Dar es Salaam. Rais wa Benin, Patrice Talon amewatuliza wananchi wa taifa hilo wakati akizungumza mubashara kupitia televisheni ya taifa baada ya jaribio la mapinduzi lililotokea mapema Jumapili Desemba 7, 2025.
Akiwa na mwenendo wa utulivu wakati wa hotuba hiyo ya jioni, Talon alitangaza kuwa hali nchini humo ipo katika udhibiti kamili na kulipongeza jeshi kwa kutekeleza wajibu wake kikamilifu.
“Ningependa kupongeza moyo wa utendaji wa jeshi letu na viongozi wake ambao wameendelea kuwa waaminifu kwa taifa,” alisema Rais Talon.
Ameongeza kuwa: “Uaminifu huu na mwamko wa vikosi vyetu umetuwezesha kuwakabili wanaotafuta fursa na kuyaepusha madhara kwa nchi yetu. Usaliti huu hautaachwa bila adhabu.”
Serikali imesema imefanikiwa kuzima jaribio hilo ndani ya muda mfupi baada ya kundi la wanajeshi kujitangaza kutwaa madaraka kupitia televisheni ya taifa.
Katika mji mkuu wa kiutawala, Cotonou, milio mikubwa ya milipuko ilisikika mchana kutwa, inadaiwa kuwa ilitokana na shambulio la anga lililolenga waasi. Kabla ya tukio hilo, rekodi za usafiri wa anga zilionyesha ndege tatu zikitoka Nigeria kuingia Benin na kisha kurejea baadaye.
Msemaji wa Rais wa Nigeria, alithibitisha kuwa ndege za kivita za nchi hiyo ziliingilia kati kudhibiti anga na kuwafurusha wapanga mapinduzi kutoka kituo cha televisheni na kambi ya kijeshi walikokuwa wamejikusanya.
Jaribio hilo linaongeza msukosuko katika ukanda wa Afrika Magharibi ambao umeshuhudia mapinduzi kadhaa katika miaka ya karibuni.
Licha ya Benin kutambulika kwa muda mrefu kama demokrasia imara na koloni la zamani la Ufaransa, Rais Talon amekuwa akikumbwa na lawama za kuwabana wakosoaji wa serikali yake.
Benin ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa pamba barani Afrika, lakini uchumi wake bado unakabiliwa na changamoto kubwa huku taifa likiorodheshwa miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani.
