Dar es Salaam. Wakati Serikali za mitaa zikisisitiza ushiriki wa wananchi katika kulinda makazi yao, baadhi ya wananchi wanalalamikia mfumo wa ulinzi shirikishi, wakidai umepoteza mwelekeo.
Wamesema mpango wa ulinzi shirikishi umegeuka kutoka kuwa msingi wa usalama wa raia na mali zao na kusababisha mpasuko katika jamii.
Miongoni mwa mambo yanayolalamikiwa ni kutozwa fedha za ulinzi shirikishi bila kuona walinzi wenyewe, wapo wanaokwenda mbali zaidi na kudai pamoja na kulipa, wanaendelea kuibiwa bila msaada.
Hata hivyo, kwenye vikao vya Serikali ya mtaa na wananchi, hujadiliwa kuhusu ulinzi shirikishi na gharama ambazo kila kaya inaweza kumudu kutokana na mazingira ya eneo husika na kwa familia ambazo hazilipi. Kiwango cha malipo ya ulinzi kinaanzia Sh1,000 hadi Sh10,000 kwa mwezi.
“Natoa Sh3,000 kila mwezi, lakini sijawahi kuwaona hao walinzi hata ninaporudi usiku mnene. Sijui wanavaa nini au kama wanafanya doria kweli, na mwisho wanakuja kutukemea tu tukichelewa kulipa,” amesema Maimuna Salehe, mkazi wa Tabata.
Amesema siku moja walifika kutaka pesa na hakuwa nayo kwa wakati huo, lakini watu hao walikosa busara na kuanza kutoa maneno machafu, jambo lililosababisha ugomvi baina yake na mumewe.
Hata hivyo, migogoro hiyo imekuwa chanzo cha wenye nyumba katika maeneo tofauti kuwaondoa wapangaji wanaokataa kuchangia pesa za ulinzi.
Agnes Chaula, aliyekuwa mpangaji eneo la Mabibo, amesema hakutoa pesa ya ulinzi miezi miwili kwa kuwa alikuwa anapishana na wachukua pesa, lakini mwenye nyumba aliingilia kati na kumweleza kuwa kodi yake ikiisha aondoke.
“Sikuwa na pesa na nilikuwa nadaiwa pesa ya ulinzi wa miezi miwili. Siku mbili baadaye nikapewa taarifa kuwa niondoke kwa sababu nilitaka kuhatarisha usalama wa mtaa,” amesema Agnes.
Edward Mwita, mkazi wa Pugu, amesema walikaa kikao na kukubaliana kuchangia pesa za ulinzi au watu kutoka kulinda, lakini ilileta mgogoro kwa sababu waliojitolea kulinda walichoka baada ya siku tatu.
“Katika kikao tulikubaliana kuwepo ulinzi ili kupunguza matukio ya wizi na kati ya watu waliokuwa wamejitokeza tulimkataa mtu mmoja kutokana na tabia zake zinajulikana, hivyo hakufaa. Hata wale wengine waliounga mkono kujumuika na kutoa pesa waliishia njiani na kuwaacha tuliowachagua,” amesema Mwita.
Baadhi ya wananchi hujificha au kutoa maagizo ya kutokuwapo nyumbani ili kuepuka kulipa mchango wa ulinzi.
“Hata kusalimiana sasa imekuwa shida. Mtu akiona mjumbe anakuja, anaingia ndani kujificha. Wengine wanasema hawalipi kwa sababu hawana imani na ulinzi huo,” amesema Salum Masangu, mjumbe wa shina mtaa wa Kwa Simba.
Pia, majirani huchongeana wakidai kuwa mfumo huo umechangia watoto wao kukamatwa au kushirikiana na wezi au kujihusisha na wizi wa moja kwa moja.
“Unaweza ukasikia mzazi akimshtumu jirani kuwa mtoto wake ni mwizi kwa sababu hakutoa pesa ya mwezi. Wakati mwingine watoto wetu wanakamatwa tu bila ushahidi,” amesema Rehema Beatus, mkazi wa Vingunguti Darajani.
Mbali na hilo, jambo lingine ni la walinzi kuwakamata watuhumiwa wa wizi na kuzunguka nao mtaani usiku kucha bila kuwapeleka polisi, kwa madai kuwa wanawaonesha wanaoshirikiana nao.
Katika mtaa wa Vingunguti, kijana anayedaiwa kuwa mhalifu alizungushwa hadi alfajiri kwa madai walimkuta akitaka kuiba, hivyo walihitaji awaoneshe anaoshirikiana nao huku akisaidia kulinda.
“Wakati natoka kwenda kwenye shughuli zangu za kila siku nilikutana na ulinzi saa 11 alfajiri na niliwakuta wamemshikiria kijana huku wakimpiga makofi. Nilipouliza waliniambia ni mwizi, walimkuta anataka kukata dirisha la watu na walizunguka naye ili aoneshe wenzake,”amesema Nassoro Sharif, mkazi wa Kwa Simba.
