KIPA Aishi Manula amerejea uwanjani akiea na jezi ya Azam. Kwa mara ya kwanza kocha Florent Ibenge alimtumia katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa Desemba 3, 2025 dhidi ya Singida Black Stars na jamaa akatoka na clean sheet baada ya timu hizo kushindwa kufungana.
Sasa kama hujui ni kwamba mechi hiyo ilihitimisha siku 637 za kipa huyo kukaa nje bila kucheza katika mechi za Ligi, kwani mara ya mwisho kuonekana uwanjani na kudaka ilikuwa ni Machi 6, 2024 wakati Simba ikipasuka uwanja wa nyumbani kwa mabao 2-1 mbele ya Tanzania Prisons.
Katika mechi hiyo, Manula alikaa langoni ikiwa ni tangu alipofungwa mabao 5-1 na Yanga kwenye Dabi ya Kariakoo iliyopigwa Novemba 5, 2023. Siku hiyo dhidi ya Prisons, Samson Mbangula akamharibia kwa kumtungua mara mbili, huku bao la kufutia machozi la Simba likifungwa na Fabrice Ngoma.
Siku hizo 637 kwa Manula ilikuwa ni safari ndefu iliyofunikwa na ukimya wa jeraha, pia kutokuaminiwa na kusihai kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu, hekaheka za presha ya mashabiki, na mapambano ya ndani ambayo hayakusemwa hadharani.
Wakati mwingine, siku hizo zilionekana kama hukumu isiyo na mwisho enzi hizo akiwa Simba na haikushangaza kuona msimu mzima akishindwa kupangwa katika mechi yoyote ya mashindano zaidi ya kudaka kwa dakika 45 dhidi ya Al Hilal ya Sudan katika mechi ya kirafiki pale KMC Complex.
Kukaa kwake nje kwa muda huo ambao ni karibu miaka miwili kasoro siku 93, kumezigusa Simba, Yanga na hata mamlaka za soka nchini kutokana na matukio yaliyotokea kipindi hicho.
Mwanaspoti inakuletea matukio yaliyotokea katika soka wakati kipa huyo akiwa nje ya uwanja kabla ya Ibenge kumrejesha uwanjani dhidi ya Singida na leo dhidi ya Simba akiwa benchi katika mechi ya Dabi ya Mzizima.
YANGA MATAJI SABA
Yanga ndio iliyotajwa sababu ya Manula kupoteza ufalme Msimbazi kutokana na kumtungua mabao 5-1 akiwa na Simba kisha Mbangula kumtibulia tena na kuwekwa benchi hadi alipomaliza mkataba na kurejea Azam baada ya kupita miaka nane tangu alipohama msimu wa 2017-2018.
Kwa kipindi chote ambacho Manula akiwa nje ya uwanjani, Yanga imefanikiwa kutwaa mataji saba tofauti, ikiwamo ubingwa wa Ligi Kuu mara mbili msimu wa 2023-2024 na 2024-2025, michuano ya Kombe la Shirikisho pia mawili ya msimu wa 2024-2023 na 2024-2025 na Ngao za Jamii mbili za mwaka 2024 na 2025 pamoja na Kombe la Muungano 2025.
Kitu cha ajabu ni kwamba katika kipindi chote hicho, timu aliyokuwa akiitumikia ilitwaa taji moja tu Kombe la Muungano 2024, lakini timu hiyo ikichapika mechi tano mfululizo mbele ya watani wao hao.
YANGA MAKUNDI MARA TATU
Licha ya kuwa na rekodi tamu za kuipeleka Simba robo fainali akiwa kikosi cha kwanza kabla ya kuwekwa benchi na Moussa Camara, kipa huyo ameshuhudia akiwa benchi Yanga ikiandika rekodi ya kutinga makundi Ligi ya Mabingwa Afrika mara tatu ikiwamo moja iliyosonga hadi robo fainali.
Yanga kuanzia 2016 hadi sasa imecheza makundi mara sita, lakini tatu zikiwa za Kombe la Shirikisho misimu ya 2016, 2018 na 2022-2023 ilipofika fainali na mara tatu kwa Ligi ya Mabingwa ikiwa mfululizo misimu ya 2023-2024, 2024-2025 na sasa 2025-2026.
Rekodi zinaonesha Simba hii ni mara ya saba katika kipindi cha miaka nane ambapo mbili ilikuwa upande wa Kombe la Shirikisho (2021-2022 na 2024-2025) huku Ligi ya Mabingwa ni (2018-2019, 2020-2021, 2022-2023, 2023-2024 na sasa 2025-2026).
