Dodoma. Huenda umewahi kukutana na mtu anayefanya kitu kwa umahiri mkubwa lakini bado anakuwa na wasiwasi. Huenda wewe ni mmoja wao.
Unafanya kitu vizuri tu lakini bado unahisi hujafanya kama ulivyotarajiwa kufanya. Muda wote unajihisi kama umepungua. Hakuna sifa unayoweza kupewa na ukaipokea. Huamini kuna jema unaweza kulifanya.
Kutojiamini, kwa muktadha wa makala haya, ni ile hali ya kukosa ujasiri, kujihisi umepungua na kutokuwa na imani na uwezo wako mwenyewe.
Maisha yanakuhitaji kujiamini. Huwezi kuaminika ikiwa wewe mwenyewe hujiamini. Unapokosa imani na uwezo wako mwenyewe si tu msukumo wa kupambania malengo yako unazorota, lakini pia unaweza kupata shida kuhusiana na watu unaowahitaji kufikia malengo unayojiwekea.
Hatuzaliwi tukijiamini. Kujiamini ni matunda ya malezi. Ili uweze kufanikiwa kumjengea mtoto imani na uwezo wake mwenyewe, ni muhimu kuelewa viashiria vya mtoto asiyejiamini na chanzo chake.
Viashiria vya kutojiamini
Kwanza kabisa, mtoto asiyejiamini, ana tabia ya ‘kumganda’ mzazi/mlezi kupita kiasi. Anapohisi dalili za kuachwa, hali ya hewa hubadilika. Katika umri wa miaka miwili, mathalani, anapotengwa na mzazi wake atalia na inaweza kumchukua muda mrefu kunyamaza.
Pili, ana tatizo la kudeka kwa kulialia bila sababu. Ingawa si mgomvi anapokuwa na wenzake kinachochosha ni wingi wa mashitaka dhidi ya wenzake. Hawezi kutatua matatizo yake bila kushitaki.
Lakini pia kuna suala la ukimya hasa anapokuwa kwenye umri wa kwenda shule. Ingawa si kila mtoto mkimya hajiamini, mara nyingi, ukimya huashiria woga na wasiwasi wa kutoeleweka na watu. Kwa msingi huo ni nadra kujichanganya vizuri na wenzake. Hana imani kuwa ataeleweka.
Hata hivyo, wapo watoto wasiojiamini wanaokuwa na tabia ya kupenda sana kuwa na watu. Msukumo wa kupenda ‘kujichanganya’ na watu, ni utoshelevu wao kutegemea watu na hivyo wanakuwa na shauku kubwa ya kutaka kuwapendeza na kuwaridhisha wengine.
Mtoto asiyejiamini anaweza kupatwa na ‘dhoruba’ nyingi anapoingia kwenye kipindi cha baleghe. Kutojiamini kunaweza kumtenganisha na wazazi wake na kunaweza kumwingiza kwenye matatizo ya kuanza mapenzi mapema kama namna ya kupata utulivu.
Kutojiamini kunachangiwa na mambo kadhaa. Kwanza, ni kutotabirika kwa upendo anaoupata kwa wazazi. Ingawa mtoto huyu huwa ana bahati ya kuwa na wazazi wenye upendo, changamoto ni kutokuwa na uhakika afanye nini kuupata upendo huo unaopatikana kwa nadra.
Kwa upande mwingine, inawezekana mzazi huyu mwenye upendo anapatikana kimwili, lakini kihisia ni kama vile hayupo. Huyu ni mzazi asiyejali hisia za mtoto, mazingira yanayomchanganya mtoto asielewe ni wakati upi anaweza kubahatisha ‘urafiki’ usiojulikana utapatikana lini.
Lakini pia inawezekana mzazi huyu ni mkosoaji kupindukia. Ingawa ni mzazi mwenye utulivu na asiyetumia nguvu, inawezekana kaweka viwango vya juu mno vinavyomwia ugumu mtoto kuvifikia. Huyu ni mzazi mgumu kumridhisha kwa sababu usipofikia viwango vyake, ni sawa na hujafanya kitu.
Sambamba na hilo, inawezekana pia mzazi anamdekeza mno mtoto na hajampa nafasi kufanya vitu bila msaada kwa imani kuwa ‘mtoto hawezi kuteseka wakati mimi nipo.’
Huyu ni mzazi anayeamini mtoto kufanya vitu fulani ni kumsumbua. Mtoto asiyepewa fursa ya ‘kuhangaika kidogo’ huishia kukosa imani na uwezo wake.
Kwanza, ni vizuri kuelewa kuwa upendo kwa mtoto si zawadi. Mtoto hahitaji kufanya jitihada za ziada kuupata upendo wako kama mzazi. Unampenda mtoto kwa sababu ni mwanao na si kwa mema anayofanya.
Pili, hakikisha unapatikana kimwili na kihisia. Hata katika mazingira ambayo umebanwa na shughuli nyingi, tengeneza utaratibu wa kutabirika wakati upi unakuwepo. Unapopatikana, hakikisha unapatikana kweli kihisia. Mpe mtoto nafasi ya kukupata kwa mazungumzo na michezo. Usimfanye mtoto afanye kazi ya ziada ‘kukupata’ wakati upo.
Lakini pia usimdekeze mtoto kwa maana ya kumpa zaidi ya anachohitaji. Kumdekeza mtoto kunamuondolea kujiamini kwake. Punguza kumwonea huruma mtoto. Mwache afanye vitu kwa uhuru wake bila kumpa msaada mkubwa.
Pia, epuka kumkosoa kupindukia. Punguza matarajio. Mpe mtoto nafasi ya kukosea na msaidie kujiwekea malengo yanayosadifu uwezo alionao. Hata pale anaposhindwa kuyafikia, mtie moyo. Anapofanikiwa, hata kwa sehemu, tambua na mpongeze.