Ni dhahir sasa, Gamondi haiwezi TRA United

KOCHA wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi ni kama haiwezi TRA United (zamani Tabora United) baada ya jana jioni kuendeleza rekodi mbovu mbele ya Watoza Ushuru hao kwa kukubali kichapo cha mabao 3-1 kwenye Uwanja wa KMC Complex Mwenge jijini Dar es Salaam.

Kama hujui TRA enzi ikiwa Tabor United ndio iliyompoza Gamondi akapoteza kibarua chake akiwa Yanga iliyokubali kichapo cha mabao 3-1 ikiwa ni siku chache ilipofungwa bao 1-0 na Azam FC iliyowatibulia rekodi ya kucheza mechi nane mfululizo bila kupoteza wala kuruhusu bao lolote.

Safari hii akiwa Singida amekutana na wababe wao hao na kukubali kichapo hicho kinachokuwa cha kwanza kwa timu hiyo msimu huu katika Ligi Kuu Bara kwa mabao ya Chanda Chewe dakika ya 10, Shaaban Idd Chilunda dakika 82, huku beki Anthony Tra Bi Tra akijifunga dakika ya 87, wakati bao la Singida lilifungwa na Clatous Chama kwa penalti dakika ya 54.

GAMO 01

Ushindi huo kwa TRA unakuwa ni wa pili msimu huu katika mechi saba ilizocheza, baada ya kutoka sare mitatu na kupoteza miwili, huku kwa upande wa Singida, ikishinda miwili, sare miwili na kuchapwa mmoja kati ya mitano iliyocheza hadi sasa.

Kichapo hicho kimemfanya Gamondi kuendeleza uteja kwa TRA United (Tabora United), kwani mara ya mwisho akiifundisha Yanga, kocha huyo alichapwa katika mechi ya Novemba 7, 2024, ikiwa ni mwendelezo wa kile alichokifanya msimu uliopita.

Gamondi alijiunga na Yanga Juni 24, 2023 akichukua nafasi ya Mtunisia, Nasreddine Nabi aliyeipa mataji mawili ya Ligi Kuu, mawili ya Kombe la Shirikisho (ASFC), mawili ya Ngao ya Jamii na kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

GAMO 02

Kwa upande wa Gamondi amechukua mataji matatu na Yanga akianza na Ligi Kuu Bara msimu wa 2023-2024 na kuifanya timu hiyo kufikisha jumla ya mataji 30, tangu mwaka 1965, akachukua pia Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ngao ya Jamii mwaka 2024.

Pia Gamondi ameipa Singida Kombe la Kagame mwaka 2025, baada ya kuichapa Al Hilal Omdurman ya Sudan mabao 2-1, Septemba 15, 2025, huku akiiwezesha timu hiyo kufuzu katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza.