Nahodha Geita Gold awashtua wenzake

NAHODHA Msaidizi wa Geita Gold, Saidy Mbatty amewataka wachezaji wenzake kuendelea kucheza kwa ushirikiano mkubwa hadi mwisho wa msimu, kwani kwa kufanya hivyo itakuwa ni njia nzuri ya kufanikisha malengo ya kuirejesha timu hiyo Ligi Kuu.

Nyota huyo aliyejiunga na kikosi hicho msimu huu akitokea Fountain Gate, amesema mwenendo wa timu ni mzuri, ingawa wanahitaji kufanya vizuri zaidi, kwa sababu ni mapema na ushindani umekuwa ni mkubwa kutokana na kasi ya wapinzani wao.

“Nina uzoefu mkubwa na Championship ndio maana naongea hivyo, ukiangalia mwenendo wetu hadi sasa ni mzuri ila wapinzani pia wanafanya vizuri, hii inaonyesha hatupaswi kubweteka na hapa tulipo zaidi ya kuendelea kupambana,” amesema Mbatty.

MBAT 01

Nyota huyo wa zamani wa TRA United zamani Tabora United, amesema gepu la pointi lililopo na washindani wao ni njia nzuri kwao wachezaji kuendelea kupambana zaidi ya sasa, licha ya upinzani mkubwa uliopo hususani wanapocheza mechi za ugenini.

Geita iliyoshuka daraja msimu wa 2023-2024, msimu wa 2024-2025 wa Ligi ya Championship ilimaliza nafasi ya nne na pointi 56, chini ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Mohamed Muya na kushindwa kupanda Ligi Kuu Bara, baada ya kufeli mechi za mchujo.

Timu hiyo ilicheza mchujo upanda Ligi Kuu Bara dhidi ya Stand United ‘Chama la Wana’ iliyomaliza nafasi ya tatu na pointi 61 na kushuhudia ikiondoshwa kwa jumla ya mabao 4-2.