Nairobi. Kikao cha saba cha Baraza la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEA-7) kimeanza jijini Nairobi nchini Kenya katika wakati ambao viongozi wa mazingira duniani wanautaja kuwa na uamuzi kwa mustakabali wa dunia.
Tukio hilo linafanyika wakati changamoto za kimazingira zikiongezeka na mfumo wa utawala wa kimataifa ukitakiwa kutafuta suluhu kutokana na ongezeko la athari za mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mifumo ya ikolojia, uchafuzi wa mazingira, pamoja na kuongezeka kwa migogoro ya kijiografia.
Viongozi wa kimataifa, watunga sera, wanasayansi na wadau wengine wanatarajiwa kuleta suluhu katika mkutano huu utakaofanyika kuanzia leo Jumatatu Desemba 8 hadi 12, 2025.
Akitaja mambo muhimu ya yatakayojadiliwa mwakilishi kutoka Tanzania na Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika (AGN), Richard Muyungi amesema zipo ajenda 15 na zote zitakuwa na umuhimu.
“Miongoni mwao ambazo ni muhimu ni pamoja na kulinda kwa uthabiti mifumo ikolojia ya bahari ya kirefu, na matumbawe, mikakati ya kuthibiti mioto, matumizi ya Akili Unde (IA), kwenye kulinda mazingira na kukuza suluhu endelevu kupitia michezo,” amesema Dk Muyungi ambae pia ni mshauri wa Rais wa Tanzania kuhusu masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), Inger Andersen, ametaja migogoro mikubwa ya kimazingira ni mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa maliasili, ardhi na viumbe hai, unaojumuisha kuenea kwa jangwa na uchafuzi wa mazingira.
Akiielezea UNEA amesema kuwa, “ni chombo chenye ushawishi mkubwa zaidi duniani katika kufanya uamuzi wa kimazingira,” Andersen alisisitiza jukumu la baraza hilo katika kuongoza mwelekeo wa dunia kuhusu hatua za mazingira.
Hata hivyo, amebainisha wakati wa sasa unahitaji zaidi matendo kuliko ahadi.
“Mwaka huu, baraza hili lazima litumie historia yake ya umoja ili kwa mara nyingine kutoa suluhu endelevu kwa dunia,” alisema, huku akiongeza kuwa changamoto za kimazingira zinakua kwa kasi akitoa mfano ongezeko la joto kuvuka wastani wa 1.5°C ndani ya muongo ujao.
Dharura ya UNEA-7 inaongezewa nguvu na ushahidi wa uharibifu wa mazingira katika nyanja mbalimbali.”
“Mifumo ya ikolojia inatoweka na ardhi inaharibika. Dhoruba za vumbi zinaongezeka. Sumu zinaendelea kuchafua hewa yetu, maji na ardhi,” amesema Andersen.
Kuhusu migogoro na vita amesema, “dunia ipo katika mawimbi ya misukosuko ya kisiasa ya kijiografia, hali inayoongeza ugumu kwenye makubaliano ya kimataifa.”
Katika muktadha huu, UNEA-7 haionekani tu kama jukwaa la majadiliano, bali pia kama kichocheo cha suluhu zinazotekelezeka. Kutolewa kwa Tathmini ya Mazingira Duniani ya UNEP (GEO-7), kwa mujibu wa Andersen, kunaainisha njia za mabadiliko zitakazochangia ongezeko la pato la taifa duniani, vifo vichache, njaa kidogo na umaskini mdogo, yote kupitia hatua kuhusu tabianchi, asili na uchafuzi wa mazingira.
Naye, Rais wa UNEA-7, Abdullah Bin Ali Al-Amri, amesisitiza mkutano huo unawakilisha hatua muhimu katika kufanya uamuzi wa pamoja.
Ametaja nguzo tatu muhimu kwa mafanikioni “… tunahitaji malengo makubwa kwa sababu hatua ndogo hazitoshi kukabiliana na kasi ya mabadiliko. Pili, tunahitaji mshikamano kwa sababu ustahimilivu hujengwa kwa pamoja au hautakuwepo kabisa. Tatu, tunahitaji kuongozwa na sayansi.”
Kwa mujibu wa Al- Amri, kiini cha vikao hivyo ni mjadala kuhusu Mkakati wa Muda wa Kati wa UNEP (2026–2029) na Mpango wa Kazi na Bajeti (2026–2027). Nyenzo hizi zitaamua namna UNEP itakavyosaidia nchi wanachama katika utawala wa mazingira, utekelezaji wa sera na ujenzi wa uwezo.
Al-Amri amesisitiza mafanikio yatapatikana kupitia,“maazimio yanayotekelezeka, yanayoongozwa na sayansi, na yenye mifumo ya ufuatiliaji,” sambamba na mkakati wa UNEP wenye rasilimali za kutosha na mpango kazi unaowezesha utekelezaji.
Serikali ya Kenya, kama mwenyeji, imesisitiza, usawa na ustahimilivu.
Katibu wa Baraza la Mawaziri wa Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Misitu, Dk Deborah Barasa, amesema, “Wakati wa hatua ndogo na za tahadhari umepita, tunachohitaji sasa ni hatua za ujasiri, zilizounganishwa na shirikishi.”
Amebainisha,“dunia yenye ustahimilivu ni zaidi ya kulinda mifumo ya ikolojia; ikimaanisha kutumia rasilimali zetu kwa busara, kujenga jamii zenye haki na ushirikishwaji, kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi unaheshimu mipaka ya sayari yetu, na kudumisha ubunifu ili kutabiri na kuzuia madhara kabla hayajatokea.”
Kauli zake zinaakisi uhusiano wa karibu kati ya changamoto za kimazingira, ambazo haziwezi kushughulikiwa kwa njia ya kutengana.
Ametaja matokeo yanayotarajiwa ya UNEA-7, yakiwemo kuidhinishwa kwa mkakati wa muda wa kati, azimio madhubuti la mawaziri, na uamuzi wa wazi kuhusu tarehe ya UNEA-8.
Ameonyesha matumaini kuwa maazimio yatakayopitishwa yataweza kushughulikia kwa ufanisi changamoto kubwa za kimazingira duniani.
Dk Barasa amesisitiza haja ya kuhamasisha mfuko maalumu wa fedha utakaoleta suluhu zinazolinda mazingira na uchumi rejelezi (circular economy), kuhimiza ubunifu, na kuunganisha hatua za ndani na malengo ya kimataifa.
Mbali na majadiliano jukwaa hili linalofanyika kila baada ya miaka minne hukutanisha wadau mbalimbali. Takribani washiriki 6,000 waliosajiliwa kutoka zaidi ya nchi wanachama 170, wakiwemo mawaziri 79 na manaibu mawaziri 35, wanashiriki katika mkutano huu.
Pamoja na miji, vikundi vya vijana, jamii za asili, wanasayansi, sekta ya viwanda, asasi za kijamii na kiraia, makundi ya wanawake na wafanyakazi, baraza hilo linafanya kazi kama jukwaa la kisiasa na kijamii kwa pamoja. Ushiriki huu wa pande nyingi unaimarisha nafasi ya UNEA kama jukwaa la kimataifa la mazingira.