Kimiti: Kuandamana siku ya Uhuru ni kumvunjia heshima Mwalimu Nyerere

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere, Paul Kimiti amewataka wanaopanga kuandamana Desemba 9, 2025 kuacha hatua hiyo, akisema wakifanya hivyo watamvunjia heshima mwasisi wa Taifa hili.

Kimiti aliyewahi kuwa waziri na mkuu wa mkoa kwa nyakati tofauti, amesema Desemba 9 ni siku ambayo Tanzania ilipata Uhuru wake, hivyo si vyema kufanya maandamano hayo kwa kuwa tarehe hiyo ina historia kubwa katika Taifa.

Mwanasiasa huyo mkongwe, ametoa kauli hiyo leo Jumapili Desemba 7, 2025 wakati akizungumza na wanahabari nyumbani kwake Ununio kuhusu masuala mbalimbali yanayoendelea nchini.

“Desemba 9 ni siku ya kuomba na kushukuru Mungu ya kwamba tunalinda uhuru, umoja, amani na usalama wa Taifa letu. Tuendelee kumuomba Mungu huko aliko na Mwalimu (Nyerere) atatuombea,” amesema Kimiti.

Wakati Kimiti akitoa rai hiyo, tayari polisi limeshatangaza kupiga marufuku maandamano hayo yanayodaiwa kupangwa kufanyika Desemba 9, ikisema yamekosa nguvu ya kisheria kufanyika ikiwemo wahusika kutotoa taarifa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Mbali na hilo, jeshi hilo kupitia msemaji wake, David Misime lilikwenda mbali zaidi likibainisha mambo 12 inayodai yanaendelea kupangwa mitandaoni kuelekea Desemba 9, 2025, likiwaonya wanaopanga na kuhamasisha vitendo vya uvunjifu wa amani siku hiyo kuachana navyo, la sivyo watashughulikiwa.

“Nimesikia vyombo vya habari vikitangaza kuwa viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, wapo tayari kusimamia usalama siku hiyo. Imeniuma sana kwa Watanzania tumefikia hapo, shetani gani ameingia katika nchi yetu kufanya mambo hayo siku ya heshima (Desemba 9) au kuna watu wa nje wanataka kutuvuruga? amehoji Kimiti.

Kimiti amewataka viongozi wa dini ikiwemo ya Kikristo kukemea hali hiyo, akisema Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere imechukua jukumu ya kuzungumza na wadau wake ili kuhakikisha jambo hilo halitokei.

Katika hatua nyingine, Kimiti amewataka Watanzania kutoa ushirikiano kwa Tume ya uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu, ikiwamo kutoa taarifa zitakazowezesha tume hiyo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

“Hii Tume ambayo Rais (Samia Suluhu Hassan) ameiunda, tusiwe waoga kuipelekea taarifa yoyote ile, tuisaidie ifanye kazi yake vizuri. Kama mambo mengine mnayo (wananchi) hamna pakupeleka, yapelekeni Tume ili ikitoa taarifa iwe ya uhakika itakayotusaidia kutuondoa hapa tulipo,” amesema Kimiti.