Hai. Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kuweka mikakati madhubuti na kutilia mkazo suala la ukusanyaji wa mapato, ili kuiwezesha halmashauri kuwaletea wananchi maendeleo yanayoonekana.
Wito huo umetolewa leo, Desemba 7, 2025, na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa, katika mkutano wa kwanza wa baraza la madiwani uliofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo.
Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi wa Serikali, wa dini, taasisi mbalimbali na wananchi.
Akizungumza katika kikao hicho, Nzowa amewataka madiwani kuwekeza nguvu na ubunifu wa kutosha kuboresha ukusanyaji wa mapato.
“Ninyi madiwani mtusaidie kuboresha uthibiti wa mapato ili yalete maendeleo kwa wananchi. Bila mapato hakuna miradi, hakuna kinachoendelea,” amesema Nzowa.
Amesema mapato ndiyo uti wa mgongo wa halmashauri katika utekelezaji wa majukumu yake, hivyo ajenda ya mapato inapaswa kuwa ya kudumu kwenye vikao vya baraza hilo.
Nzowa amekumbusha kuwa katika hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati akiwaapisha mawaziri, alisisitiza kuwa miradi mingi ya maendeleo sasa inategemea mapato ya ndani. Kwa msingi huo, halmashauri zina wajibu wa kuongeza ufanisi katika ukusanyaji na udhibiti wa matumizi ya mapato hayo.
“Haina maana kukusanya kwa wingi kama matumizi si kwa masilahi ya wananchi. Boresheni pia udhibiti wa matumizi,” amesema.
Nzowa amewataka madiwani kuimarisha nidhamu kwa watumishi, akisisitiza kuwa pamoja na wengi wao kufanya kazi vizuri, bado wapo watumishi legelege wanaoshindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo.
“Msisite kuwashauri au kuchukua hatua dhidi ya watumishi wanaolegalega. Wanapaswa kufanya kazi ya kutumikia wananchi,” amesema.
Aidha, amewataka viongozi na wananchi kuendelea kulinda amani ya nchi, akisisitiza kuwa bila amani hakuna maendeleo.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Hai, Saashisha Mafuwe, amesema Serikali ina vipaumbele vya maendeleo katika kipindi cha miaka mitano, vikiwemo uboreshaji wa kilimo cha umwagiliaji kupitia skimu saba zinazofanyiwa kazi, ili kuongeza uzalishaji na kuboresha uchumi wa wananchi.
“Kila diwani aende kwenye eneo lake kutafuta fursa ambazo zitawawezesha wananchi kuondokana na umaskini,” amesema Mafuwe.
Pia, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hai, Edmund Rutaraka, na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Dionis Myinga, nao kwenye hotuba zao wamewataka madiwani na watumishi kufanya kazi kwa umoja na upendo ili kufikia adhima ya Serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Hai, Hassan Bomboko, amesema baraza hilo ndilo chombo kitakachosimamia halmashauri kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
“Naombeni sana, dhamana mliyopewa iheshimiwe. Jambo la kwanza ni kupendana na kuwa kitu kimoja. Ushirikiano ndiyo msingi wa mafanikio,” amesema Bomboko.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Hai, Wanguba Maganda, amewataka madiwani hao kuzingatia kiapo walichokula cha kuwatumikia wananchi, kwa kuwasikiliza na kutatua changamoto wanazokutana nazo.
“Kiapo ni kitu kizito. Ukishaapa, kumbuka uzito wake,” amesema Maganda.
