Serikali yapinga shauri kufutwa sherehe za Uhuru

Dar es Salaam.  Wakati Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma, ikitarajia kusikiliza shauri la maombi ya kibali cha kupinga uamuzi wa kufuta sherehe za maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika mwaka 2025, Serikali imewasilisha pingamizi la awali ikiomba shauri hilo lifutwe bila kupewa nafasi ya kusikilizwa.

Shauri hilo lilifunguliwa na Wakili Peter Madeleka dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kutokana na uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kufuta sherehe za maadhimisho ya Uhuru, Desemba 9, 2025.

Uamuzi huo ulitangazwa na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, Novemba 24, 2025, akisema Rais Samia ameelekeza fedha ambazo zingetumika kwenye sherehe hizo zitumike kukarabati miundombinu iliyoharibiwa wakati wa ghasia za maandamano ya wakati wa Uchaguzi Mkuu, Oktoba 29, 2025.

Madeleka katika hati ya maombi ya shauri hilo alilolifungua Novemba 26, 2025, anaomba ruhusa ya mahakama kufungua shauri la kupinga uamuzi huo kwa utaratibu wa mapitio ya mahakama kumwezesha kuomba amri tatu.

Amri hizo ni, mahakama kufuta uamuzi wa Rais wa kufuta sherehe hizo, akidai si halali na usio na maana. Nyingine ni ya kumlazimisha kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria, pia ya zuio la kufuta sherehe hizo.

Shauri hilo limepangwa kusikilizwa na Jaji Juliana Masabo Jumatatu, Desemba 8, 2025.

Hata hivyo, wajibu maombi wamewasilisha kiapo kinzani kujibu maombi hayo, sambamba na taarifa ya pingamizi la awali dhidi ya shauri hilo.

Katika taarifa ya pingamizi la awali iliyoandaliwa na kuwasilishwa mahakamani Ijumaa, Desemba 5, 2025, iliyosainiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Stanley Kalokola, wajibu maombi wamebainisha sababu mbili za pingamizi dhidi ya shauri hilo.

Katika sababu ya kwanza wanadai shauri hilo ni batili kisheria kwa kuwa linakiuka kifungu cha 19 cha Sheria ya Maboresho ya Sheria (Kuhusu Ajali Mbaya na Masharti Mbalimbali) na kifungu cha 8(1) cha Sheria ya Masuala ya Rais; Marejeo ya mwaka 2023.

“Maombi haya ni batili kwa kuwa hayakuambatanishwa na uamuzi ambao unaombewa ruhusa ya kuwasilisha shauri la mapitio ya kimahakama, kupata amri za kufuta uamuzi huo, amri ya kumlazimisha na amri ya zuio (dhidi ya Rais)” inaeleza hati hiyo kuhusu sababu ya pili.

Kutokana na sababu hizo za pingamizi, wajibu maombi wanaiomba mahakama ilitupilie mbali shauri hilo bila hata kusikiliza hoja za msingi.

Katika kiapo na hati ya maelezo yake zinazounga mkono maombi hayo, Madeleka anadai uamuzi wa Rais kufuta sherehe hizo alioutoa kupitia kwa Waziri Mkuu Novemba 24, 2025, uliripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari likiwemo gazeti la Mwananchi la Novemba 25, 2025.

“Sherehe hizo zilizoelezwa hapo juu huadhimishwa kihalali kila Desemba 9 na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kuenzi Uhuru wa Tanganyika wa Desemba 9, 1961 chini ya uratibu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” ameeleza.

Madeleka anasema yeye ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mkazi wa Dar es Salaam, ambaye ana haki ya kusherehekea sherehe hizo, chini ya uratibu wa Serikali kwa mujibu wa sheria.

Anadai endapo sherehe za maadhimisho ya siku hiyo kwa mwaka 2025 hazitafanyika, haki zake zitaguswa kwa kadiri sherehe hizo zinavyomhusu, kwani yeye ni mnufaika halali wa sherehe hizo.