Malipo chanzo cha migogoro
Katika mitaa mingi, walinzi wamesema hawalipwi kwa muda, mtu analimbikiza deni miezi miwili au mitatu mfululizo.
“Hii kazi ya ulinzi tunajitolea kutokana na makubaliano ya kikao cha Serikali ya mtaa na wananchi. Sioni sababu ya watu kukaidi kutoa pesa ya ulinzi, jambo linaosababisha kupelekena sehemu ambayo tunajengeana uhasama,” amesema Joshua Anthony, mlinzi wa Tabata.
Kutolipwa kwa walinzi kunasababisha doria hafifu, kupungua kwa hamasa, na mara nyingine walinzi kuacha kazi ghafla bila taarifa, jambo linaloacha maeneo bila ulinzi.
Kuhusu kushirikiana na wezi, amesema inawezekana jambo hilo linafanyika kwa sababu wanagawa sehemu za kulinda, na hawaongozani, pia wamekuwa sehemu ya kusaidia polisi kujua vijiwe vya wahalifu.
Kauli za Serikali za mtaa
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Majengo-Vingunguti, Israel Mwantimwa, amesema Serikali imekuwa ikianza kwa kutoa elimu kwa wakazi kabla ya kuchukua hatua zozote kuhusu ulinzi shirikishi, akisisitiza changamoto nyingi hutokana na wananchi kutotambua kuwa usalama wa mtaa unategemea ushiriki wao.
Amesema baadhi ya wakazi hulalamika kuibiwa licha ya kuchangia ulinzi, lakini mara nyingi uchunguzi unaonesha uzembe kama madirisha kutofungwa au kuacha mazingira mepesi kwa wahalifu.
Kwa upande wa matukio hayo, Mwantimwa amesema ulinzi shirikishi umechangia kupunguza vibaka, ingawa uhalifu hauwezi kuisha kutokana na mbinu mpya za wahalifu.
“Serikali ya mtaa haina uwezo wa kulipa fidia kwa watu walioibiwa, kwa kuwa mfumo huo si ajira ya serikali, bali unategemea michango ya jamii,” amesema.
Kuhusu wahalifu wanaokamatwa, mwenyekiti amesema hawatoi adhabu za mitaani, bali huwakabidhi polisi.
“Tunatoa elimu kwanza… ulinzi shirikishi hauwezi kulinda kila nyumba moja kwa moja, lakini tunashirikiana kuhakikisha mtaa unakuwa salama,” amesema.
Mwenyekiti wa mtaa wa Darajani, Tabata Kimanga, Marius Alphonce, amesema bado zipo changamoto zinazojitokeza, hususan katika ulipaji wa michango ya ulinzi, uelewa mdogo wa wananchi, na ushirikiano baina ya walinzi na wakazi wa mtaa.
Amesema changamoto kubwa ni wananchi kutolipa ada ya ulinzi shirikishi, wapo wanaosubiri kusukumwa kila mwezi, na wengine wanakaidi licha ya faida wanazopata kupitia ulinzi huo.
“Kuna wengine ukimuita analipa vizuri tu, ila ukimfuata bila kumuita anakua msumbufu,” amesema.
Naye, Mwenyekiti wa Mtaa wa Feri na Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Serikali za mitaa Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Mwingamno, amesema wananchi mara nyingi hawafahamu namna walinzi shirikishi wanavyofanya kazi, jambo linalosababisha lawama zisizo za haki.
“Mlinzi anapolinda, anakuwa sehemu ambayo haiwezi kuonwa kirahisi. Anaweza kupanda juu ya mti, kuficha mwilini, au kutumia mwanga wa taa kumchunguza mhalifu. Wewe kama mkazi, unaingia nyumbani kwako ukidhani hakuna mtu, kumbe mlinzi yupo kazini anakuchunga,” anasema Mwingamno.
Akiizungumzia hoja ya wananchi wanaolalamika kuibiwa licha ya kuwa na ulinzi shirikishi, Mwingamno amesema baadhi ya matukio hutokana na uzembe wa wakazi wenyewe.
“Mtu analalamika simu kuibiwa, lakini ukisikia mazingira utakuta ameacha dirisha wazi, taa zikiwa zimewashwa, simu juu ya meza, halafu yeye akaingia bafuni. Hapo hujaibiwa bali umetoa mwaliko. Hata siyo mwizi wa kitaalamu, mtu yeyote angeichukua.”
Hata hivyo, alikiri kuwa pamoja na uwepo wa ulinzi shirikishi, uhalifu hauwezi kuisha.
“Tangu dunia ianze, uhalifu umekuwepo. Kazi ya ulinzi shirikishi ni kupunguza kiwango cha uhalifu, si kukimaliza. Ukiondoa ulinzi shirikishi, uhalifu ungeongezeka maradufu.”
Akizungumza na Mwananchi Septemba 27, 2025, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, alisema ili kudhibiti uhalifu mitaani, wananchi wanatakiwa kuwa na kikundi cha ulinzi shirikishi kitakchowasaidia.
