IPU yaridhishwa maandalizi ya mkutano mkuu Tanzania, Dk Tulia…

Dar es Salaam. Wajumbe wawakilishi kutoka Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) wameridhishwa na maandalizi ya Tanzania kuelekea mkutano mkuu wa umoja huo.

Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano mkuu wa IPU utakaofanyika Oktoba 2026 ukijumuisha wajumbe kutoka mataifa mbalimbali wanachama wa umoja huo.

Hayo yamebainishwa leo Jumatatu, Desemba 8, 2025, katika kikao kazi cha mabalozi wawakilishi wa IPU kilichofanyika katika ofisi ndogo za Bunge la Tanzania, jijini Dar es Salaam.

Katika kikao hicho, Mwenyeji wa wajumbe hao, Spika wa Bunge la Tanzania, Azzan Zungu, amewaeleza hali ya nchi akiwahakikishia Tanzania ipo tayari kuwa mwenyeji wa mkutano huo na maandalizi yanaendelea vizuri.

Spika pia amewahakikishia hali ya ulinzi na usalama iko shwari na mkutano utafanyika katika mazingira ya amani na utulivu.

Kwa upande wake, Mkuu wa wawakilishi hao kutoka IPU, Balozi Anda Filip, ameeleza kuridhishwa na mazingira na miundombinu aliyoitembelea nchini katika maandalizi ya mkutano huo.

Balozi Filip ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma kwa Wabunge wa IPU makao makuu ameambatana pia na Tara Staub, ambaye ni mratibu wa mikutano ya kibunge katika umoja huo.

Akizungumzia hali ya ukumbi na huduma muhimu, Balozi huyo ampongeza maandalizi yanayofanywa kuelekea mkutano huo.

“Tumetembelea ukumbi wa mikutano wa Arusha, tumeona mazingira na maandalizi mazuri kuendesha mkutano huo,” amesema.

Aidha, katika mkutano huo moja ya ajenda kuu zitakazojadiliwa na kufanyiwa kazi ni uchaguzi wa rais mpya wa IPU.

Kwa sasa, aliyekuwa spika wa bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson ndiye anashikilia nafasi hiyo tangu alipochaguliwa mwaka 2023.

Kwa kanuni za IPU, rais wake anashikilia wadhifa huo kuanzia wakati anapochaguliwa mpaka pale uchaguzi mwingine utakapofanyika kwa mujibu wa kalenda ya mabunge hayo.

Kwa maantiki hiyo, licha ya Dk Tulia kutokuwa kwenye nafasi ya uspika   anaendelea kuwa rais wa IPU mpaka hapo uchaguzi utakapofanyika.

Hivyo, mkutano mkuu wa Oktoba mwakani utakaofanyika hapa nchini, utahitimisha rasmi uongozi wa Dk Tulia baada ya kuchaguliwa rais mpya.

ni taasisi ya kimataifa inayozikutanisha mabunge ya nchi mbalimbali kwa lengo la kukuza demokrasia, amani, haki za binadamu na diplomasia ya kibunge.

Aidha, IPU ni jukwaa linalowapa wabunge nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika majadiliano na maamuzi ya masuala ya kimataifa.

IPU ilianzishwa mwaka 1889, ikiwa ni taasisi ya kwanza duniani kuwaleta pamoja wabunge wa mataifa tofauti.

Wazo la kuanzishwa kwake lililenga kutumia mijadala ya kibunge badala ya migogoro ya kivita katika kutatua changamoto za kimataifa.

Hadi sasa, IPU ina zaidi ya mabunge wanachama 180, hatua inayoiweka kuwa jukwaa muhimu la kisiasa la mabunge duniani.

Tanzania ilijiunga na IPU mwaka 1962, muda mfupi baada ya uhuru, na imekuwa mshiriki hai katika shughuli zake kwa miongo kadhaa.

Mikutano mikuu ya IPU hufanyika kwa utaratibu maalumu ambapo huwakutanisha wabunge kutoka nchi wanachama kujadili ajenda za kimataifa, kupitisha maazimio na kubadilishana uzoefu wa kibunge.

Katika historia ya karibuni, Tanzania iliandika ukurasa mpya ndani ya IPU baada ya Dk Tulia Ackson kuchaguliwa kuwa rais wa taasisi hiyo, katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 27, 2023 wakati wa mkutano mkuu wa 147 wa baraza hilo uliofanyika mjini Luanda, Angola.

 Katika uchaguzi huo, Tanzania iliweka alama ya kihistoria kwa kuwa na mwanamke kutoka Afrika kuongoza taasisi hiyo ya mabunge duniani.