Tanzania, Marekani zajadili uwekezaji sekta za gesi, madini

Dar es Salaam. Tanzania na Marekani zimejadili uwekezaji katika miradi ya kuchakata gesi kuwa kimiminika (LNG) na mradi wa madini ya kimkakati wa Tembo Nickel ambao umeingia hatua za mwisho na sasa unasubiri utiwaji saini rasmi.

Mbali na miradi hiyo, pia, mradi ule wa Mahenge Graphite bado unaendelea kufanyiwa kazi.

Haya yamebainika leo Jumatatu, Desemba 8, 2025 baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kufanya mazungumzo na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Andrew Lentz katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Lengo la mazungumzo hayo ni kuendeleza maeneo muhimu ya ushirikiano wa pande mbili na kuthibitisha upya dhamira ya kujenga ushirikiano wa kisasa na wenye manufaa kwa pande zote.

Rais Samia kupitia majadiliano hayo aliuhakikishia ujumbe wa Marekani kwamba Tanzania imejizatiti kukamilisha hatua za kiutaratibu zilizobaki katika miradi hiyo

“Kama nchi isiyofungamana na upande wowote, Tanzania iko wazi, iko tayari na imejizatiti kufanya kazi na washirika wote wanaoheshimu mamlaka yetu na wanaoshirikiana katika dira yetu ya ustawi,” amesema Samia.

Zaidi ya mwenendo wa miradi hiyo ya uwekezaji, mazungumzo hayo yaligusia pia maeneo mapana ya ushirikiano yakiwamo uthabiti wa kisiasa, usalama wa kikanda, mageuzi ya kiuchumi, ukuaji wa sekta binafsi, ushirikiano wa afya na uhusiano wa watu kwa watu.

Mradi wa LNG uliozungumziwa katika majadiliano hayo una thamani ya zaidi ya  Dola 42 bilioni za Marekani (Sh102.9 trilioni) huku ukihusisha kampuni za kimataifa za nishati na unalenga kufungua hazina ya gesi iliyopo baharini.

Kukamilishwa kwake kunatarajiwa kuongeza mapato ya Taifa, kuzalisha ajira na kuiweka Tanzania kama mmoja wa wazalishaji wakuu wa gesi ya LNG duniani.

Mbali na mradi wa LNG,  mradi wa Tembo Nickel, wenye thamani ya Dola 942 milioni za Marekani (Sh2.3 trilioni), unatarajiwa kuchochea ukuaji wa viwanda, kuimarisha nafasi ya Tanzania katika mnyororo wa usambazaji wa nishati safi duniani na kuongeza mapato ya Taifa.

Uwekezaji huo wa madini ya kimkakati unaotekelezwa Ngara, unahusisha uzalishaji wa nikeli, madini muhimu katika utengenezaji wa betri za magari ya umeme.

Mradi mwingine uliojadiliwa ni wa Mahenge Graphite wenye  thamani ya Dola 300 milioni za Marekani nao unatarajiwa kuimarisha nafasi ya Tanzania kama muuzaji mkuu wa malighafi za betri duniani.

Mradi huo unatajwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya grafiti ya daraja la juu duniani, uliobuniwa kuendeleza sekta ya betri na nishati mbadala.

Akizungumza katika majadiliano hayo, Balozi Lentz, aliyefuatana na Mshauri wa Masuala ya Kisiasa na Uchumi, amesisitiza dhamira ya Washington ya kuweka upya katika misingi ya uhusiano huo na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa na kiusalama kati ya mataifa hayo mawili.

Ametumia nafasi hiyo kupongeza mipango iliyowekwa kupitia

dira 2050 na kusisitiza kwamba Serikali ya Marekani iko tayari kuunga mkono utekelezaji wa mpango huo na kufufua falsafa ya Rais ya 4R katika uongozi.

“Marekani imejizatiti kujenga ushirikiano usioegemea kwenye utegemezi wa misaada, bali ustawi wa pamoja,” amesema Balozi Lentz.

Pande hizo mbili zilikubaliana kuimarisha mawasiliano, kufanya mashauriano ya mara kwa mara na kuchukua hatua za haraka katika makubaliano yaliyosalia ni muhimu katika kufungua uwezo kamili wa uhusiano kati ya Marekani na Tanzania.

Mkutano huo unaashiria hatua muhimu katika kubadili na kuimarisha upya uhusiano wa Marekani na Tanzania.

Dhamira iliyooneshwa na Serikali zote mbili ni ishara ya mwanzo wa ushirikiano wa kisasa, wenye uwazi, unaoongozwa na sekta binafsi na unaojengwa juu ya ustawi wa pamoja, kuheshimiana na ushirikiano wa kimkakati wa muda mrefu.