TPLB yatembeza rungu wamo waamuzi, makamishna

KAMATI ya Usimamizi wa Ligi Kuu Bara imeshusha adhabu Mbeya City, Namungo, Coastal Union, waamuzi na maofisa wengine.

Adhabu ya Mbeya City imewakumba mastaa wawili Gabriel Mwaipola akifungiwa mechi tano sambamba na faini ya Sh5 milioni kufuatia kosa la kumpiga kwa kiwiko Rajab Mfuko wa Namungo wakati timu hizo zilipokutana.

Vitalis Mayanga amekumbana na adhabu kama hiyo akifungiwa na faini ya Sh1 milioni kwa kosa la kumpiga kwa kiwiko beki wa Simba Antony Mligo.

Timu ya Namungo imekumbana na adhabu ya faini ya Sh5 milioni kwa kosa la wachezaji kuonekana wanamwaga maji ambayo hayakujulikana ni ya nini wakati wakipasha misuli.

Nayo Coastal Union imepigwa faini ya Sh5 milioni kwa kosa la kuwakilishwa na maofisa watatu badala ya watano kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo dhidi ya Mbeya City, huku kocha wa makipa, Issa Shaban akipewa onyo kwa kosa la kuingia eneo la kuchezea wakati mchezo huo unaendelea.

Kwa upande wa waamuzi mwamuzi wa kati Gabriel Mrina kutoka Kilimanjaro ameondolewa kwenye mizunguko mitatu ya ligi kwa kosa la kushindwa kutafsiri vyema sheria kwenye mchezo wa Mbeya City dhidi ya Namungo kufuatia tukio la Mwaipola.

Naye kamishna wa mchezo wa Mbeya City na Namungo, Obedi Mollel kutoka Arusha amefungiwa kwa miezi mitatu kwa kosa la kushindwa kutoa taarifa kwa bodi kufuatia tukio hilo.

Mwamuzi wa kati Ahmada Simba kutoka Kagera ameondolewa kwenye mizunguko mitano ya ligi kwa kosa la kushindwa kutafsiri sheria, akiipa Yanga penalti ambayo mchezaji wa Fountain Gate alibainika hakuwa ameushika mpira wakati Yanga ikicheza dhidi ya Fountain Gate.

Vilevile kamishna wa mchezo huo Rehule Nyaulawa kutoka Lindi, amefungiwa kwa miezi mitatu kwa kosa la kushindwa kutoa taarifa kwa bodi kutokana na upungufu wa mwamuzi kwenye mchezo huo.

Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Desemba 5, 2025 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi yafuatayo;

Mechi Namba 058: Coastal Union FC 2-0 Mbeya City

Klabu ya Coastal Union ya mkoani Tanga imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la kuwakilishwa na maofisa watatu (3) badala ya watano (5) kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo (MCM) kuelekea mchezo tajwa hapo juu, kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:2(2.1) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Kocha wa magolikipa wa klabu ya Coastal Union, Issa Shabani amepewa Onyo Kali kwa kosa la kuingia kwenye eneo la kuchezea (pitch) bila ruhusa ya mwamuzi wakati golikipa wa timu hiyo akipatiwa matibabu.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi Namba 065: Mbeya City FC 0-1 Namungo FC

Klabu ya Namungo ya mkoani Lindi imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la wachezaji wake kuonekana wakimwaga kiwanjani vitu visivyofahamika, wakati wachezaji wa timu hiyo wakipasha moto misuli, jambo lililotafsiriwa kama kitendo kinachoashiria imani za kishirikina.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

Mchezaji Gabriel Daud Mwaipola wa klabu ya Mbeya City ya mkoani Mbeya amefungiwa michezo mitano (5) na kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kumpiga ngumi mchezaji Rajabu Abdallah Mfuko wa klabu ya Namungo wakati wa mchezo tajwa hapo juu.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:21 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.

