Dar es Salaam. Serikali imeweka mkakati wa muda wa kupunguza foleni za magari jijini Dar es Salaam kwa kuagiza kufunguliwa kwa barabara za makutano katika maeneo yanayotekelezwa miradi ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT).
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Aisha Amour, ametoa agizo hilo jana Jumamosi, Desemba 6, 2025 alipotembelea na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Amesema msongamano wa magari unatarajiwa kuongezeka kuelekea kipindi cha sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya, hivyo ili kukabiliana na hali hiyo, ametoa maagizo ya kufunguliwa kwa makutano ya barabara na kuruhusu matumizi ya njia za michepuko.
“Tumeona njia ya haraka ya kupunguza msongamano katika kipindi hiki ni kufungua barabara za makutano wakati tukisubiri ujenzi wa kudumu wa barabara hizo unaoendelea, ikiwemo ule wa BRT,” amesema.
Aidha, ameelekeza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuhakikisha barabara zote za michepuko zinapitika na ziko katika hali nzuri, ili kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi na wafanyabiashara.
Ili kuhakikisha ufanisi na utekelezaji wa maagizo hayo, Katibu Mkuu amemuagiza mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa barabara ya Mwenge–Tegeta kuweka lami ya muda katika barabara ya michepuko ili kuboresha upitishaji wa magari wakati ujenzi ukiendelea.
Amesisitiza kuwa Serikali inatambua usumbufu unaosababishwa na utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu, hususan BRT, ameitaka Tanroads kutoa taarifa za mara kwa mara ili kuwasaidia watumiaji wa barabara kufahamu njia mbadala wanazoweza kutumia katika shughuli zao za kila siku.
“Taarifa hizi zitasaidia kupunguza malalamiko na kuwapa wananchi fursa ya kupanga safari zao mapema kwa kutumia njia mbadala,” amesema.
Pia, amewasihi wananchi kuendelea kufuata sheria za usalama barabarani, ikiwemo kuzingatia vibao vya muda vitakavyowekwa katika maeneo ya ujenzi, ili kuepusha ajali na kuhakikisha mtiririko mzuri wa magari.
Kwa upande wake, meneja wa Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Alinanuswe Kyamba, akipokea maelekezo hayo amesema wameanza kuchukua hatua kwa vitendo ili kutekeleza maagizo hayo.
“Tayari tumeanza kuwaelekeza baadhi ya wakandarasi kuanza kufungua barabara za makutano na kuboresha barabara za michepuko kupunguza msongamano wa magari,” amesema.
Amesema Tanroads itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mkakati huo na kuhakikisha unaleta unafuu wa haraka kwa watumiaji wa barabara wakati ujenzi wa mradi wa barabara hizo ukiendelea.
Hatua hiyo ya Katibu Mkuu imekuja takribani wiki moja baada ya Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, kutoa maagizo kwa Tanroads kuhakikisha foleni za magari zinakomeshwa.
Akiwa ziarani jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, kukagua maendeleo ya upanuzi wa barabara ya Mbagala Rangi Tatu – Kongowe (kilomita 3.8), aliwaeleza wananchi wa eneo hilo kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameidhinisha zaidi ya Sh54 bilioni kwa ajili ya kutatua kero ya foleni kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani.
Katika ziara hiyo, Ulega aliwaagiza viongozi wa Tanroads nchi nzima kuhakikisha wanashughulikia changamoto za msongamano wa magari katika maeneo yao kwa ufanisi na kwa wakati.
“Ninawaagiza mameneja wote wa Tanroads nchi nzima kumaliza tatizo la foleni. Nikisikia habari za foleni zinalalamikiwa na wananchi na hakuna suluhu ya muda mfupi na ya muda mrefu, hufai kuwa meneja,” alisema Ulega.
Aidha, Ulega alitoa angalizo kwa mameneja hao katika kipindi hiki cha mvua zinazotarajiwa kuendelea kunyesha kuhakikisha barabara hazileti athari kwa wananchi na kusababisha kushindwa kufanya shughuli zao kutokana na kukosa suluhu ya jambo hilo mapema.
“Mameneja, fanyeni kazi, msikae kimazoea na kuona jambo hilo ni la kawaida, kukatika kwa barabara tafsiri yake meneja hukagua barabara yako na kuona hapa kuna udhaifu ambao lolote likitokea, pataharibika,” alisisitiza.
Vilevile, Waziri Ulega alimuagiza Meneja wa Tanroads Mkoa wa Pwani kuitengeneza barabara ya zamani ya Morogoro haraka iwezekanavyo ili iwe njia mbadala ya kutatua changamoto za magari kukwama katika barabara kuu ya Dar es Salaam hadi Chalinze na kusababisha foleni za magari katika barabara hiyo kuu ya kutoka jijini Dar es Salaam kuelekea mikoani.
