Maombi nguvu ya ndoa iliyosahaulika kwa wenza

Mwanza. Katika zama hizi ambapo takwimu za kuvunjika kwa ndoa zinazidi kupanda, mijadala kuhusu nini kimetokea kwenye misingi ya familia imekuwa mingi, lakini wachache wanagusia chanzo kikuu cha kukosekana kwa nguvu ya maombi ndani ya ndoa.

Viongozi wa dini na wataalamu wa masuala ya kijamii wanasema, ndoa nyingi zimepoteza ladha ya kiroho na kugeuzwa kuwa makubaliano ya kijamii badala ya ibada ya kiimani.

Imamu wa Msikiti wa Ibadhi mkoani Mwanza, Sheikh Baarut Zaid anasema tatizo kubwa katika ndoa za leo ni kwamba Mungu hatangulizwi mbele.

Anasema, kwa mujibu wa mafundisho ya Mtume Muhammad (Rehma na amani zimshukie), ndoa si tukio la kijamii tu bali ni ibada inayoambatana na dua tangu mwanzo wake.

“Mtume  anatufundisha kwamba mwanaume anapofunga ndoa na kwenda ndani kwa ajili ya kumchukua mke wake, anatakiwa amshike kichwa na kumuombea dua; ‘Mwenyezi Mungu nakuomba unipe kheri yake na unikinge na shari yake.’ Dua hii ni kumbukumbu kuwa ndani ya kila neema kunaweza kuwepo na shari,” anasema.

Anabainisha kuwa hata baada ya kufunga ndoa, Waislamu wanafundishwa kuswali rakaa mbili wanapoingia nyumbani kwa mara ya kwanza kama wanandoa, ili kuanza maisha yao kwa kumkabidhi Mwenyezi Mungu ndoa hiyo.

“Baada ya hapo utamchukua mke wako ukimfikisha nyumbani kwako unasali rakaa mbili yote hii ni kuendelea kumuomba dua Mwenyezi Mungu aidumishe ndoa yenu na iepukane na shari,”anaeleza.

Katibu wa Baraza la Masheikh Mkoa wa Mwanza, Sheikh Othmani Masasi anasisitiza kuwa ndoa katika Uislamu, ni ibada yenye uzito mkubwa hadi kufananishwa na nusu ya imani.

Anaeleza kuwa sababu nyingi za kuvunjika kwa ndoa za leo zinatokana na wanandoa kuacha na kupuuzia maombi.

“Siku hizi maombi yameachwa. Wanandoa hawasali pamoja, hawaombi wanapokula, hawamuombi Mungu wanapotoka kazini wala wanaporudi. Ni mara chache sana utakuta mke anamuombea mume wake au mume anamuombea mke wake,” anasema Sheikh Masasi.

Anaongeza kuwa hali hiyo imesababisha mifarakano, migogoro, na hata kuvunjika kwa familia, kwani maombi ndiyo ngao ya upendo na subira katika ndoa.

“Leo tumeona ndoa zikivunjika kirahisi, watoto kulelewa bila maadili, na wanaume wengi kukosa wajibu wao kama viongozi wa familia. Wanawake wanalazimika kubeba majukumu yote kutoka kutafuta riziki hadi kulea watoto. Hii yote ni matokeo ya kuikosa nguvu ya maombi ndani ya nyumba,” anasema Sheikh Masasi na kuongeza:

 “Utaona nguvu ya maombi katika ndoa ni jambo kubwa na adhimu sana na kwakuwa sasa limesahaulika, ndoa imechukuliwa kama jambo la dharura halina umuhimu zaidi na ndio mana kila mmoja anaweza kuishi anavyotaka bila kufuata misingi.

Ndiyo leo tunakutana na kesi nyingi za ndoa kuliko kesi zingine zozote wake wakiomba talaka pia wapo na wanaume ambao wanafika ofisini kwetu wakitaka kuwaacha wake zao.” 

Sheikh Masasi anasema hata malezi ya watoto yameathirika kwa kukosekana kwa maombi ndani ya ndoa na familia, hivyo kuzalishwa kizazi cha watoto watukutu na wasiyo na maadili.

“Wazazi wengi leo wanatumia maneno mabaya kwa watoto wao, bila kujua malaika wanaitikia kila dua hata ile ya matusi. Ndiyo maana tunapata watoto wasiosikia, wasio na heshima, kwa sababu wamelelewa nje ya maombi,” anasema.

Mhubiri, Mwalimu Peace Marino kutoka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Ebeneza Nyashimo, Jimbo la Kaskazini mkoani Simiyu, anakubaliana na umuhimu wa maombi, lakini anasisitiza kuwa maombi yanahitaji kuambatana na utii na unyenyekevu hasa kutoka kwa mwanamke.

“Ni sawa tunatakiwa kuomba sababu kinamama ni walinzi hapo kuna vifungu vya Biblia vinavyoonesha Mungu ameumba kitu kipya mwanamke atamlinda mume wake.

Kweli tunatakiwa kulinda kwenye maombi. Lakini ambacho tungeweza kusisitizana mama akiamua ndoa yake isimame inasimama hata kama mume awe mkorofi kiasi gani. Biblia imesema mwanamke anatakiwa kuwa mtiifu, shida inapoanzia ni pale kwa mwanamke kutotii,”anasema na kuongeza: 

“Ni kweli tunatakiwa kuomba sana ili ndoa ziende lakini zaidi ya maombi ni lazima kila mtu atambue nafasi yake. Yaani baba asimame katika nafasi yake na mama asimame katika nafasi yake…lakini aliye na uwezo wa kuokoa ndoa ni mama.”

Anasema mahali popote kwenye ndoa ambapo mwanamke ni mtiifu, mnyenyekevu na muombaji basi ndoa hiyo haiwezi kuvunjika, kwa sababu kuna namna mama anaweza kumsaidia baba kukaa kwenye mstari pasipo hata yeye kujua.

“Hakuna kinachoshindikana kwenye maombi lakini ni ngumu kumuombea mume wako wakati umemchukia, yaani anapokukosea ukajenga chuki kwake hata hayo maombi hayawezi kufanya kazi,”anaonya.

Naye Mchungaji wa Kanisa la Waadventista Wa Sabato mkoaniTabora, Joel Josephat anasema maombi si jambo la hiari;  ni msingi wa kudumu wa ndoa kwakuwa yanajenga mawasiliano, yanazalisha rehema na kusafisha mioyo ya wanandoa.

“Bila maombi, chuki na kiburi huchukua nafasi, na hapo hata mapenzi makubwa yanayeyuka.Hakuna kinachoshindikana kwenye maombi, lakini ni lazima kila mmoja atambue nafasi yake”anasema.

Anaeleza ndoa ni zaidi ya makubaliano ya wawili kupendana, kwani ni safari ya kiimani inayohitaji maombi kila hatua.

Anashauri jamii ya wanandoa irudi kwenye misingi ya kumuomba Mungu pamoja, kumshukuru, na kumtanguliza mbele katika kila jambo akieleza huenda kikaonekana kizazi kipya cha ndoa zenye utulivu, upendo na baraka za kweli.

Mtaalamu wa masuala ya familia, Grace Malusu anasema, maombi si tu ibada bali ni tiba ya kihisia na kiroho na kwamba , yanapofanyika kwa dhati,  huleta hali ya unyenyekevu, kusamehe, na kujifunza kuvumilia upungufu wa mwenza wako.

“Kila mtu ana upungufu. Maombi yanakufundisha kuyavumilia na kuona mema zaidi ya mabaya,” anasema Malusu.