Mwamuzi wa kati wa mchezo tajwa hapo juu, Gilbert Mrina kutoka Kilimanjaro ameondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa mizunguko mitatu (3) kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu na kushindwa kuchukua hatua kwa kitendo cha ukiukwaji wa sheria za mpira kilichofanywa na mchezaji Gabriel Daud Mwaipola.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42:1(1.6) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.

Kamishna wa mchezo tajwa hapo juu, Obed Mollel kutoka Arusha amefungiwa kwa kipindi cha miezi mitatu (3) kwa kosa la kushindwa kutoa taarifa kwa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania kuhusiana na kitendo cha ukiukwaji wa sheria za mpira kilichofanywa na mchezaji Gabriel Daud Mwaipola, licha ya mwamuzi kutotoa adhabu yoyote kwa mchezaji huyo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 43:4(4.7 & 4.8) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Kamishna.

Mechi Namba 093: Simba SC 3-0 Mbeya City FC

Mchezaji wa klabu ya Mbeya City, Vitalis Mayanga amefungiwa michezo mitano (5) na kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kumpiga kiwiko kwa makusudi mchezaji wa klabu ya Simba, Anthony Mligo, tukio ambalo lingeweza kuhatarisha usalama wa mchezaji huyo.

Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:21 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.

Mechi Namba 095: Young Africans SC 2-0 Fountain Gate FC

Mwamuzi wa kati wa mchezo tajwa hapo juu, Ahmada Simba kutoka Kagera ameondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa mizunguko mitano (5) kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu ambapo mwamuzi huyo alitoa adhabu ya penati kwa klabu ya Fountain Gate katika tukio ambalo mlinzi wa timu hiyo hakuwa ameushika mpira huo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42:1(1.8) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.

Kamishna wa mchezo tajwa hapo juu, Rehule Nyaulawa kutoka Lindi amefungiwa kwa kipindi cha miezi mitatu (3) kwa kosa la kushindwa kutoa taarifa kwa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania kuhusiana na mapungufu ya mwamuzi wa mchezo huo katika kutafsiri sheria za mpira wa miguu kama yalivyoainishwa hapo juu.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 43:4(4.7 & 4.8) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Kamishna.

Mechi Namba 031: Mbuni FC 1-2 Songea United FC

Daktari wa klabu ya Songea United, Mboto Shabani ametozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) na kufungiwa michezo mitatu (3) kwa kosa la kuonekana akimwaga kimiminika kisichofahamika kiwanjani na kuwamwagia kimiminika hicho wachezaji wa timu hiyo wakati wa mapumziko ya mchezo tajwa hapo juu, jambo lililotafsiriwa kama kitendo kinachoashiria imani za kishirikina.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

Mechi Namba 033: KenGold FC 3-1 Hausung FC

Klabu ya KenGold ya mkoani Mbeya imetozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kushindwa kukamilisha kwa wakati maandalizi ya mchezo tajwa hapo juu kwa mujibu wa kanuni ya 17:48 ya Championship kuhusu Taratibu za mchezo, jambo lililosababisha mchezo huo kuchelewa kuanza.

Gari ya kubebea wagonjwa iliyoandaliwa na klabu hiyo ilichelewa kufika uwanjani ambapo iliwasili saa 10:09 alasiri, ikiwa ni dakika tisa (9) baada ya muda wa kuanza kwa mchezo huo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi Namba 036: Polisi Tanzania FC 1-1 Bigman Security FC

Klabu ya Polisi Tanzania imetozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la mmoja

wa walinzi wake wa uwanjani, Innocent Timanya kuonesha utovu wa nidhamu kwa kumshambulia mtunza vifaa wa klabu ya Bigman Security, Uhuru Mwambungu. Kosa hili limeainishwa kwenye Kanuni ya 17:7 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo na adhabu yake ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Championship kuhusu Taratibu za

Mechi Namba 044: African Sports 0-1 Geita Gold FC

Klabu ya African Sports ya mkoani Tanga imetozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kuwakilishwa na maofisa wanne (4) badala ya watano (5) kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo (MCM) kuelekea mchezo tajwa hapo juu kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:2(2.1) ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.

