Iringa. Pamoja na manufaa makubwa yanayoletwa na maendeleo ya teknolojia, changamoto mpya za ukatili wa kijinsia zimeendelea kuibuka na kuathiri wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Hayo yamebainishwa na wadau wa masuala ya jinsia wakiwemo wa kutoka Shirika la Norwegian Church Aid (NCA) kwenye mikutano ya uhamasishaji iliyofanyika katika kijiji cha Lugalo, wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa pamoja na ule wa Shule ya Sekondari The Lord’s Hill.
Msimamizi wa mradi wa kupinga ukatili wa kijinsia wa NCA, Zaria Mwenge, alieleza kuwa lengo la kukabiliana na vitendo hivyo si kuwafanya wanaume na wanawake kuwa sawa katika maumbile, bali kuhakikisha wote wanapata haki na fursa sawa katika maisha ya kila siku.
“Katika umiliki wa mali na fursa za kiuchumi, kila mmoja anapaswa kufikiwa sawasawa. Si sahihi mwanaume pekee awe anazalisha mali halafu maamuzi yote yawe mikononi mwake. Tunataka jamii ifurahie usawa katika elimu, uchumi, afya na maisha ya kijamii,” alisema.
Mwenge aliongeza kuwa hata maandiko ya dini yanakataza unyanyasaji, na kwamba jamii yenye huruma na upendo ndiyo msingi wa ustawi wa familia na maendeleo.
Kwa upande wake, Afisa uchechemuzi na mawasiliano wa NCA, Nizar Suleiman, alisema kaulimbiu ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia mwaka huu inalenga haswa ukatili wa kijinsia mtandaoni, unaoendelea kushika kasi kutokana na matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii na vifaa vya kidijitali.
“Ukatili huu hauwahusu wanawake peke yao. Hata wanaume wanakumbana na manyanyaso kutoka kwa wanawake wenzao. Kuna wanawake wababe, wanapiga waume zao au kuwadhalilisha huo nao ni ukatili,” alisema.
Akizungumza katika mkutano huo, Mchungaji Karistus Mnyagala alisema jamii ina wajibu wa kupinga aina zote za unyanyasaji. Alisema pindi matukio yanapotokea, hatua ya kwanza ni kuripoti kwa mamlaka za Serikali, na ikiwa yanahusisha madhara ya kiafya, mhanga anapaswa kufikishwa katika kituo cha afya haraka iwezekanavyo.
Mchungaji huyo alihusisha hata ongezeko la mahusiano ya pembeni maarufu kama michepuko na ukatili wa kiuchumi ndani ya familia.
“Kama mmoja ananyimwa mahitaji ya msingi, lazima atafute pa kupata msaada. Hiyo pia ni dalili ya ukatili. Tuzime ukatili na kuwasha usawa,” alisisitiza.
Kijana wa kijiji cha Lugalo, Josias Mpogole, alisema ukatili wa kijinsia mtandaoni unajumuisha vitendo vya kudhalilisha mtu kupitia maudhui yanayosambazwa bila ridhaa, matusi, picha au video zisizofaa.
“Vijana wanatumia bando kufanya mambo mabaya badala ya kujifunza. Mtu anaandika mambo yako mtandaoni au mnaachana, anasambaza picha zenu. Unateseka kisaikolojia, wengine wanajiua,” alisema.
Mwingine, Dyness Kiwonde, alishuhudia kupokea matusi mazito kupitia ujumbe mfupi kutoka kwa mwanamke aliyedai kuwa na uhusiano na mume wake.
“Aliniambia kuwa kuzaa si tatizo, hata mbwa wanazaa. Huo ni ukatili wa kidijitali kabisa,” alisema.
Katika mdahalo na wanafunzi wa Shule ya Sekondari The Lord’s Hill, washiriki walibainisha kuwa maendeleo ya teknolojia, hususan akili bandia (AI), yameongeza kasi ya utengenezaji na usambazaji wa maudhui yenye kudhalilisha.
Walisema teknolojia hiyo inatumika kutengeneza picha, video au taarifa za uongo zinazoweza kuharibu heshima ya mtu bila yeye kujua wala kushiriki.