Arusha. Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, imemuachia huru Ernest Mashurano (71), aliyekuwa ameshtakiwa kwa mauaji ya binti yake, Namala Ernest (13), baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha kesi dhidi yake.
Mauaji hayo yalitokea Julai 15, 2024 katika Kijiji cha Kibimba wilayani Kyerwa mkoani Kagera, ambapo mwili wa Namala ulikutwa ukielea juu ya kisima cha maji kilichopo karibu na nyumbani alipokuwa akiishi na baba yake na mdogo wake, baada ya baba yake kutengana na mama yao.
Baada ya mwili wa Namala kuonekana ukielea kisimani hapo, taarifa zilimfikia baba yake ambaye alienda nyumbani na kuanza kuchimba kaburi, hali iliyosababisha wanakijiji wenzake kuchoma nyumba yake wakimtuhumu kuwa ni mchawi.
Hukumu hiyo imetolewa Novemba 7, 2025 na Jaji Immaculata Banzi aliyekuwa akisiliza kesi hiyo ya mauaji na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.
Katika hukumu hiyo, Jaji Banzi amesema baada ya kupitia ushahidi wa pande zote Mahakama inamkuta Ernest hana hatia ya mauaji kutokana na upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha kesi dhidi yake na kuamuru aachiwe huru.
Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi sita na vielelezo vinne, huku mshtakiwa aliyekuwa shahidi pekee wa upande wa utetezi.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alikuwa akiishi na watoto wake wawili, Namala na Albinus Ermest (ambaye alikuwa shahidi wa tatu) na kuwa kila mmoja alikuwa akilala chumbani kwake.
Albinus alidai kuwa usiku wa tukio, wakati kila mtu amelala, Namala alimuomba afunge mlango kwani alikuwa akienda chooni kujisaidia na alitii na kufunga mlango kisha kurudi kulala.
Alidai asubuhi iliyofuata, mshtakiwa aliwaamsha kwenda shuleni na aliondoka kwenda shamba bila kuona kama walikuwa wameamka au la na baada ya hapo, wanawake wawili walienda kuchota maji kwenye kisima cha maji kilicho karibu na nyumbani kwao, ambapo walimkuta marehemu akielekea kwenye kisima hicho.
Shahidi huyo alidai kujulishwa na kukimbia kumwita mshtakiwa ambaye alipofika eneo hilo na alipoona mwili wa mwanaye alirudi nyumbani na kuanza kuchimba kaburi, ambapo watu walianza kumtukana wakimwita mchawi kisha kuchoma nyumba yake.
Ilidaiwa wananchi hao walitaka kuchoma nyumba ya pili ya mshtakiwa ambapo walimpiga wakimtuhumu kwa uchawi kisha kumpeleka kituo cha Polisi Mabira.
Baada ya kupata taarifa hizo askari polisi Sajenti Ibrahim na G.6112 Sajenti Mustapha, walienda eneo la tukio wakiwa wameambatana na daktari, Ramadhan Mrisho ambaye alikuwa shahidi wa pili wa Jamhuri.
Askari hao walipofika eneo la tukio walifanikiwa kudhibiti fujo na kwenda kwenye kisima cha maji ambapo walikuta mwili wa marehemu ukielea.
Kwa mujibu wa shahidi wa nne na wa tano, kisima hicho kilikuwa na maji yalikuwa kidogo hivyo mwili wote ulionekana ambapo marehemu aliyekuwa amevalia sketi ya shule alikuwa amelala kwa tumbo.
Askari polisi wakisaidiwa na wanakijiji waliingia kisimani na kuutoa mwili huo, ambapo shahidi wa pili aliuchunguza mwili na kueleza kukuta michubuko kwenye shingo, mguuni na damu kwenye mapaja, huku sehemu zake za siri kukiwa na mbegu za kiume na michubuko.
Alidai mbali na hayo kulikuwa na michubuko kwenye sehemu ya juu ya uke, huku sehemu yake ya haja kubwa kukiwa na kinyesi.
Shahidi huyo alidai kutumia vifaa maalumu vya kukusanya sampuli kutoka sehemu mbalimbali za mwili wa marehemu ikiwemo sehemu za siri na shingoni kisha kuziweka kwenye chombo maalumu.
Alidai kuzikabidhi kwa ofisa wa polisi, Jimmy Brighton ambaye alizikabidhi kwa shahidi wa nne.
Shahidi huyo wa pili alihitimisha kuwa chanzo cha kifo ni kukosa hewa kutokana na kubanwa kwa shingo na kusababisha upungufu wa oksijeni kwenye ubongo, na mshtuko wa moyo. Huku uwepo wa michubuko sehemu zake za siri kulisababishwa na kuingiliwa na kitu butu.
Shahidi wa tano alidai kuchora ramani ya mchoro wa eneo hilo huku shahidi wa nne akihifadhi vielelezo kwenye friji vikisubiri kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, ambapo vielelezo hivyo vilipakiwa kwenye bahasha na mifuko ya nailoni.
