KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Mohamed Bajaber amesimulia namna alivyokuwa anapitia wakati mgumu kipindi alipokuwa anasumbuliwa na majeraha na ilibaki kidogo aondolewe kikosini bila kuonja mechi ya mashindano.
Japokuwa Bajaber alikiri wachezaji wenzake walikuwa wanampa moyo, lakini hilo halikumuondolea kujisikia vibaya na kutamani itokee siku moja acheze mechi ya Ligi Kuu Bara kama alivyopata nafasi dhidi ya Mbeya City, na kufunga bao katika ushindi wa mabao 3-0 ilioupata Simba.
“Ni kipindi kigumu kwa mchezaji kukaa nje bila kucheza, inahitaji moyo wa uvumilivu na kutokukaa tamaa, nilikuwa naumia moyo sana kuona wenzangu wanacheza halafu mimi nauguza majeraha kwa muda mrefu, sina maana kwamba sipendi wacheze wengine ila nilitamani kuona natoa mchango wangu,” amesema Bajaber na kuongeza;
“Baada ya kurejea katika ufiti kabla ya kuondoka kwa kocha Dimitar Pantev alitaka kuniondoa jambo ambalo lilikuwa linaniumiza kwani Simba ni klabu kubwa inayojenga CV ya mchezaji, hivyo kingekuwa kitu kibaya kwangu.”
Amesema kitendo cha kupata nafasi dhidi ya Mbeya City na kufunga bao kimeibua matumaini mapya na kuleta furaha ya moyo, kuona angalau kafanya kitu: “Angalau jina langu litatajwa kwa kucheza mechi, ilikuwa inaniumiza kuona lingeishia kutajwa katika usajili lakini nisicheze.”
Miongoni mwa timu zilizokuwa zinatajwa huenda angetolewa kwa mkopo ni Polisi ya Kenya na TRA baada ya kumpata kocha mpya Etienne Ndayaragije aliyewahi kumfundisha Kenya.
Kutokana na hilo Bajaber amesema: “Etienne ni kocha aliyenifundisha Polisi ya Kenya na tulichukua ubingwa kama nilivyosema baada ya kurejea kutoka katika majeraha kocha Pantev alitaka nitolewe kwa mkopo.”
