Dar es Salaam. Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema Tanzania inajimudu kuendesha bajeti kuu ya Serikali bila kutegemea msaada kutoka nje, hata ikitokea msaada huo umekosekana.
Msigwa amesema hayo jana, Jumamosi Oktoba 6, 2025, alipozungumzia masuala mbalimbali ya kitaifa katika mahojiano maalumu na kituo cha televisheni cha Star TV.
Akizungumzia mjadala wa kujitegemea kufuatia matamko ya mataifa na taasisi za kimataifa kuinyima misaada Tanzania, Msigwa amesema bajeti ya Serikali ni takribani Sh56.49 trilioni, Kati ya hizo, Sh40.47 trilioni zinatokana na makusanyo ya ndani.
Amesema misaada ni Sh1.07 trilioni pekee, huku mikopo ikiwa ni Sh14.95 trilioni, hali inayotoa uhakika wa nchi kujitisheleza bila misaada hiyo.
“Ni kweli tunahitaji misaada na ushirikiano, lakini si kwamba hatuwezi kuishi bila misaada,” amesema.
Amefafanua kuwa hata mikopo inayochukuliwa hulipwa, hivyo kwa mantiki hiyo bado nazo ni fedha za Taifa, siyo msaada.
“Katika trilioni 56, trilioni 40 ni za makusanyo yetu, trilioni 14 ni mkopo tunaokopa na kuulipa, kwa hiyo, nazo ni fedha zetu,” amesema.
Msigwa amesisitiza kuwa Sh 1.7 trilioni pekee ndiyo misaada ya moja kwa moja, na kwa uwiano huo amesema hakuna mantiki ya kudai kuwa nchi haiwezi kuendelea bila msaada.
Kauli hiyo ya Msemaji Mkuu wa Serikali imekuja wakati ambapo mataifa mbalimbali ya Ulaya na Marekani yameendelea kutoa matamko yakionesha kudhoofika kwa uhusiano wake na Tanzania, hali inayotishia uwezekano wa mataifa hayo kusitisha kutoa misaada kwa Tanzania.
Aidha, hivi karibuni, Bunge la Ulaya (EU) lilipitisha azimio la kusitisha misaada kwa nchi ya Tanzania, hatua inayoonesha huenda misaada ya mataifa hayo ikapungua au kutokupatikana kabisa kwa mwaka huu wa fedha.
Tayari Rais Samia Suluhu Hassan alishatangaza mikakati ya kujiandaa kukabiliana na hatua hiyo alipohutubia Bunge na alipowaapisha mawaziri wapya aliowateua, ambapo alitoa wito wa kufunga mikanda ili Taifa litekeleze mipango yake hata kama kutakuwa na kukosekana kwa misaada hiyo.
Akifafanua kauli hiyo ya Rais kuhusu kufunga mkanda kufuatia kukosa misaada ya kimataifa, Msigwa amesema Rais alilenga kuhimiza maandalizi ya ndani kuhakikisha nchi inajitosheleza endapo misaada hiyo ya Sh1.7 trilioni haitapatikana.
“Ukikosa ile Sh 1.7 trilioni ya msaada lazima uweke utaratibu wa kuziba pengo hilo kwa vyanzo vingine,” amesema.
Msigwa amewataka Watanzania kuwa macho dhidi ya juhudi zinazolenga kuichafua nchi kwa kutumia hoja za haki kama kigezo.
Amesema baadhi ya wanaolikosoa Taifa sasa wamefikia hatua ya kupinga watalii na wawekezaji kuja nchini, badala ya kutaja mambo wanayolalamikia.
“Walitumia kigezo cha haki, lakini sasa wanapinga watalii wasije na wawekezaji wakimbie, hicho ndicho walichokuwa wanataka,” amesema.
Msigwa amesema Tanzania ipo katika hatua kubwa za maendeleo ikielekea kwenye uchumi wa mafuta na gesi, uwekezaji wa bandari za Bagamoyo mkoani Pwani na Dar es Salaam, reli ya kisasa ya SGR pamoja na nishati ya umeme, akitaja kuwa haya ni mambo yanayovutia maadui.