Kwa msingi huo, anasema ndiyo maana anaomba ruhusa ya kufungua shauri la mapitio ya mahakama kupinga uamuzi wa Rais kufuta sherehe hizo, ili aombe mahakama itoe amri hizo tatu dhidi ya uamuzi huo.

Madeleka anadai anakusudia kuomba amri hizo kutengua uamuzi wa Rais ili kuheshimu sheria zilizowekwa za kuadhimisha siku ya Uhuru wa Tanganyika wa Desemba 9, 1961.

Anaeleza Sheria ya Siku za Mapumziko ya Umma (Sura ya 35 Toleo la 2023) inaelekeza Uhuru wa Tanganyika uliopatikana Desemba 9, 1961 utaadhimishwa kila Desemba 9 ya mwaka.

“Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaweka wajibu kwa kila raia wa Tanzania kuzingatia Katiba na sheria nyingine za nchi,” ameeleza.

Hivyo, ataomba amri ya mahakama kumlazimisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kutekeleza sheria zilizoanzishwa za kuadhimisha siku ya Uhuru wa Tanganyika Desemba 9.

Pia ataomba amri ya kumzuia Rais, kuendelea kutekeleza tangazo lake la kusitisha sherehe hizo mwaka huu, kwani kufanya hivyo hakujafuata utaratibu, ni kinyume cha Katiba na sheria nyingine za nchi.

“Mjibu maombi wa kwanza (Rais) hawezi kuruhusiwa kutumia mamlaka ambayo hana kisheria au ambayo yanakiuka sheria za nchi,” ameeleza.

Awali, shauri hilo lilipangwa kusikilizwa upande mmoja Novemba 28, 2025. Hata hivyo, siku hiyo upande wa wajibu maombi kupitia Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali baada ya kupata taarifa hizo kupitia vyombo vya habari, alifika mahakamani akaeleza hawajapata nakala za shauri hilo.

Hivyo, alipinga shauri hilo kusikilizwa siku hiyo upande mmoja kwa madai kuwa, wao wajibu maombi walikuwa hawajapewa nakala za nyaraka za shauri hilo.

Vilevile akadai Rais alipaswa apewe kwanza taarifa kwa mujibu wa kifungu cha 9(3) cha Sheria ya Masuala ya Rais.

Alidai Rais hajapewa taarifa hiyo, hivyo waliomba shauri liahirishwe mpaka watakapopewa nyaraka na Rais atakapopewa taarifa.

Madeleka alidai chini ya Kanuni ya 5(1) na (2) na 5 za Kanuni za Marekebisho ya Sheria (Kuhusu Ajali Mbaya na Masharti Mbalimbali) (Utaratibu wa Mapitio ya Kimahakama na Ada), za mwaka 2014 shauri hilo linapaswa kusikilizwa upande mmoja.

Alidai kuwapatia au kutokuwapatia nyaraka hizo hakuwezi kuzuia usikilizwaji wake kwa kuwa hata kama wangekuwa nazo, katika hatua hiyo hawangeweza kusema lolote.

Jaji Masabo katika uamuzi alikubali hoja za Madeleka akasema kifungu cha 9 (3) cha Sheria ya Masula ya Rais hakihusiki katika mashauri ya mapitio ya kimahakama.

Jaji Masabo alisema kwa mujibu wa Kanuni za Marekebisho ya Sheria (Kuhusu Ajali Mbaya na Masharti Mbalimbali) (Utaratibu wa Mapitio ya Kimahakama na Ada), shauri la kibali cha kufungua shauri la mapitio dhidi ya Rias linaweza kusikilizwa bila kumuarifu.

“Hivyo, pingamizi hili linatupiliwa mbali. Shauri hili litaendelea kusikilizwa,” alisema Jaji Masabo na kuwataka wajibu maombi wawasilishe mahakamani kiapo kinzani kabla au Desemba 5 na shauri litasikilizwa Desemba 8, 2025.

Kufuatia uamuzi huo, wajibu maoni kwenye kiapo chao yameambatanisha na pingamizi wakitaka litupiliwe mbali bila kusikilizwa.