Spika Zungu ataka huduma ya viungo bandia ipewe kipaumbele

Dar es Salaam. Spika wa Bunge la Tanzania, Azzan Zungu, ameitaka Serikali kuweka mkazo katika huduma ya miguu bandia ili kuwasaidia wahitaji wenye ulemavu nchini.

Amesisitiza haja ya kuendeleza huduma hata baada ya wataalamu wa nje wanaotoa huduma hizo kuondoka nchini.

Wito huo ameutoa leo Jumatatu, Desemba 8, 2025 alipofanya ziara katika kambi maalumu ya utoaji viungo bandia bure kwa wenye uhitaji inayoendelea Masaki jijini Dar es Salaam, ambapo ameshuhudia mahitaji makubwa ya huduma hiyo yakizidi uwezo wa bajeti iliyopo.

Kambi hiyo ya miezi miwili iliyoanza Novemba 26, 2025 ikitolewa kwa ushirikiano wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Taasisi ya Kisukari na madaktari kutoka India, inaendelea kutoa huduma zake kwa wenye uhitaji.

Akiwa kambini hapo, ametembelea ukumbi maalumu ambapo miguu hiyo bandia inatengenezwa na kupata maelezo jinsi huduma hizo zinavyotolewa.

Aidha, amewatembelea na kuzungumza na Watanzania wanaopata huduma hizo katika kambi hiyo.

Akizungumza katika kambi hiyo, Spika Zungu amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali ya India kwa kuridhiana na kutoa huduma hiyo yenye gharama kubwa bila malipo kwa Watanzania.

“Nitamwomba Waziri wa Afya aje hapa aone kazi nzuri inayofanyika, ili wakishaondoka hawa nasi tuendeleze,” amesema.

Spika Zungu amesisitiza watoa huduma hao kutoka India hawatakaa nchini milele akitoa wito kwa Serikali kuhakikisha inachukua uzoefu huo na kuendeleza hapa nchini.

Akitaja idadi ya wanufaika wa huduma hiyo, Spika amesema hadi sasa kumekuwa na maombi mengi zaidi ya uwezo wa bajeti ya watoa huduma wa kambi hiyo.

“Hadi sasa, maombi yaliyopokelewa ni zaidi ya elfu moja lakini bajeti yao hawa ni watu 600,” amesema.

Hatua hiyo inaonesha umuhimu mkubwa wa Serikali kuwekeza katika huduma hiyo ili kuhudumia maelfu ya Watanzania wenye uhitaji wa viungo hivyo.

Wengi wa wagonjwa na walemavu aliozungumza nao Spika, wameeleza kuwa ulemavu huo uliwafika kwa ajali za barabarani zikiwemo za bodaboda, ndipo akatoa wito kwa jamii kuzingatia sheria za barabarani.

“Niwasihi vijana wetu na mamlaka zinazohusika kuzingatia sheria za barabarani ili kupunguza ajali hizi zinazosababisha ulemavu kwa watu,” amesema.

Kwa upande wake, Balozi wa India nchini Tanzania, Bishwadip Dey ameshukuru ushirikiano wa Serikali ya Tanzania katika kuwezesha huduma hiyo akiwakaribisha Watanzania kwenda kupata huduma hizo.

“Ninashukuru sana kwa ushirikiano mzuri tunaopata katika huduma hii, karibuni sana mpate huduma,” amesema.

Daktari bingwa wa magonjwa yasiyoambukiza, Profesa Kaushik Ramaiya kutoka taasisi ya kisukari nchini, amesema kambi hiyo imekuwa msaada mkubwa katika kuwezesha Watanzania wenye uhitaji kupata huduma ya miguu bandia bila gharama.

Amesema, ukiacha ajali ambazo ndizo zinazosababisha wengi kuvunjika viungo na kuhitaji huduma hizo, amesema wengine wamepata shida hizo kutokana na athari za ugonjwa wa kisukari.

Kwa upande wake, Mtaalamu wa vifaa tiba na vifaa saidizi kutoka MOI, Charles Mahua amesema Muhimbili imekuwa ikiwezesha Watanzania wengi kupata huduma za kibingwa kupitia ushirikiano wake na madaktari wa taasisi za nje.

Amesisitiza kupitia ushirikiano huo, sasa Watanzania wenye uhitaji wa miguu bandia wanaipata na kuhudumiwa bila gharama ambayo wangelazimika kulipia.

Mwananchi limezungumza na baadhi ya wenye ulemavu wanaopata huduma hizo, ambapo mmoja wa wanufaika hao, Isack Bitebo kutoka Mwanza, ameshukuru kupata huduma hiyo akieleza alipata ulemavu huo kutokana na ajali ya pikipiki akiwa Mwanza.

“Nashukuru sana kwa huduma hii, nilipata ajali ya pikipiki nikiwa Mwanza, nimekuwa nikitibiwa kwa muda mrefu tangu nikatwe mguu lakini niliposikia taarifa ya miguu hii bandia jana nilikuja hapa na leo nimehudumiwa vizuri,” amesema.