TAFCA Mwanza yamkingia kifua Matola

CHAMA cha Makocha Tanzania (TAFCA) Mkoa wa Mwanza kimeungana na baadhi ya mashabiki na wadau wa soka nchini wanaompigia chapuo kocha mzawa Selemani Matola kuaminiwa na Simba na kupewa jukumu la kukinoa kikosi hicho moja kwa moja.

Matola amedumu Simba kama kocha msaidizi kwa takriban miaka 10 akiwa chini ya makocha wengi wa kigeni katika nyakati tofauti.

Kocha wa mwisho kusaidiana na Matola ni Dimitar Pantev aliyekuwa akiitwa meneja, aliyefukuzwa Desemba 2 kutokana na matokeo yasiyoridhisha kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo Matola aliiongoza timu katika mechi ya Ligi Kuu akiisaidia kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mbeya City.

TAF 01

Katika mechi hiyo kiwango cha timu kiliwakuna mashabiki na kuutaka uongozi wa Wekundu wa Msimbazi kumpa kazi Matola.

Akizungumza na Mwanaspoti jijini Mwanza, Kocha na Mwenyekiti wa TAFCA Mwanza, Kessy Mziray, aliunga mkono maoni ya mashabiki hao akiamini elimu aliyonayo inatosha kupewa kazi hiyo.

Amesema mbali na elimu, lakini uzoefu aliojizolea Matola akiwa chini ya makocha zaidi ya 10 wa kigeni ndani ya Simba, ana sifa na uwezo wa kuongoza benchi la ufundi kwa mafanikio makubwa.

TAF 02

“Sababu kubwa anakidhi vigezo vyote vinavyohitajika ikiwemo elimu na uzoefu, kwasababu amekuwa kwenye Ligi Kuu kwa muda mrefu. Ana utaalamu wa kutosha kutoka kwa makocha wakubwa waliopita Simba,”  amesema Mziray.

“Lazima ana hamu ya mafaniko akiwa kocha mkuu, hivyo uongozi ukimwamini na kumpatia mahitaji yake muhimu atatimiza malengo.”