Ile siku ndo leo! Ni vita ya Ibenge, Matola Kwa Mkapa

WENGI wanaamini Mzizima Derby huwa ni vita vya wanandugu, lakini ukweli hili ni pambano la kukata na shoka baina ya Simba na Azam FC na baada ya kupiga danadana kwa sababu hizi na zile, sasa ngoma inapigwa leo kuanzia saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Simba na Azam zimekuwa zikinasibishwa udugu, kutokana na ukweli bilionea wa matajiri wa Chamazi, Said Salim Bakhresa amewahi kuwa kiongozi na mfadhili wa Simba miaka ya 1980.

Hata hivyo, bado Dabi hiyo si mechi ya kuchukuliwa poa, licha ya madai hayo ya ‘uswahiba’ wa timu hizo umekuwa ukichangia kuifanya Azam isiikazie sana Simba tofauti na ikikutana na Yanga.

Ukiachana na tuhuma hizo na hata rekodi zinaonyesha jinsi Azam inavyoteseka mbele ya Simba, lakini bado ukweli unabaki kuwa, Mzizima Derby ni mechi ngumu na kubwa katika Ligi Kuu.

Kama hujui ni kwamba, timu hizo zinakutana leo katika mechi ya 35 ya Ligi Kuu tangu 2008, huku  Simba ikiwa na kaimu kocha mkuu, Seleman Matola wakati Azam ikiwa na Florent Ibenge.

Licha ya kuwa chini ya makocha wenye uzoefu na dabi hiyo, lakini klabu hizo zimesajili mashine mpya vikosini ambazo baadhi zimeshawasha moto katika mechi za Ligi Kuu na michuano ya CAF.

Kumbuka Simba na Azam ni kati ya timu nne za Tanzania zilizofuzu makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.

Azam imefuzu makundi kwa mara ya kwanza katika Kombe la Shirikisho sambamba na Singida Black Stars, wakati Simba imeendeleza rekodi sawia na Yanga katika Ligi ya Mabingwa na zote yaani Simba na Azam zimeanza na vipigo vya mechi mbili mfululizo katika makundi yao.

Kwa mechi za Ligi Kuu, timu hizo mara ya mwisho kukutana msimu uliopita zilishindwa kutambiana kwa kutoka sare ya mabao 2-2, Azam ikichomoa bao dakika za jioni kabisa.

Pambano hilo lililopita lilijaa msisimko kwani lilikuwa ni moja la mechi zilizokuwa zimeshikilia hesabu za mbio za ubingwa ambao hata hivyo ulinyakuliwa na Yanga kwa msimu wa nne mfululizo, ikishinda Dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba.

Asikuambie mtu, pambano baina ya Azam na Simba lina mvuto na msisimko, kiasi huziweka juu juu roho za mashabiki kutokana na ushindani uliopo baina ya timu hizo tangu Azam ipande Ligi Kuu mwaka 2008.

Ingawa timu hizi zimekuwa zikikutana na kuonyeshana kazi katika michuano mbalimbali ikiwamo ile ya Ngao ya Jamii, Kombe la Shirikisho (FA), Mapinduzi, Kombe la Muungano na Kombe la Kagame, hapa chini Mwanaspoti inakuletea rekodi kadhaa za michezo 34 ya ligi baina ya timu hizo tangu msimu wa 2008-2009, pale Azam ilipopanda daraja.

Katika michezo 34 zilizochezwa baina ya timu hizo, Simba ndio inayoonekana kuwa wababe zaidi mbele ya Azam kwa takwimu mbalimbali.

Simba imeshinda michezo mingi zaidi mbele ya Azam, ikifanya hivyo mara 15 dhidi ya sita tu ya Wanalambalamba, huku ikiongoza pia kwa idadi ya mabao ya kufunga ikiwa na 48 dhidi ya 31 ya wageni wa mchezo, yaani Azam.

Rekodi zinaonyesha timu hizo zimeshindwa kutambiana katika mechi 13 iliyoisha kwa sare tofauti, huku Simba ikivuna jumla ya pointi 58 katika michezo yote 34 dhidi ya 31 za wapinzani wao ambao msimu uliopita ilichezea kichapo cha mabao 2-0 katika mechi ya kwanza iliyochezwa New Amaan Complex, visiwani Unguja Zanzibar.

Simba imepoteza mechi nne ikiwa nyumbani, huku ikitoka sare sita ikiwa wenyeji, wakati ni mechi mbili tu ndizo ilizopoteza ikiwa ugenini na kutoka sare saba ikicheza huko.

Hali ni tofauti kwa Azam kwani imepoteza michezo nane nyumbani sawa na imepoteza saba ugenini na pia kupata sare saba wakiwa wenyeji, ilihali imeambulia sare sita ugenini mbele ya Simba.