Kwa rekodi hiyo ya Simba Manula amekosekana misimu miwili tu huku misimu mingine yote akiwa ameandika rekodi ya kukaa langoni.
VIPIGO VITANO MSIMBAZI
Licha ya kutupiwa mzigo wa lawama baada ya kichapo cha mabao 5-1, Manula akiwa benchi kwa siku 637 ameishuhudia timu ya Simba ikichezea vichapo mara tano kutoka kwa Yanga kuonyesha kuwa, tatizo halikuwa lake tu mbele ya Vijana wa Jangwani.
Baada ya kipigo hicho cha mabao 5-1 katika mechi ya Novemba 5, 2023, Manula alikuwa benchi Simba ilipopasuka 2-1 katika mechi ya marudiano , kisha kufuatiwa na kipigio cha 1-0 cha Ngao ya Jamii 2024, kabla ya kupigwa tena nje ndani katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita na hata msimu huu Simba ilikufa tena kwa bao 1-0 mechi ya Ngao ya Jamii 2025 iliyopigwa Septemba 16.
AZAM FC MAKUNDI
Alikuwa sehemu ya nyota walioipa Azam FC ubingwa wa Ligi Kuu 2014 na kurejea tena kwenye kikosi hicho kikiwa katika kilele cha mafanikio msimu huu kwa kutinga hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika.
Licha ya kuwa sehemu ya kikosi cha Azam FC msimu huu, kipa huyo hajapata nafasi ya kucheza kimataifa lakini ameingia kwenye rekodi ya kuwa miongoni mwa wachezaji walioifikisha Azam FC hatua ya makundi baada ya miaka 21.
Msimu huu Azam FC ikiwa chini ya kocha mwenye rekodi kubwa soka la Afrika, Florent Ibenge ameisaidia timu hiyo kuandika rekodi ya kutinga hatua ya makundi kwa mara ya kwanza tangu ipande daraja ikitwaa taji moja la ligi.
Wakati timu hiyo inaandika rekodi hiyo kipa Manula alikuwa bado hajapata nafasi ya kucheza hadi hapo aliposimama langoni akiwa na mwaka mmoja tangu alipocheza mechi ya ligi akiwa na Simba mchezo dhidi ya Tanzania Prisons na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili mchezo ulipigwa Machi 6, 2024.
SIMBA FAINALI SHIRIKISHO
Yanga na Simba zinaendelea kuwa kwenye vitabu vya kumbukumbu za soka la Tanzania kwamba ndiyo timu zilizocheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Ilianza Yanga kucheza fainali ya michuano hiyo msimu wa 2022-2023 na kupoteza kwa kanuni ya bao la ugenini dhidi ya USM Alger ya Algeria kufuatia matokeo ya jumla kuwa 2-2. Mechi ya kwanza nyumbani Yanga ilifungwa 2-1, ugenini ikashinda 1-0. Hii haiingii kwenye matukio ya Manula kwani tayari alikuwa anacheza.
Kwa upande wa Simba, imecheza fainali msimu uliopita 2024-2025 dhidi ya RS Berkane ya Morocco, ikiwa imepita misimu miwili tu tangu Yanga ifanye hivyo. Simba ilipoteza fainali kwa jumla ya mabao 3-1, mechi ya kwanza ugenini nchini Morocco ilifungwa 2-0, nyumbani ikatoka sare ya 1-1.
GAMONDI AENDA NA KURUDI
Miguel Gamondi ni kocha mkuu wa Singida Black Stars tayari ameandika rekodi mbili akiipa timu hiyo taji la Kagame Cup na kuifikisha hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika.
Gamondi amefikia rekodi hiyo baada ya kurudi tena nchini kwa mara ya pili baada ya awali kuwa kocha mkuu wa Yanga akiipa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na kuifikisha timu hiyo hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza.
Kocha huyo aliondoka Yanga akiwa amechukua mataji matatu na timu hiyo akianza na Ligi Kuu Bara msimu 2023 na kukifanya kikosi hicho kufikisha jumla ya mataji 30, tangu mwaka 1965, akachukua pia Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ngao ya Jamii kwa msimu 2024. Gamondi aliipeleka timu hiyo hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza baada ya miaka 25, kufuatia kufanya hivyo mara ya mwisho 1998.