Alidai Agosti 27,2024 aliagizwa kwenda Hospitali ya Wilaya ya Kyerwa kuchukua sampuli kutoka kwa mshtakiwa ambapo alikusanya kwa pamba ya mdomo na damu kutoka kwa mshtakiwa na kuwa Agosti 29,2024, alipeleka ofisi ya mkemia mkuu Mwanza.
Sampuli hizo zilisafirishwa hadi ofisi kuu ya mkemia jijini Dar es Salaam kwa uchunguzi wa vinasaba (DNA).
Shahidi wa sita, Anna Chuwa, alidai Septemba 2,2024 alipeleka vielelezo vitano ambapo A,B na C vikitoka kwa Namala huku D na E vikitoka kwa mshtakiwa.
Alidai katika uchanganuzi wake, kielelezo A lilithibitishwa kuwa na wamiliki zaidi ya mmoja, wa kike na wa kiume huku B na C yakitoka kwa mmiliki zaidi ya mmoja (wa kike na kiume).
Alidai DNA katika vielelezo D na E kutoka kwa mshtakiwa ililingana na DNA katika vielelezo A, B na C na uwezekano wa kuonyesha D na E kutohusiana na maelezo ya DNA katika vielelezo A, B na C ni moja katika bilioni.
Katika utetezi mshtakiwa alikana tuhuma hizo na kudai kuwa alikuwa akimpenda sana binti yake na amekuwa akimtunza tangu 2023, baada ya mama yake kuondoka na kwenda kuolewa na mtu mwingine.
Alidai kuwa ana watoto wengine ambao amekuwa akiwalea tangu mwaka 1995 mama yao alipofariki na hajawahi kuwanyanyasa hata mmoja wao.
Aliieleza mahakama kuwa siku ya tukio aliamka asubuhi kwa lengo la kwenda shambani, ila kabla ya kuondoka aliwaita watoto wake wajiandae kwenda shule wafunge mlango, lakini ni shahidi wa pili aliyeitikia.
Alidai baada ya hapo, alikwenda shambani na akiwa huko, shahidi wa tatu, alienda kumjulisha kuwa Namala amekutwa akielea kisimani na alipothibitisha alienda kumjulisha shahidi wa kwanza ambaye alitoa taarifa polisi.
Alidai mahakamani hapo kuwa watu walikusanyika na kuanza kumpiga kwa mawe wakimtuhumu kuwa muuaji wa binti yake, na kuwa aliwaonyesha ni wapi wangelichimba kaburi endapo atapelekwa polisi huku akikana kuchimba kaburi kama ilivyodaiwa na mashtaka.
Alidai kupelekwa Kituo cha Polisi Mabira na kutokana na majeraha kichwani, alipelekwa katika Kituo cha Afya cha Kamuli ambako majeraha yake yalishonwa na kuomba Mahakama imuachie huru, kwani hahusiki na mauaji hayo.
Jaji Banzi amesema baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, suala kuu la kuamuliwa ni iwapo kosa la mauaji dhidi ya mshtakiwa lilithibitishwa pasipo shaka yoyote.
Jaji amesema kuwa sheria inataka kabla ya kukusanya sampuli, ofisa sampuli anatakiwa kutoa taarifa kwa chanzo cha sampuli pamoja na mambo mengine, kupata kibali, sababu ya kuchukua sampuli na muhimu zaidi, inaweza kutumika kama ushahidi dhidi yake.
Jaji Banzi amesema ushahidi unaonyesha kuwa, mshtakiwa alikamatwa Julai 15, 2024 na kukaa mahabusu hadi Agosti 28, 2024 alipofikishwa mahakamani na kuwa inashangaza mshtakiwa kukaa chini ya ulinzi wa polisi mwezi mmoja na nusu bila kuchukuliwa sampuli hizo.
Amesema Mahakama imebaini mashaka kuhusu namna sampuli zilivyokusanywa, kuhifadhiwa na kusafirishwa ikiwemo kukosekana kwa kibali cha maandishi kama sheria inavyotaka, kutokuitwa maofisa muhimu waliohusika na usafirishaji wa sampuli, taarifa kupingana kuhusu ufungashaji wa sampuli.
Sababu nyingine ni ripoti ya DNA kuonyesha mbegu za kiume kwenye njia ya haja kubwa bila ushahidi wa kitu butu kupenya sehemu hiyo na kuwa mapungufu hayo yaliharibu mnyororo wa utunzaji wa sampuli, hivyo kufanya matokeo ya DNA kutoaminika.
Mahakama ilihitimisha kuwa ushahidi wa DNA hauwezi kuthibitisha pasipo shaka yoyote kwamba ni mshtakiwa ndiye aliyemuua Namala na kuamuru Ernest aachiliwe huru.