Ni mara tatu timu hizo katika Ligi Kuu zimekutana nje ya Dar es Salaam baada ya lile la Sept 11, 2010 uliopigwa Uwanja wa Mkwakwani Tanga, uliotumiwa kama Uwanja wa nyumbani wa Azam na timu hiyo kulala 2-1 mbele ya Mnyama.

Mechi nyingine iliyopigwa nje ya Dar ni ile ya msimu uliopita lililochezwa Februari 9, 2024 ambapo Simba ikiwa wenyeji waliupeleka CCM Kirumba, jijini Mwanza na kumalizika kwa sare ya 1-1, Mnyama akichomoa dakika za lalasalama bao la Prince Dube kupitia Clatous Chama na msimu uliopita zilienda kuvaana visiwani Zanzibar, Azam ikiwa wenyeji walilala 2-0. Mabao ya mchezo huo yaliwekwa kimiani na Leonel Ateba na Fabrice Ngoma.

Na kama hujui ni kwamba pambano moja tu baina ya timu hizo katika Ligi Kuu liliwahi kulazwa kiporo na kulazimika kuchezwa siku mbili, likiwa ni ule uliopigwa Mar 30, 2009, ambapo kwanza ulipigwa siku moja na kushindwa kumalizika kutokana na mvua kubwa na kurudiwa kesho yake na Azam iliyokuwa wenyeji wa mchezo huo wa marudiano kwa msimu wa 2008-2009 ikalala mabao 3-0.

Katika mechi hizo 34 zilizopigwa hadi sasa wanaume hao wamezalisha jumla ya mabao 77, ikiwa ni wastani wa kila mechi moja kuzalisha mabao 2.26, huku Simba ikiongoza kwa kufunga mabao 48 ikiwa ni wastani wa kufunga mabao 1.41 kwa kila mchezo, huku Azam yenye mabao 31 ikiwa na wastani wa 0.91 ya bao kwa kila mechi hizo 34 ilizocheza hadi sasa.

Ni mapambano mawili tu yaliyowahi kuzalisha mabao mengi kwa kila dakika 90, likiwamo lile la Januari 23, 2011 ambapo Simba iliifunga Azam kwa mabao 3-2, kisha Azam nayo ikaja kufanya kama hivyo Machi 4, 2020 ilipoichapa Simba pia kwa mabao 3-2.

Huku ni msimu mmoja tu wa 2017-2018 uliozalisha idadi ndogo ya mabao kwa kufungwa bao moja wakati Simba iliposhinda bao 1-0 katika mechi ya marudiano, huku ile ya kwanza ikiisha kwa suluhu, ilihali msimu wa 2010-2011 na ule wa 2012-2013 ndio pekee iliyozalisha mabao mengi kwani kila moja ulishuhudiwa yakifungwa mabao manane kupitia mechi mbili za kila msimu.

Na wachezaji wawili pekee waliowahi kujifunga katika michezo hiyo 34 iliyopita kwa timu hizo katika ligi wote wakiwa ni mabeki wa kati wa Azam, akianza Aggrey Morris Machi 14, 2010 wakati Azam ikilala mabao 2-0, kisha akafuata Abdallah Kheri ‘Sebo’ Februari 21, 2023 wakati akiisawazishia Simba bao dakika ya 90 katika harakati za kuokoa shuti la Kibu Denis.

Rekodi zinaonyesha kuwa, winga wa zamani wa kimataifa aliyewahi kukipiga katika hizo mbili, Jamal Mnyate ndiye mchezaji wa kwanza kufunga bao katika Dabi ya Mzizima.

Mnyate alifunga bao katika pambano la kwanza kwa timu hizo msimu wa 2008-2009 mchezo uliochezwa Oktoba 4, 2008 ambapo Simba ilicharazwa nyumbani 2-0. Mnyate enzi hizo akiwa Azam alifunga katika dakika ya 42 kabla ya Shekhan Rashid  aliyewahi pia kuichezea Simba, kuongeza la pili kwa penalti dakika ya 90+5 na kuwapa Wanalambalamba ushindi huo mtamu.

Rekodi zinaonyesha pia, Mkenya Mike Barasa ndiye mchezaji wa kwanza kufunga mabao mawili katika pambano moja baina ya timu hizo akifanya hivyo katika mechi ya Machi 14, 2010 wakati Simba ikishinda ugenini mabao 2-0.

Ukiachana na rekodi hizo, nahodha aliwahi kuziongoza timu hizo kwa vipindi tofauti, John Bocco ‘Adebayor’ ndiye anayeongoza orodha ya kufunga mabao mengi zaidi, akitupia mabao manane, akifunga sita kipindi akiwa Azam na kuongeza mawili alipokuwa Simba iliyomtema msimu huu.