Klabu ya African Sports imepewa Onyo Kali kwa kosa la kuchelewa kuwasili uwanjani kuelekea mchezo tajwa hapo juu.

African Sports iliwasili uwanjani saa 8:37 mchana badala ya saa 8:30 mchana kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:15 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi Namba 052: Mbuni FC 1-0 Gunners FC

Klabu ya Mbuni ya mkoani Arusha imetozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la mashabiki wake kuifanyia vurugu timu ya Gunners ilipokuwa ikifanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha Novemba 26, 2025 kwa mujibu wa Kanuni ya 17:45 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi Namba 056: Polisi Tanzania FC 1-1 Transit Camp FC

Klabu ya Transit Camp imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kukataa kutumia chumba maalum cha kuvalia kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:20 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.

Klabu ya Transit Camp imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la mashabiki wake wakiongozwa na mkuu wa msafara kuanzisha vurugu. Mkuu huyo wa msafara alikwenda kusimama nyuma ya lango, ambapo walinzi wa uwanjani (stewards) walipojaribu kumuondoa alikataa na ndipo vurugu hizo zilipoanza.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 47:1 ya Championship kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

Mechi Namba 059: Stand United FC 2-1 Mbuni FC

Klabu ya Stand United ya mkoani Shinyanga imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la kuwaondoa kiwanjani watoto waokota mipira (ball kids) mara baada ya timu hiyo kupata bao la pili na la ushindi katika mchezo tajwa hapo juu.

Kitendo hicho ambacho kimekuwa kikifanywa mara kwa mara na klabu ya Stand United, na ambacho kiliathiri mwendelezo mzuri wa mchezo huo, ni kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:7 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mtunza vifaa wa klabu ya Mbuni, James Majeka ametozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kuiba mpira mmoja miongoni mwa mipira inayotumika kwenye kituo cha Shinyanga kwa ajili ya michezo ya Ligi.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 45:2(2.5) ya Championship kuhusu Udhibiti kwa Makocha na Maofisa Wengine wa Mchezo.

Mechi Namba 3A: Moro Kids vs Green Warriors

Klabu za Moro Kids na Green Warriors zimetozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kila moja kwa kosa la kuchelewa kuwasili uwanjani kuelekea mchezo tajwa hapo juu.

Green Warriors iliwasili saa 8:49 mchana huku Moro Kids ikiwasili 9:00 alasiri badala ya saa 8:30 mchana kama inavyoelekezwa kwenye Kanuni ya 17:15 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.

Klabu ya Moro Kids imepewa ushindi wa mabao matatu (3) na pointi tatu (3) katika mchezo tajwa hapo juu, huku Green Warriors ikipoteza mchezo huo kwa mujibu wa Kanuni ya 17:31 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.

Green Warriors ilisababisha mchezo huo kutofanyika baada ya kubainika haikuwa na mchezaji yeyote mwenye leseni hivyo kukosa kabisa wachezaji wenye sifa za kucheza mchezo huo wa Ligi.

Mechi Namba 4B: COPCO FC vs Biashara United FC

Klabu ya Biashara United imepoteza mchezo tajwa hapo juu na timu ya COPCO FC imepewa ushindi wa mabao matatu (3) na alama tatu (3) kwa kosa la Biashara United kushindwa kufika kwenye uwanja wa Amani, Njombe bila ya sababu za msingi na zinazokubalika hivyo kusababisha mchezo huo kushindwa kufanyika.

Sambamba na adhabu hiyo, Biashara United imetozwa faini ya Sh. 2,000,000 (milioni mbili), kutakiwa kulipa fidia ya maandalizi ya mchezo huo pamoja na kupokwa alama tatu (3) katika msimamo wa First League.

Pia Mwenyekiti wa klabu ya Biashara United, Arnold Lyimo amefungiwa kwa kipindi cha mwaka mmoja (1) kwa kosa la klabu yake kushindwa kufika uwanjani.

Adhabu hizi ni kwa mujibu wa Kanuni ya 31:1(1.1, 1.2, 1.3 & 1.4) ya First League kuhusu Kutofika Uwanjani.