Serikali yaja na mkakati kukomesha uagizaji bidhaa nje

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema Serikali imepanga kuokoa Sh2.8 trilioni kutokana na uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Amesema utekelezaji wa hilo utafanyika kwa Serikali kuhakikisha bidhaa nane kati ya 96 zinazoagizwa nje ya nchi zinaanza kuzalishwa nchini kupitia wawekezaji.

Hatua hiyo ya Serikali inakuja wakati ambao, mwaka 2024, bidhaa 96 ziliagizwa kutoka nje ya nchi ambazo thamani yake ni Sh15 trilioni.

Profesa Kitila ametoa kauli hiyo leo, Jumatatu Desemba 8, 2025, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu vipaumbele na fursa za vijana katika wizara anayoiongoza.

Amezitaja baadhi ya bidhaa hizo nane zitakazozalishwa nchini na kuacha kuagizwa kutoka nje ya nchi kuwa ni sukari, akisema kwa wawekezaji waliopo sasa, kuanzia mwakani, Tanzania itajitosheleza kwa zao hilo.

“Kuanzia mwakani hakutakuwa na uhitaji wa kuagiza sukari nje ya nchi, zaidi tutakuwa na kazi ya kutafuta masoko kwa ajili ya kuuza ziada itakayozalishwa ndani,” amesema.

Bidhaa nyingine aliyosema itazalishwa ndani ni mafuta ya kupikia. Kazi hiyo itaanza kwa kuanzisha viwanda na mashamba maalumu kwa ajili ya uzalishaji wa alizeti na kuzalisha mafuta hayo.

“Changamoto tuliyonayo ni kwamba tuna viwanda vya alizeti, lakini hatuna malighafi, kwa hiyo mkakati tunaokuja nao ni wenye viwanda kuwa na mikataba na wakulima kama inavyofanyika kwenye miwa,” amesema.

Profesa Kitila amesema ngano ni bidhaa nyingine ambayo Serikali imepanga kuiondoa katika orodha ya zile zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.

“Ingawa uzalishaji wa ngano ni mdogo nchini, juhudi zinafanyika kuvutia uwekezaji wa kilimo cha ngano na kuweka nguvu ya ziada ili tujitegemee,” ameeleza.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof Kitila Mkumbo akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu, Desemba 8, 2025 Dar es Salaam. Picha na Said Khamis

Maeneo mengine aliyosema Serikali inapanga kuondokana na uagizaji nje ya nchi ni ufugaji, akidokeza kutaanzishwa maeneo ya malisho na ranchi na kubadili uchungaji kuwa ufugaji ili ng’ombe mmoja azalishe maziwa ya kutosha.

Amesema changamoto iliyopo ni kwamba tayari kuna viwanda vya kutosha, lakini wawekezaji wanakosa malighafi, hivyo ranchi zitabadilishwa ili ziendeshwe kibiashara.

Uvuvi ni eneo lingine alilolitaja, akisema lengo ni shughuli hizo kufanyika katika kina kirefu na ufugaji samaki, hasa wa vizimba, uzingatiwe.

Profesa Kitila amesema sekta ya utalii ni eneo lingine linalotarajiwa kuboreshwa ili kujitegemea, kwa kuhakikisha vivutio vipya takribani vitano vinafunguliwa na kukuzwa kama ilivyo vya ukanda wa Kaskazini.

Katika sekta hiyo, amesema utalii wa fukwe bado haujatumika vema, hivyo Serikali itashirikiana na sekta binafsi kuhakikisha unatumika ili kufungua ajira kwa vijana.

Eneo lingine, amesema, ni ujenzi wa majengo, kumbi za mikutano na ofisi, na kwamba miji itaanza kuhuishwa na kupangwa upya.

“Tunahusisha sekta binafsi. Inakuja, tunaiunganisha na wenye nyumba. Zibomolewe, yajengwe maghorofa. Mtu anakuja anakujengea nyumba, anakupa ghorofa moja, kuna ubaya?” amesema.

Mpango huo kwa Dar es Salaam, amesema, unaanzia katika maeneo ya Vingunguti, Manzese na Buguruni, na kwamba wawekezaji wanaendelea kutafutwa kufanikisha hilo.

Akizungumzia hilo, mtaalamu wa uchumi, Profesa Benedict Mongula amesema mafanikio ya mkakati huo yatategemea zaidi kupatikana kwa wawekezaji, hasa sekta binafsi.

“Hili linaihitaji zaidi sekta binafsi. Ili kuivutia sekta binafsi, ni muhimu Serikali irahisishe mazingira ya uwekezaji. Kwa hiyo jambo muhimu ni kurahisisha mazingira ya uwekezaji,” amesema.

Utekelezaji wa mkakati huo, Profesa Kitila amesema, unaendana na hatua za dhati za Serikali kuvutia uwekezaji kwa kuimarisha Kituo cha Mahala Pamoja ili kumwezesha mwekezaji kupata huduma zote katika eneo moja.

“Taasisi zote zinazotoa huduma ziwepo pale na ziwe na mamlaka kamili. Kwa hiyo kama ni suala la kupata hati, upate hati na uondoke, kama ni kusajili biashara, isajiliwe na ukitoka hapo unaondoka,” amesema.

Sambamba na hilo, amesema Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza) imepewa jukumu la kuanzisha benki ya ardhi, na hadi sasa inamiliki hekta 170,176.96 kwa ajili ya uwekezaji.

Kati ya hekta hizo, amesema mashamba ya jumla ni hekta 78,444, na yaliyotoka kwenye taasisi za Serikali ni 56,209, huku kutoka sekta binafsi ni mashamba 124.

