Jamhuri bado inachunguza kesi ya uhaini inayomkabili Mkangara

Dar es Salaam. Mshtakiwa Nasrim Mkangara anayekabiliwa na kesi ya uhaini katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ataendelea kubaki rumande hadi Desemba 22, 2025 kutokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokukamilika.

Pia, shtaka la uhaini linalomkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Leo, Jumatatu Desemba 8, 2025 wakili wa Serikali, Cathbert Mbiling’i ameieleza Mahakama hiyo upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea.

Mbiling’i ametoa maelezo hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Hata hivyo, mshtakiwa hakuwepo mahakamani hapo kutokana na usafiri wa Magereza kupata hitilafu wakati akiwa njiani kuletwa mahakamani akitokea Gereza la Segerea.

“Mheshimiwa hakimu, kesi hii imeitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika na mshtakiwa hajaletwa Mahakama hapa kutokana na taarifa nilizopata kuwa usafiri wa Magereza umepata hitilafu ukiwa njiani kuja hapa mahakamani,” amedai wakili Mbiling’i

Amedai Mkangara ni miongoni mwa washtakiwa 48 waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya uhaini mahakamani hapo, hata hivyo, Novemba 24, 2025 Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) aliwafutia mashtaka washtakiwa 47 na kuwaachia.

“Hata hivyo, wakati hao washtakiwa 47 wakiachiwa huru, mshtakiwa mmoja pekee ndio amesalia katika kesi naye ni Nasrim Laurence Mkangara, ambaye DPP anaendelea na mashtaka dhidi yake,” alidai Wakili Mbiling’i.

Amedai kutokana na hali hiyo, aliomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Baada ya taarifa hiyo, hakimu Lyamuya ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 22, 2025 kwa kutajwa.

Kwa mara ya kwanza, Mkangara na wenzake walipandishwa kizimbani Novemba 10, 2025 na kusomewa kesi ya uhaini.

Katika kesi hiyo uchunguzi wa awali (PI) namba 26645 ya mwaka 2025, washtakiwa wote walisomewa mashtaka mawili; kula njama za kutenda uhalifu wa uhaini na shtaka la uhaini.

Wote kwa pamoja katika shtaka la kwanza walidaiwa kuwa kwa nyakati tofauti kati ya Aprili Mosi na Oktoba 29, 2025 walikula njama za kutenda kosa la uhaini.

Katika shtaka la pili, washtakiwa wote walidaiwa Oktoba 29, 2025 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, wakiwa chini ya utii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walitengeza nia kuzuia Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.

Washtakiwa hao walidaiwa kuwa walitengeneza nia hiyo kwa lengo la kuitisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuithibitisha nia hiyo kwa kusababisha hasara kubwa kwa mali za Serikali zilizokusudiwa kutoa huduma muhimu.