Hekta 170 za Mlima Hanang zaungua moto

Hanang. Hekta 170 za hifadhi ya mazingira asili ya mlima Hanang mkoani Manyara, zimeungua moto uliodumu kwa muda wa siku tatu.

Mlima Hanang una ukubwa wa hekta 5,371 na urefu wa mita 3,4200 kutoka usawa wa bahari ni wa tano kwa urefu nchini ukitanguliwa na Kilimanjaro, Meru, Loolmalasin na Oldonyo Lengai.

Ofisa uhifadhi wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Abubakary Mpapa akizungumza leo Desemba 7,2025 amesema moto huo umeharibu zaidi ya hekta 170.

Mpana ameeleza kwamba moto huo ambao bado chanzo chake hakijafahamika mara moja ulianza Desemba 3,2025.

Ameeleza kwamba Waziri wa Maliasili na Utali, Ashatu Kijaji anatarajia kufanya ziara wilayani Hanang kwa ajili ya kukagua athari za moto huo.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amewataka wakazi wa eneo hilo kuepuka kufanya shughuli za kuharibu mlima ikiwemo uvutaji wa sigara na kurina asali.

“Jamii kwa ujumla zilizopo jirani na mlima Hanang wanapaswa kuwa makini katika kufanya shughuli za kibinadamu ili kuepuka madhara ambayo siyo ya lazima,”  amesema Sendiga.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, mkoani Manyara, Emmanuel Kiabo amesema askari wa jeshi hilo, mgambo na vijana   wanasaidia kuzima moto huo.

Kiabo amesema jitihada za kuuzima moto huo zinaendelea vyema ili kuuzuia usisambae kwenye vyanzo vya maji na makazi ya watu jirani na mlima.

Mkazi wa mji mdogo wa Katesh, Magreth John amesema matukio ya  kuzuka moto katika eneo hilo yanapaswa kuchukuliwa tahadhari kwani unaathiri mlima Hanang.

Amesema katika miaka ya hivi karibuni hii ni mara ya tatu kutokea kwa moto katika mlima huo, unaosababishwa na kufanyika kwa shughuli za kibinadamu ikiwemo warina asali.

Usiku wa kuamkia Desemba 3,2023 kulitokea maafa katika mlima Hanang ambapo zaidi ya watu 100 walifariki dunia kwa kusombwa na maji, matope na majabali yaliyotokea katika mlima huo.