MK 14, Meddie Kagere aliyekuwa Simba anafuata kwa kufunga jumla ya mabao matano, akiwa ndiye mchezaji aliyeitesa Azam kwa miaka ya karibuni kwa kufunga mfululizo, akifuatiwa na Kipre Tchetche aliyefunga mabao manne enzi akiichezea Azam hadi anaondoka.

Prince Dube aliyepo Yanga kwa sasa ndiye anayefuata akiwa na mabao matatu akifuata nyayo za Kagere za kufunga mfululizo timu pinzani.

Timu hizo zinakutana kwa mara ya kwanza msimu huu, huku kila moja ikiwa chini ya kocha tofauti na wale wa msimu uliopita na sura za wachezaji tofauti ambao wamepewa nafasi kubwa ya kuamua matokeo.

Simba ina kaimu kocha mkuu, Seleman Matola atacheza mechi ya kwanza dhidi ya Azam lakini ya pili baada ya kuiongoza mbele ya Fountain Gate na kushinda 3-0.

Matola ambaye ni mzoefu klabuni ataendelea kuwategemea kipa Yacoub Suleiman na Hussein Abel kutokana na kipa namba moja, Moussa Camara, Ellie Mpanzu, Jean Charles Ahoua, Rushine de Reuck, Nady Camara, Neo Maema, Jonathan Sowah, Kibu Denis, Seleman Mwalimu na wengine walio na viwango bora kwa sasa.

Ahoua aliyemaliza kama kinara wa mabao wa Msimbazi na Ligi Kuu kwa msimu uliopita hadi sasa katika mechi nne zilizopita amefunga bao moja na asisti moja kama aliyonayo Maema, Yusuf Kagoma na Joshua Mutale.

Beki wa kati Rushine ana mabao wawili, huku Sowah akiwa kinara akitupia matatu wakati Chamou Karaboue na Seleman Mwalimu kila mmoja akiwa na moja.

Ahoua, Sowah, Mwalimu, Maema, Mutale na Ellie Mpanzu sambamba na Kibu Denis watakuwa na kazi ya kuisumbua ngome ya Azam chini ya Yeison Fuentes, Yoro Diaby na viungo wanaojua soka, Sadio Kanoute, Yahya Zayd, James Akaminko na Feisal Salum ‘Fei Toto’ anayeongoza kwa mabao kwa timu hiyo akiwa na mawili.

Hata hivyo, Azam sio timu ya kubezwa, kwani chini ya Ibenge imeonekana inajitafuta kwani katika mechi nne imeshinda moja na kutoka sare tatu ikiwamo iliyopita ilipolazimishwa suluhu na Singida Black.

Timu hiyo iliyomaliza nafasi ya tatu katika Ligi Kuu iliyopita nyuma ya Yanga na Simba zilizokamata nafasi ya kwanza na ya pili itaendelea kumtegemea Fei Toto, mwenye rekodi nzuri na bahati ya kuitungua Simba tangu alipokuwa Yanga.

Pia kuna kuna Paschal Msindo, Idd Seleman ‘Nado’, Nassoro Saadun, Abdul Suleiman ‘Sopu’, mbali na straika mpya linalojua kutupia nyavuni, Japhte Kitambala na wengineo.

Ni wazi makocha na wachezaji wa timu zote mbili wanajua ugumu wa pambano hilo na hivyo kujiweka vizuri kuwapa raha mashabiki wao bila kujali matokeo ya mechi 34 zilizopita.

Ushindi wowote kwa timu mojawapo utakuwa mwanzo mzuri kwa Matola na Ibenge, kwani hili ni pambano la awali la Dabi ya Mzizima na wasingetamani kuanza na mguu mbaya.

Msimu uliopita Fadlu Davids alianza na mguu mzuri kwa kushinda ugenini kwa mabao 2-0 mbele ya Rachid Taoussi wa Azam aliyepokea kipigo kisha kuambulia sare ya 2-2 ziliporudiana.

Azam 0-0 Simba               

Azam 0-2 Simba (Zanzibar)

Simba 3-0 Mbeya City (Ligi Kuu)

Stade Malien 2-1 Simba (CAF)

Simba 0-1 Petr Atletico (CAF)

JKT TZ 1-2 Simba (Ligi Kuu)

Simba 0-0 Nsingizini (CAF)

v Mtibwa Sugar (Ligi Kuu)

Azam 0-0 Singida BS (Ligi Kuu)

Namungo 1-1 Azam (Ligi Kuu)

v Coastal Union (Ligi Kuu)