“Unaweza kuwa na shamba kubwa, unaliwasilisha Tiseza, wanakusaidia kutafuta mwekezaji. Akipatikana mnashirikiana,” amesema.

Amesema tayari maeneo maalumu ya kiuchumi yamefikia 34 sawa na hekta 22,623.7 kati ya hayo 15 yanamilikiwa na Tiseza, manne na Serikali za mitaa na mengine sekta binafsi.

“Changamoto ya ardhi ya uwekezaji imepungua sana baada ya Serikali kuanzisha benki ya ardhi, na tunawasihi watu wenye ardhi kuhakikisha wanawasilisha mashamba yao ili wapate wawekezaji kwa kushirikiana na Tiseza,” amesema.

Mengine yatakayofanyika, amesema, ni kuanzishwa kwa jukwaa la uwekezaji la kitaifa na kuanzia Januari, kwa kushirikiana na mawaziri wenzake, atakutana na wawekezaji kila baada ya miezi mitatu kusikiliza changamoto zao na kuzitatua.

Amesema badala ya kukutana nao mara moja kwa mwaka, kwa sasa watakuwa wanawasikiliza kila baada ya miezi mitatu.

Hata hivyo, amesema miradi ya uwekezaji itachaguliwa kwa kuzingatia iwapo mradi husika utazalisha ajira, kuongeza mauzo ya bidhaa za Tanzania nje na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine.

Pia, itaangaliwa nafasi ya uwekezaji husika katika kuongeza thamani, kwa kuwa mpango wa Serikali ni kusafirisha bidhaa zikiwa zimeongezwa thamani.

“Ndio maana tunasisitiza wawekezaji wakija hapa, katika upande wa madini, waje kuongeza thamani,” amesema.

Lingine, amesema, ni fursa ya sekta katika kukuza mapato ya Serikali na uwekezaji katika kilimo na uchakataji wa mazao yake.

“Tukitathmini uwekezaji wako tunajua kuwa utaiingizia Serikali kodi ya kutosha, mradi wako utapewa kipaumbele,” amesema.

Kuhusu utulivu wa kisiasa

Kwa kuwa uwekezaji unategemea utulivu wa kisiasa, Profesa Kitila amesema ni kawaida kila nchi duniani kupitia kipindi cha majaribu na kwamba lazima kivuke.

“Kila nchi ina kipindi chake cha majaribu na kipindi chake kigumu. Basi nasi tupo katika kipindi hicho, na hilo tutalitibu, tutalishinda jaribu hilo na tutakuwa nchi moja yenye maelewano,” amesema.

Amesema kuhusu matamko ya jumuiya za kimataifa, utafanywa utaratibu wa kuhakikisha Serikali inawasilisha upande wake na kufikia muafaka tarajiwa.

Amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anajivunia utaifa wake na kunufaika na fursa na rasilimali zilizopo.

Katika hatua nyingine, amesema Serikali inakuja na mfumo mpya wa upimaji wa utendaji wa mashirika ya umma ili kuona kwa kiwango gani yanatimiza majukumu yake.

Amesema baadhi ya mashirika ya umma yatatakiwa kujisajili katika soko la hisa ili Watanzania wanunue hisa na kumiliki mashirika hayo, hivyo kuongeza uwazi katika uendeshaji wake.

Pia, amesema kutawekwa masharti kwa watendaji wakuu na wajumbe wa bodi za mashirika hayo kupatikana kwa njia ya ushindani wataomba na kushindanishwa.

“Sheria ikipitishwa Julai mwaka huu, ukitaka kuwa mkurugenzi utaomba na utaingia kwenye mchakato wa ushindani,” amesema.

Ameeleza kuwa chanzo mahsusi cha kupata mitaji kwa mashirika ya umma yanayofanya biashara kitaanzishwa ili kuhakikisha yanaendelea kuwa na mitaji ya kutosha.

Ili kuchochea uwekezaji wa tija na kutoa fursa kwa vijana, amesema Serikali inaanzisha kituo cha kuhudumia na kuwezesha vijana katika eneo la EPZA ili kuwapa maarifa ya uwekezaji.

Programu maalumu, amesema, inaanzishwa kwa ajili ya vijana kuwawezesha wawekezaji vijana wakabuni na kuanzisha miradi ya kuwekeza.

Baada ya mafunzo, amesema, vijana watawezeshwa kufungua kampuni, kisha watakabidhiwa eneo na kuunganishwa na wenye mitaji.

“Tunataka mwekezaji wa sekta binafsi awekeze kwa kujenga mitambo, lakini ndani mule awakabidhi vijana, mfano kiwanda cha kuzalisha nguo au bidhaa yoyote,” amesema.

Amesema Serikali itaweka miundombinu mbalimbali na vijana watapangishwa katika maeneo hayo ili kuzalisha ajira.

Amesema tayari Serikali imezungumza na taasisi mbalimbali za fedha na zimekubali.

Amesema tayari ekari 100 zimetengwa Nala, Pwani ekari 20, Mara ekari 100, Ruvuma ekari 100 na Bagamoyo ekari 20 kwa kuanzia.

Maeneo hayo matano yenye jumla ya ekari 340 ni kwa ajili ya vijana wanaomaliza vyuo vikuu, hasa vile vya ufundi kuwekeza.

“Kwa kufanya hivi, nadhani tutabadili mtazamo kwamba ajira ni serikalini pekee. Pia, badala ya kuajiriwa wakajiajiri na kuajiri wengine,” amesema.