Sasa kocha huyo amerejea na Manula amepata nafasi ya kucheza dhidi ya timu anayoinoa ya Singida Black Stars akiwa tayari amemaliza siku hizo 638, ni sawa na mwaka mmoja, miezi minane na siku 28 ambapo Manula alikuwa akiishia benchi au jukwaani bila ya kuvuja jasho katika mechi za klabu.
Gamondi alijiunga na Yanga Juni 24, 2023 akichukua nafasi ya Mtunisia Nasreddine Nabi aliyeipa mataji mawili ya Ligi Kuu, mawili ya Kombe la Shirikisho (ASFC), mawili ya Ngao ya Jamii na kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
MAKIPA WAPISHANA SIMBA
Manula aliyekuwa kipa namba moja wa Simba mara baada ya kupata shida ya kuwekwa benchi kwa mwaka mzima klabu hiyo, ilisajili makipa wapya watatu akiwamo Ayoub Lakred na Moussa Camara hawa ndio walimweka benchi sambamba na Ally Salim aliyehama kwa sasa kwenda Dodoma Jiji na kumpisha Yakoub Suleiman.
Kwa sasa Camara anajiuguza jeraha la goti ambalo limemuweka nje kuanzia mwanzo wa msimu huu akiwa tayari ameitumikia Simba kwa msimu mmoja na kufanikiwa kuibuka kipa bora wa msimu uliopita kabla ya Yakoub kutua na sasa kutumika kama kipa namba moja akimweka benchi Hussein Abel aliyecheza pia pamoja na Manula.
MAKOCHA WALIOPITA
Ni makocha wanne wamepita Simba ndani ya mwaka mmoja, miezi minane na siku 28 ambapo Manula alikuwa akiishia benchi au jukwaani bila ya kuvuja jasho katika mechi za klabu akiwa Simba na Azam FC.
Makocha hao ni Dimitar Pantev aliyetambulishwa Oktoba 3, 2025 kama Meneja Mkuu mwenye taaluma ya ukocha, ameiongoza timu hiyo katika mechi tano za mashindano ikiwamo moja ya Ligi Kuu Bara na nne za Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya Desemba 2, 2025 kusitishiwa mkataba.
Kutoka Oktoba 3, 2025 hadi Desemba 2, 2025 ni siku 61 zilizohitimisha maisha ya Mbulgaria huyo ndani ya Simba baada ya uongozi wa klabu kusitisha mkataba kwa makubaliano ya pande mbili na Matola amekaimishwa na kuingoza timu kwa sasa ikielezwa anatafutwa kocha mpya.
Fadlu Davids ambaye alijiunga na Simba Septemba 22, 2025 na mkataba wake na Simba kufikia tamati baada ya kocha huyo raia wa Afrika Kusini kujiunga rasmi na Raja Casablanca ya Morocco aliyokuwa akiinoa awali kabla ya kuja Tanzania. Aliitumikia kwa siku 444 tu na kurejea Raja ambako siku za nyuma alikuwa kocha msaidizi. Fadlu na wasaidizi wanne kuondoka kulitokea siku sita tu baada ya mchezo wa watani wa jadi, Simba na Yanga ‘Dabi ya Kariakoo’ uliochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Septemba 16, 2025 na timu kubaki mkononi mwa Matola kabla ya kuletwa kwa Pantev.
Abdelhak Benchikha, raia wa Algeria alijiunga na kikosi hicho Novemba 24, 2024 akitoka kuipa USM Alger ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuibwaga Yanga kwa faida ya mabao mengi ya ugenini kufuatia sare ya 2-2 na kubeba pia CAF Super Cup kwa kuifunga Al Ahly ya Misri.
Simba ilisitisha mkataba na kocha huyo kwa kile kinachofahamika ni kutokana na matatizo ya kifamilia ya kuuguliwa huko Algeria, akiwa amedumu kwa siku 156 tangu alipotambulishwa akichukua nafasi ya Roberto Oliveira ‘Robertinho’ na timu kuachwa chini ya Selemani Matola.
Tangu alipokuwa na Simba, Benchikha aliiongoza timu hiyo katika mechi 21 katika mashindano mbalimbali ikiwemo ya Ligi Kuu Bara, Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ligi ya Muungano iliyorejea mwaka huu. Katika Ligi Kuu aliiongoza mechi 11, timu ikishinda sita, kutoka sare tatu na kupoteza mechi mbili ikifunga mabao 18 na kufungwa manane.
