Mwanza. Ulishawahi kujiuliza, ukifikisha umri wa miaka 60 au zaidi, nini hasa utakitegemea ili kuishi maisha yenye furaha, afya na utulivu wa moyo? Wengi hudhani familia, watoto au marafiki wa karibu ndio msaada wa uhakika uzeeni.
Lakini kwa kiuhalisia, kadri miaka inavyosonga mbele, hali za maisha hubadilika. Uhusiano unapoa, watoto hujishughulisha na maisha yao, na hata marafiki waliokuwa karibu, hupotea au kuwa na vipaumbele tofauti.
Ndiyo, familia ni muhimu lakini haitoshi. Maisha ya uzeeni yenye heshima na furaha yanahitaji maandalizi ya muda mrefu na msimamo binafsi. Kutegemea familia pekee ni kujidanganya. Unaweza kuishi uzeeni ukiwa na heshima kwa kujenga nguzo zako binafsi mapema.
Hivyo, kabla hujafikia umri huo, ni muhimu kujipanga kwa kuzingatia mambo kadhaa ambayo yanaweza kuwa tegemeo lako la kweli ukiufikia uzee kuliko hata familia, ndugu na marafiki unaodhani.
Fedha inaweza isinunue furaha, lakini inaweza kununua usalama wako, uhuru wako na kutuliza nafsi na akili yako.
Ukifika miaka 60 na kuendelea bila akiba au chanzo cha mapato cha kuaminika, hata familia inaweza kushindwa kukusaidia inavyotakiwa. Akiba, pensheni, au uwekezaji ni nguzo muhimu ya maisha ya baadaye.
Ripoti ya Benki ya Dunia (WB) inaonyesha kuwa wazee wengi Afrika Mashariki hukosa usaidizi wa kifedha kwa sababu ya kutokuwa na maandalizi ya kustaafu.
Aidha, ripoti ya mwaka 2023 ya FinScope Tanzania inaonyesha kuwa asilimia 28 ya watu wazima nchini Tanzania hawana mipango ya kustaafu, na asilimia nane wanategemea watoto wao kwa usaidizi wa kifedha, huku asilimia mbili wakitegemea msaada kutoka kwa marafiki au jamaa.
Lakini, pia utafiti uliofanywa na shirika la HelpAge Tanzania, umeonyesha kuwa wazee wengi wanaofaidika na mifuko ya pensheni kama vile Zanzibar Universal Pension Scheme (ZUP) wameweza kuboresha hali zao za kifedha na kupunguza utegemezi kwa familia.
Kwa mfano, ZUP iliongeza pensheni kutoka Sh20,000 hadi Sh50,000 ambapo wazee 28,513 kati yao wanawake wakiwa 16,614 walifaidika.
Bila afya bora ya akili na mwili, kila kitu hupoteza maana. Afya ndiyo msingi wa maisha kwakuwa unapokuwa na afya njema unaweza kujitegemea, kufurahia maisha, na kuepuka utegemezi kwa wengine.
Watu wengi wanapuuzia suala zima la afya wakiamini uzeeni kuna watu hasa watoto wao watakaowasaidia ikiwemo kuwauguza, lakini ukweli mchungu hata kama familia yako itakupenda, kumbuka na wao wana maisha na watu wengine wanawategemea, hivyo wanaweza wasiwe na muda wala nafasi ya kukuuguza.
Bila afya bora, huwezi kufurahia maisha, hata kama una fedha au familia inayokuunga mkono. Na ili uwe na afya bora ni lazima kuzingatia ulaji mzuri, kufanya mazoezi ya mwili, kufanya vipimo vya afya hospitalini mara kwa mara, kulala usingizi wa kutosha na kuepuka mawazo na huzuni.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linashauri wazee waendelee kufanya mazoezi ya angalau dakika 150 kwa wiki ili kudumisha afya ya mwili na akili.
Kujichanganya na jamii/ kutengeneza marafiki wapya
Miongoni mwa makosa yanayofanywa na baadhi ya watu wakielekea uzeeni, ni kujitenga katika maisha ya kila siku.
Kujiweka mbali na vikundi vya kijamii, vikundi vya ibada, au vikundi vya burudani ni mwanzo wa kuukaribisha upweke.
Upweke huo hautoumiza tu hisia zako lakini pia utahatarisha afya kwa ujumla pamoja na uwezo wa kufikiri na hata kufupisha maisha.
