Dar es Salaam. Shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na masuala ya kisheria, Everlasting Legal Aid Foundation (ELAF), limewataka viongozi wa dini, Serikali na jamii kuendeleza uzalendo na kulinda tunu za Taifa, hususan katika kipindi hiki cha maadhimisho ya miaka 64 ya Uhuru wa Tanzania.
Akizungumza leo Desemba 8, 2025, ofisini kwake jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari, Mkurugenzi wa ELAF, Dk Khamis Masoud, amesema kuwa licha ya Serikali kutangaza kufuta sherehe za Uhuru mwaka huu, taasisi hiyo inaona ni muhimu kuikumbusha jamii juu ya wajibu wa kutafakari thamani ya Uhuru pamoja na misingi ya kitaifa.
“Serikali imefuta sherehe, lakini haijafuta wajibu wa Taifa kuzungumza kuhusu Uhuru, kujadili msingi wake, na kukumbushana wajibu wa kuuenzi,” amesema Dk Masoud.
Ameongeza kuwa Uhuru hauwezi kutenganishwa na misingi ya haki, umoja, amani na uadilifu, ambazo ndizo nguzo kuu zinazolifanya Taifa kuwa thabiti.
Dk Masoud amewataka Watanzania kutumia muda huu wa maadhimisho kufanya tafakari ya kina kuhusu nchi ilipotoka, ilipo na inapokwenda kama Taifa.
Pia, ELAF imewaasa viongozi wa dini kusimamia mafundisho sahihi ya dini zao na kujiepusha na matamko yanayoweza kuchochea chuki, misimamo mikali au kuibua hisia za udini katika jamii.
“Viongozi wa dini wana nafasi kubwa sana katika kuunda fikra za jamii. Mafundisho yao yanapaswa kutuunganisha, si kutugawa,” anasema Masoud.
Anasema kuwa katika kipindi hiki ambacho Taifa limepitia machafuko ya kisiasa na mijadala mikali kufuatia matukio ya Oktoba 29, kauli za viongozi wa dini zinatakiwa kuwa za hekima, kujenga matumaini na kuhamasisha amani.
Aidha, Dk Masoud ameiomba Serikali kujiepusha na matamko ya harakaharaka, au kauli ambazo zinaweza kutafsiriwa baadaye kuwa ni za mihemko na hivyo kuongeza chuki miongoni mwa wananchi.
“Viongozi wa Serikali wanapaswa kutafakari kabla ya kuzungumza. Kauli zinazotolewa kwa hasira au zilizojaa hisia zinaweza kulitumbukiza Taifa kwenye mgawanyiko mkubwa,” anasema.
Amesisitiza kuwa katika kipindi ambacho Taifa limepita kwenye majeraha ya kisiasa, viongozi wanapaswa kuwa mfano wa utulivu na umoja kwa wananchi.
Pia, ELAF imetamka hadharani kuwa inatarajia kuona viongozi na watendaji waliohusishwa na matukio ya Oktoba 29 wakichukua hatua za kiuongozi, ikiwemo kukaa pembeni ili kupisha uchunguzi wa kina kufanyika bila ushawishi
“Tunaona aibu kubwa kama Taifa. Ikiwa wananchi wanaodaiwa kuharibu miundombinu waliweza kukamatwa na kufikishwa mahakamani haraka, ni kwa nini wale waliopewa dhamana ya kulinda raia na mali zao hawapaswi kuachia nafasi zao kupisha uchunguzi?” amehoji Masoud
