Matola aulizwa maswali mazito, Mnyama akipasuka kwa Azam FC

Mechi bora ya Ligi Kuu Bara imepigwa leo kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam na Azam kumaliza ubabe wa Simba kwa kuichapa mabao 2-0.

Huu ulikuwa mchezo muhimu kwa timu zote kuhakikisha zinajiweka kwenye mazingira mazuri kwenye Ligi Kuu lakini pamoja na kosakosa za kila mara bado timu zote zilishindwa kutikisa nyavu  katika dakika 45 za mwanzo, lakini mashabiki waliohudhuria uwanjani walishuhudia moja ya mchezo bora zaidi kwenye ligi msimu huu.

Kabla ya mchezo huu, Simba ilikuwa haijadondosha pointi yoyote kwenye ligi ikiwa na ushindi kwa asilimia 100 kwenye michezo minne, lakini sasa imekuwa sawa na timu nyingine nyingi kwenye ligi hiyo.

KWA 01

Katika mchezo huo, Japhet Kitambala wa Azam alikuwa mwiba mchungu kwa Simba kutokana na kupiga mipira mitatu ya vichwa ambayo yote iliokolewa na kipa bora wa mchezo huo Yakoub Suleimani ambaye alionyesha kiwango bora zaidi.

Hata hivyo dakika ya 82 alionyesha makali yake baada ya kufunga bao safi akipokea pasi nzuri ya Nassoro Saadun, ambapo dakika chache baadaye Idd Nado aliifungia timu yake bao la pili kwa kutumia makosa ya mabeki wa Simba.

KWA 02

Kwa upande wa Azam, walikuwa na wakati mgumu sana wa kumbana kiungo mshambuliaji wa Simba Elli Mpanzu ambaye alikuwa na kiwango bora zaidi kwenye mchezo huo huku mashuti yake mawili ya kila kipindi yakigonga mwamba.

Huu ni ushindi wa kwanza kwa Azam kwa michezo ya hivi karibuni, baada ya mechi yao ya mwisho ya ligi msimu uliopita kumalizika kwa sare ya mabao 2-2, hali ambayo ilianza kupoteza matumaini ya Simba ya kutwaa ubingwa ambao ulikuja kuchukuliwa na Yanga kwa tofauti ya pointi nne.

Matokeo haya yalikuwa mazuri kwa Azam ambayo awali ilikuwa imeshinda mchezo mmoja tu wa Ligi Kuu msimu huu kati ya minne iliyokuwa imecheza na kutoka sare mitatu.

KWA 03

Hata hivyo, kwenye rekodi Simba imeonekana kuwa na historia nzuri katika mechi dhidi ya Azam na kuthibitisha hilo, walikuwa hawajapoteza mechi sita mfululizo za Ligi Kuu dhidi ya timu hiyo inayonolewa na Florent Ibenge ambapo tangu Simba ilipofungwa bao 1-0 na Azam FC, Oktoba 27, 2022, imeshinda mechi mbili zilizofuata na kutoka sare nne lakini sasa ubabe huo umezimwa.