Hivyo kabla ya kufikia hali hiyo ni muhimu kutengeneza marafiki wapya, kujichanganya katika shughuli za kijamii ili kupata watu watakaokujulia hali, kukufurahisha na kukuletea nguvu ya kutamani uendelee kuishi kuliko kutegemea familia yako pekee.
Utafiti wa Chuo Kikuu cha Harvard kuhusu furaha na ustawi wa binadamu (Harvard Study of Adult Development) uliofanywa kwa washiriki kwa zaidi ya miaka 80, uligundua uhusiano mzuri wa kijamii ni kipengele muhimu zaidi kinachochangia furaha na ustawi wa binadamu.
Mduara wa kijamii unakuwa msaada mkubwa hasa unapokutana na changamoto za afya au hali ngumu. Wakati mwingine, marafiki na majirani ndio wanaoweza kukupeleka hospitalini au kukusaidia kujua jinsi ya kutunza afya yako.
Watu wengi hukata tamaa baada ya kustaafu kwa sababu hawana shughuli au malengo mapya, hivyo watalaamu wa masuala ya maisha na uhusiano wanashauri hata mara baada ya kustaafu au kuzeeka, kuna umuhimu wa kuwa na sababu ya kukufanya uamke asubuhi ikiwemo kuendeleza kile ulichokuwa ukikifanya enzi za ujana wako.
Wazee wanasahuriwa kuacha kujitenga badala yake kama wana ujuzi wafundishe vijana mfano useremala, ushonaji, kilimo au wanaweza kujitolea kwenye kanisa, msikiti, au wakati mwingine wanaweza kusaidia wajukuu au watoto wa jirani kusoma, kulima bustani au kuchangamana na watoto au vijana kuwasimulia hadithi na hata kuziandika.
Wazee wenyeb malengo katika maisha yao kama vile kujitolea au kushiriki katika shughuli za jamii wana furaha zaidi na wanajiona kuwa na manufaa kwa jamii.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Dk Patrick Hill wa Chuo Kikuu cha Carleton nchini Canada pamoja na Dk Nicholas Turiano wa Kituo cha Matibabu cha Chuo Kikuu cha Rochester (USA) mwaka 2014, kuwa na lengo la maisha kunaweza kuongeza muda wa kuishi.
Kwa kutumia data kutoka utafiti wa Midlife in the United States (MIDUS), waligundua kuwa watu wenye lengo thabiti la maisha, walikuwa na asilimia 15 hadi 30 chini ya hatari ya kufariki kuliko wale wasiokuwa na lengo la wazi.
Katika maisha hakuna kitu kinachobaki vile vile kilivyokuwa, kwani hata watu hubadilika.Uliowategemea hawawezi kuwa kama ulivyodhani.
Kitu pekee kitakachokufanya uendelee kuishi kwa furaha ni uwezo wa kukubali na kukabiliana na mabadiliko hasa kwa kuvumbua vitu vipya, kujaribu mabadiliko ya teknolojia na kukubali kujifunza vitu ambavyo huvifahamu hata kama ni kutoka kwa vijana wadogo, kwakuwa kujifunza hakumaliziki hasa kwa karne hii ya mabadiliko ya haraka.
Tafiti za Shirika la Umoja wa Mataifa, Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) zimeonyesha kuwa programu za kutoa ujuzi mpya na kuboresha ujuzi wa wazee, zinasaidia kuongeza uhuru wao, kukuza afya bora, na kuboresha ubora wa maisha yao.
Haijalishi una umri gani, lakini ni ukweli usiopingika maisha yana njia nyingi za majaribu. Hata uzeeni changamoto hazikosekani, zinakuwepo na wakati mwingine zinaongezeka ikiwemo wale uliowategemea kuwa msaada kwako kufariki dunia, marafiki kukutenga au urafiki kuvunjika au kupata matatizo ya afya na wakati mwingine maisha kuwa ya upweke kuliko ulivyodhani.
Haya yote unaweza kuyaepuka uzee ukibisha wodi iwapo utajijenga kuwa na uwezo wa kukubaliana na mabadiliko, kuhimili hisia zako na kutafuta amani wakati wa kipindi kigumu, kwakuwa ndivyo vitu vitakavyokufanya usonge mbele hata kama mambo hayaendi vile ulivyopanga ujanani mwako.
Mzee mwenye ustahimilivu wa kihisia huweza kukabiliana na matatizo kwa hekima, kulinda afya ya akili, kuendelea kuwa na matumaini na kuishi maisha yenye utulivu, heshima na furaha.