Aidha, amesema vyombo vya habari vinawajibu wa kiusalama katika kulinda na kutetea maslahi ya Taifa.
Pia, amefafanua kuwa katika maudhui yake, kila chombo kinapaswa kuwa na mkakati wake juu ya nini kinalenga, akifafanua kuwa kuishambulia Serikali kwenye vyombo vya habari kunakofanywa na vyombo vya nje ni sehemu ya mkakati wa kuichafua nchi, akisisitiza vyombo vya ndani kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia amani na usalama wa Taifa.
Msemaji huyo wa Serikali amesema kuandika makala au taarifa zinazohukumu Serikali kwa kunukuu wanaharakati tu bila kuipa Serikali nafasi ya kujieleza si tu ni kinyume cha taaluma hiyo, bali pia ni sehemu ya mkakati wa kuichafua nchi.
Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amesema uandishi wa habari unapaswa kuzingatia haki, mizani na usikilizaji wa pande zote.
“Huwezi kuandika makala kwa kuhukumu Serikali kwa kunukuu wanaharakati tu bila kuishirikisha kupata maelezo yake,” amesema.
Akizungumzia maudhui ya picha na video ambayo yamekuwa yakisanbazwa na vyombo vya habari vya nje, kikiwemo CNN, Msigwa amesema baadhi ya picha na video zilizosambazwa hivi karibuni hazikuwa sahihi, akieleza kuwa nyingine ni za kutengenezwa, nyingine zimetoka nchi nyingine na baadhi ni za zamani.
“Picha na video hizo lazima zihakikiwe, maana tumeziona zina kasoro nyingi. Baadhi ni matukio ya zamani, nyingine ni za nchi nyingine na pia nyingine ni za kutengenezwa,” amesema.
Msigwa amesema Serikali imekuwa ikiipa sekta ya habari ushirikiano wa kutosha tangu ateuliwe kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali.
“Tangu nimekuwa Msemaji Mkuu wa Serikali mwaka 2021, kazi yangu imekuwa kuwezesha vyombo vya habari kufanya kazi yao vyema,” amesema.
Ameongeza kuwa endapo mwandishi yoyote anakwama kupata taarifa, yuko tayari kusaidia moja kwa moja, akikosoa baadhi ya waandishi wa habari wanaolalamikia kukosa taarifa kutoka serikalini kwa kukosa ushirikiano wa mamlaka za Serikali wanapotaka ufafanuzi.
Akisifu uzalendo wa vyombo vya ndani, Msigwa amesema vyombo vya habari vya ndani viliripoti matukio ya Oktoba 29, kwa uwajibikaji na kwa kuzingatia masilahi ya Taifa.
“Wewe Tanzania imepata tatizo, utafurahi kuisema vibaya ichafuke? Vyombo vya habari duniani kote vinafanya kazi kwa ajenda za kulinda masilahi ya nchi zao,” amesema.
Amesisitiza kuwa chombo cha habari ni sehemu ya mfumo wa kiusalama wa nchi, hivyo, waandishi wanapaswa kujiuliza wajibu wao kwa taifa kupitia kazi zao.
Taasisi za dini zakumbushwe wajibu wake
Akiizungumzia nafasi ya taasisi za dini, Msigwa amesema Serikali inatarajia viongozi wa dini kuendeleza misingi ya haki, amani na upendo, si kugawa au kuchochea chuki.
“Ukisikia kiongozi wa dini anahubiri chuki, unajiuliza sasa huyu au amesahau amri kuu ya Mungu?” amesema.
Amesisitiza kuwa sheria zipo wazi na uchochezi wowote hauwezi kuvumiliwa.
Tangu matukio ya Oktoba 29, kumekuwa na matamko mbalimbali ya viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali wakitoa ushauri na msimamo wao kufuatia ghasia hizo.
Matamko hayo yamekuwa yakisisitiza Serikali kuchukua hatua mbalimbali, zikiwemo za kumaliza tatizo hilo na kuendesha maridhiano ya kuunganisha Taifa.
