KIUNGO wa Mogbwemo Queens, Mtanzania Zuwena Aziz ‘Zizou’ amesema amebaini vitu tofauti tangu alipojiunga na chama hilo linaloshiriki Ligi Kuu ya Wanawake Sierra Leone.
Kiungo huyo alijiunga na timu hiyo akitokea Tausi (zamani ikiitwa Ukerewe Queens) ambako alidumu msimu mmoja akiipandisha katika Ligi Kuu ya Wanawake Bara.
Akizungumza na Mwanaspoti, Zizou amesema amepokelewa vizuri na timu hiyo lakini pia imeweka utaratibu mzuri wa malazi kwa wachezaji kwani kila mmoja ana chumba chake. “Tunaishi kambini na nilipofika tu nilipokelewa vizuri ilka cha tofauti ni kwamba huku hakuna kuchangia chumba kila mmoja ana chake sijui kwa sababu kikosi kizima kina wachezaji 18 lakini ni utaratibu mzuri sana,” amesema.
“Kati ya hao 18 Mtanzania peke yangu watano timu ya taifa, Sierra Leone na wengine kutoka Ghana, Niger, Gine, Liberia na nchi nyingine za Afrika Magharibi.”
Aliongeza kuwa tayari amefanya mazoezi ya timu siku moja lakini kila mchezaji anaonyesha ushindani hivyo kwake anatamani kupambana na kupata nafasi kwenye kikosi hicho. “Natamani nicheze na kuisaidia timu kunyakua ubingwa wa ligi msimu huu kisha twende Ligi ya Mabingwa Afrika na mimi niandike rekodi nyingine.”
