SMZ yaahidi kuimarisha sekta ya michezo Zanzibar

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema  itaendelea kutoa ushirikiano katika kuhakikisha sekta ya michezo inaimarika zaidi na kutoa faida chanya kwa wanamichezo.

Hayo yamesemwa leo Jumapili Desemba 7, 2025 na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla katika bonanza la mchezo wa mazoezi ya viungo, lililofanyika Kinduni, Kaskazini Unguja. 

Hemed amesema, hayo yote yanayofanywa na Serikali ni kuhakikisha wananchi wake wanakuwa na afya bora na kujiepusha na maradhi yasiyo ya kuambukiza ikiwemo kisukari.

Pia, amesema mazoezi huimarisha zaidi afya ya mwili na akili, hujenga umoja, upendo na mshikamano katika jamii.  

Amewataka, wanamichezo na wananchi kujitokeza kuchangia damu ili kuokoa maisha ya watu wenye uhitaji kama vile wanaofanyiwa upasuaji, waathirika wa ajali, akina mama wanaopoteza damu wakati wa kujifungua na wagonjwa wenye magonjwa yanayohitaji damu mara kwa mara.

Katika bonanza hilo, Hemed amewasisitiza wananchi kuendelea kudumisha amani na utulivu iliyopo nchini na kujiepusha na kujiingiza katika vitendo vinavyoweza kupoteza amani hiyo.

ZN 01

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Riziki Pembe Juma amekishukuru chama cha mchezo wa viungo Zanzibar (Zabesa) kwa kuendelea kushirikiana na wizara ya hiyo kuelimisha wananchi umuhimu wa kufanya mazoezi.

Pembe, amewataka Wazanzibari kujenga utamaduni wa kuhamasishana kufanya mazoezi kwa rika zote ili kulinda afya zao na magonjwa nyemelezi ambayo yamekuwa yakiwakumba wananchi wengi kutokana na kutokufanya mazoezi. 

Akisoma risala kwa niaba ya wanamichezo wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mwenyekiti wa chama hicho, Amour Hamad Amour amesema wanamichezo wanaunga mkono juhudi za Serikali katika kuleta maendeleo kwa wananchi.

Amour, ametoa wito kwa wanamichezo na wananchi wa Kaskazini Unguja mara baada ya kumalizika kwa Bonanza hilo kujitokeza kupima afya zao na kuchangia damu ili kusaidia wananchi wenye uhitaji.