MABOSI wa Simba wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Crescentius Magori, muda wowote kuanzia kesho Jumatatu wataitisha kikao kizito ili kuamua hatma ya kocha mpya, huku kukiwa na pande mbili za msako wa kubeba mikoba ya Dimitir Pantev aliyeondoka hivi karibuni.
Awali Mwanaspoti lilipenyezewa taarifa kwamba Simba kupitia kigogo wa zamani wa klabu hiyo, imeanza mazungumzo na kocha Antonio Casano Cantos kutoka Hispania akiwa na sifa za kufundisha soka Angola na Morocco kupitia timu za Petro Atletico na Moghreb Atletico Tetouan.
Hata hivyo, taarifa zaidi zilizolifikia Mwanaspoti ni kwamba mbali na kocha huyo, mchakato wa kumsaka mrithi wa kuziba nafasi ya Pantev umesukiwa mikakati tofauti ikiwamo kupitia kikao hicho ambacho mbali na Magori, kitahusisha vigogo wengine na kitafanyika katika moja ya hoteli yenye hadhi ya nyota tano ikihusisha pia Wajumbe wa Bodi upande wa Mwekezaji Mohammed ‘MO’ Dewji na wale wote wa klabu chini ya Mwenyekiti Murtaza Mangungu.
Taarifa hizo kutoka ndani ya Simba zinasema pande hizo mbili zitakapokutana mezani kwao yatawekwa majina ya makocha waliotuma kabla ya kuteuliwa wasiopungua watatu likiwamo la Steve Barker wa Stellenbosch ya Afrika Kusini likipewa nafasi kubwa kwani kuna kigogo mmoja ameshawasilisha wasifu wake.
Pia kuna majina mengine mawili, likiwamo la kocha atakayeletwa na upande wa klabu chini ya Mangungu na mabosi watayajadili na kila mmoja atakuwa na kazi wa kuwasilisha ufundi kama uliopo katika wasifu wao (CV) yakiwamo masuala ya mbinu, mifumo ambayo timu itacheza uwanjani pamoja na mambo mengine ya msingi ya aina hiyo.
Katika uwasilishaji huo kwa makocha hao watatu watakaopita katika mchakato huo, watafanyiwa uchunguzi na mmoja ambaye atakuwa bora kati ya hao atapewa mikoba ya kuinoa Simba akishirikiana na Selemani Matola anayekaimu nafsi hiyo kwa sasa.
Hata hivyo, Mwanaspoti linafahamu kuna baadhi ya mabosi hasa wale wa upande wa klabu wameanza kuingiwa na mawazo ya kuwashawishi wenzao kuwa, Matola aachiwe timu kutokana na kukidhi vigezo vya sifa za kuwa kocha mkuu pamoja na uzoefu alionao klabuni kwa muda mrefu.
Hivyo, sio ajabu kama makocha wanaopigiwa hesabu wakaishia kufanyiwa usaili na kisha kupigwa chini ili Matola apewe timu jumla.
Matola anapigiwa chapuo zaidi kulingana na ukweli anaonekana ni kocha mwenye sifa na pengine asiweze kuikamua kiasi kikubwa cha fedha kulinganisha na makocha hao wa kigeni ambao taarifa zinadokeza wamewekewa dau maalumu ambalo uongozi hautaki livuke zaidi ya hapo.
Taarifa zaidi kutoka ndani ya Simba zinasema mara baada ya mchakato huo kukamilika kama ni kuletwa kocha mpya ataenda na timu katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 na kukiangalia kikosi kabla ya kutoa tathmini ya kuongeza wachezaji wapya kupitia dirisha dogo.
Dirisha dogo la usajili linatarajiwa kufunguliwa Januari Mosi 2026 na Simba imepanga kusikilizia mapendekezo ya kocha mpya au Matola kama atapenya kisha kujiweka tayari kwa mechi nne za Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi zikiwamo mbili za nje ndani dhidi ya Esperance ya Tunisia.
Simba ipo Kundi D, mbali na Esperance pia zipo Stade Malien ya Mali na Petro Atletico ya Angola ikisaka nafasi ya kucheza robo fainali kwa mara ya saba tangu 2018-2019.
