wakiwa 1,066.
Licha ya wingi wao, baadhi ya wahitimu wanawake wamefaulu kwa kiwango cha juu na hata kufikia hatua ya kutambuliwa kuwa wanafunzi bora.
Miongoni mwa wahitimu hao wanawake waliotambuliwa kwa kufanya vizuri zaidi ni Cynthia Yalimba, aliyehitimu Shahada ya Awali ya Elimu ya Jamii katika Utekelezaji wa Sheria kutoka UDSM.
Yalimba, mtoto wa wazazi wajasiriamali, mama lishe na dereva wa bodaboda amepata ufaulu wa daraja la kwanza kwa kiwango cha GPA ya 4.4.
Licha ya kuwa hakuwa miongoni mwa wanafunzi bora, alitambuliwa kutokana na kuvunja rekodi ya ufaulu ambao haujafikiwa na mwanafunzi yeyote wa Shahada ya Awali ya Elimu ya Jamii katika Utekelezaji wa Sheria kutoka UDSM kwa zaidi ya muongo mmoja (miaka 10).
Kwa hatua hiyo, mkuu wa chuo hicho, Rais mstaafu Jakaya Kikwete, alimpongeza Yalimba.
Katika mahojiano na Mwananchi, Yalimba ambaye ni mtoto wa kwanza kati ya saba katika familia yao anaeleza safari yake ya elimu na maisha kwa jumla.
Anasema mwaka 2008 alianza shule ya msingi mkoani Njombe na tangu hapo aliweka malengo ya kufaulu vizuri ili aweze kusoma Shule ya Sekondari Anne Makinda.
Bahati haikuwa yake, alipohitimu elimu ya msingi alichaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Mabatini, alikohitimu mwaka 2019.
“Japokuwa sikufikia malengo yangu, sikukata tamaa. Nilijipa moyo kuwa maisha ni popote,” anasema.
Anasema elimu ya kidato cha tano na sita aliipata katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Tabora alikohitimu mwaka 2022 akachaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kusoma Shahada ya Awali ya Elimu ya Jamii Katika Utekelezaji wa Sheria.
“Safari yangu ya elimu ya msingi na sekondari kwa jumla haikuwa rahisi na kila malengo ya kitaaluma niliyojiwekea yalikuwa hayatimii,” anasema.
“Mfano, kidato cha nne niliweka malengo ya kupata ufaulu wa pointi 1.7 lakini niliishia kupata 1.12, hata kidato cha sita nilitamani kupata 1.3 sikufanikiwa nikapata 1.5, lakini sikukata tamaa. Nikasema nikifika chuo kikuu nitapambana kuhakikisha navunja rekodi katika fani nitakayochaguliwa kusoma.”
Anaeleza ilikuwa furaha alipopokea ujumbe kuwa amechaguliwa kujiunga UDSM kusoma fani iliyojikita katika utekelezaji wa sheria.
“Niliona nuru katika kufikia ndoto yangu, kwani tangu nikiwa na umri mdogo nilitamani kufanya kazi katika taasisi zinazojishughulisha na masuala ya uhamiaji,” anasema.
Hata hivyo, baada ya kuwasili chuoni anasema alisikia kauli za waliomtangulia kuwa kozi aliyopangiwa ni ngumu, hivyo siyo rahisi kufaulu.
Anasema awali, alikatishwa tamaa lakini baadaye aliibadili hofu yake kuwa fursa kwa kuhakikisha anafaulu.
“Awali, niliona masomo ni magumu hasa sheria za kimataifa, nikajiuliza hivi nitafika? Nakumbuka nilirudi hosteli nikawaza lakini kuna mwenzangu wa mwaka wa pili kutoka fani ya uhandisi alinionesha matokeo yake ya mwaka wa kwanza ana ufaulu wa GPA ya 4.8 nilipata moyo, nikaona hata kwangu inawezekana,” anasema.
Anaeleza alikataa kuishi katika historia, akaamua kufanya juhudi iliyomfikisha alipo japokuwa lengo lake lilikuwa kuwa mwanafunzi bora wa jumla.
“Nilichojifunza katika safari yangu ya elimu ni kuwa, maisha yanahitaji juhudi endelevu na kutokata tamaa, kwani siyo mara zote utapata kile unachokitaka,” anasema.
“Kila mtu ana nafasi ya kuandika historia bora ya maisha yake. Hata kama wengine walishindwa, haimaanishi kuwa wewe hautaweza, ni muhimu kukataa kuishi katika historia.”
Anasema anatamani kufanya kazi kwenye taasisi zinazohusu masuala ya uhamiaji na huduma kwa wakimbizi, pia kujiendeleza katika masomo kufikia ngazi ya Shahada ya Uzamivu.
Shukrani zake ni kwa wazazi wake waliomsaidia, kumuongoza na kuhakikisha anapata mahitaji yote muhimu wakati akiendelea na masomo licha ya kuwa na kipato kidogo.
“Wazazi wangu wamepambana, wamenishika mkono hadi kufikia hapa. Nawashukuru bila wao pengine nisingefika hapa,” amesema.
Rose John, mama mzazi wa mhitimu huyo anasema changamoto alizopitia utotoni na kusababisha asiende shule ndizo zilizomsukuma kuhakikisha mwanaye anapata elimu.
Mama huyo mkazi wa Njombe, anasema baada ya baba yake kufariki dunia, hali ya uchumi iliyumba hakuweza kuendelea na masomo akabaki nyumbani akisubiri kudra za Mungu.
“Niliapa sitakubali maumivu ya kutopata elimu niliyopitia yatokee kwa watoto wangu, nimepambana kuhakikisha mwanangu anafika hapa,” anasema.
Anasema binti yake humsaidia katika biashara anapokuwa likizo, hivyo kumwezesha yeye kufanya shughuli za kilimo ili kujiongezea kipato.
Mama huyo anatoa wito kwa wazazi hasa wenye kipato cha chini na cha kawaida kutokata tamaa, kwani wanaweza kusomesha watoto wao.
“Kipato chetu kisitutie unyonge, tupambane tuwawezeshe watoto wetu kusoma vizuri ili wapate hatima iliyo njema,” anasema.
Amidi wa Shule Kuu ya Sheria, Dk Fransis Sabby anasema moja ya changamoto inayowafanya baadhi ya wanafunzi kuona masomo yanayohusiana na sheria ni magumu na kutofanya vizuri ni dhana wanayoiweka akilini mwao kuwa masomo hayo ni magumu.
Pia, baadhi ya wanafunzi kutokuwa tayari kujifunza na kutozingatia mambo ya msingi katika kujifunza.
Dk Sabby anatolea mfano wa baadhi ya wanafunzi kutohudhuria vipindi darasani na wengine kutumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii kuliko kusoma darasani na kujisomea.
“Mtu wa namna hii ni ngumu kufanya vizuri kwani katika kufaulu hakuna miujiza,” anasema Dk Sabby.
Anasema kama mwanafunzi atakuwa na nia na utayari wa kujifunza atafaulu kwa viwango vya juu.
Dk Sabby anasema katika nyakati za sasa usomaji umerahisishwa kutokana na kukua kwa utandawazi.
“Kupitia intaneti wanaweza kujifunza mambo mbalimbali kwa urahisi zaidi, hivyo nafasi ya kufanya vizuri ni kubwa,” anasema.
