Wananchi walalamikia uhaba wa maji, Aweso aagiza suluhisho la haraka

Pwani, Dar es Salaam. Wakazi wa baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam wamemueleza Waziri wa Maji, Jumaa Aweso adha ya kukosa huduma ya maji wanayoipitia katika siku za karibuni, ambapo  ametoa maagizo kwa mameneja.

Akiwa katika ziara ya kukagua huduma ya maji maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam pamoja na tenki la Kisanga na mkondo wa Mto Ruvu, leo Desemba 8,2025 amekutana na wananchi waliokuwa wakisaka maji mtaani.

Wakazi hao wameeleza wanavyopata taabu kufanya shughuli za nyumbani ikiwemo kufua, kuoga huku wakiomba jitihada zaidi huduma hiyo irejee kikamilifu, ambapo wamefafanua kuwa wamekosa maji kwa siku tatu huku baadhi yao wakienda kutafuta kwa waliohifadhi kwenye matenki.

Hata hivyo, ziara hiyo imefanyika kufuatia upungufu wa maji unaoendelea kushuhudiwa kutokana na kupungua kwa kiwango cha maji katika Mto Ruvu, hali inayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, kuongezeka kwa joto na kuchelewa kwa mvua.

Maria Samson, mkazi wa Tegeta Wazo amesema amekosa maji kwa siku tatu na amechoka kuzunguka kusaka huduma hiyo muhimu.

“Tunaomba Serikali ituletee maji jamani tutakufa. Yaani huwezi kuamini sijafua jana, juzi nabangaiza maji kwa majirani,” amesema.

Mariam Ismail amesema hakuwahi kumiliki tenki la kuhifadhia maji ila kutokana na kadhia aliyopitia siku tatu hizi anakwenda kutafuta chombo hicho ili awe tayari hata ikitokea maji yakikata tena.

Michael Joel ameomba Serikali kuweka mifumo itakayohifadhi maji hata itakapotokea shida ikiwemo kuvuna yale ya mvua kwa wingi.

Hata hivyo, wakati wa ziara hiyo Waziri Aweso akiwa na uongozi wa mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), Katibu Mkuu wake, Mwajuma Waziri, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando ameshuhudia kufunguliwa kwa tenki la Kisanga linalohifadhi na kusambaza maji lita milioni sita.

Watakaopata huduma ni wakazi wa Kunduchi, baadhi ya maeneo Kawe, Mbezi Beach, Kwa Zena.

Baada ya kufunguliwa kwa tenki hilo, Mwananchi imeshuhudia maji yakianza kutoka baadhi ya maeneo ambapo Waziri amepita nyumba kwa nyumba kushuhudia hali hiyo.

Mjumbe wa serikali mtaa wa Tegeta, Happy Daniel amesema ameteseka yeye na familia yake kwa siku hizo tatu alizokosa maji huku akishukuru kwa sasa yameanza kutoka.

“Nilikuwa nawasumbua viongozi wa wizara kuhusu kukosekana na maji na wao wameonesha ushirikiano hadi sasa maji yanatoka,” amesema.

Kwa upande wake Amir Ramadhan, mkazi wa Wazo Hill Tegeta amesema changamoto ya maji ipo na anaomba ishughulikiwe huku akitoa rai kwa wananchi wenzio kuwa na vyombo vikubwa vya kuhifadhia maji.

 Waziri Aweso amewataka mameneja wa Dawasa katika maeneo yao kutokaa ofisini bali waende mitaani kutatua kero kwa wananchi.

“Wakitoka ofisini watasaidia wananchi, unaweza kukuta mtu hapati maji kwa sababu tu kuna sehemu imeziba kwa hiyo wakifanya hiyo kazi mambo yatakuwa sawa,” amesema.

Waziri huyo amefika hadi kijiji cha Kitomondo Mlandizi mkoani Pwani kujionea hali halisi ya Mto Ruvu ambapo ameshuhudia shughuli ya kurejesha mto huo katika njia yake ya asili baada ya kuchepuka.

Mto ulihama na kuacha njia yake ya asili ambapo shughuli ya kurudisha inaendelea huku ikitarajiwa kukamilika hapo kesho.

Waziri Aweso amesema wanahakikisha mto unarudi kwenye njia yake ya asili ambapo wizara kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama vinahakikisha vyanzo vinalindwa.

“Tunahakikisha mto unarudi kwenye njia yake ya asili na naelekeza bodi ya Wami-Ruvu kufanya kazi kwa njia shirikishi na jamii kuhakikisha maji yanarudi kwenye njia yake si hapa Kitomondo bali na maeneo mengine.

“Bodi ya Wami-Ruvu pamoja na menejimenti yake vyombo vya ulinzi na usalama jamii na wadau wote wanapaswa wahakikishe kwa pamoja vyanzo vyote vya maji vinalindwa,” amesema Aweso.

Amesema kwa sasa mtiririko wa maji unaridhisha ya kwamba uzalishaji utaongezeka na tunarudi katika hali ya kawaida.

“Wenzetu wa mamlaka ya hali ya hewa wametuambia mvua zitaanza kunyesha juma la pili la Desemba hii. Hii ni habari njema kwani jana zimeanza na dalili ni nzuri,” amesema.

“Tunataka haya yaliyopo yanagawiwa kwa usawa bila upendeleo lakini niseme wananchi wawe na tabia ya kuhifadhi maji. Tumepita tayari maeneo mengine watu washaanza kupata maji.

Amesema watakuja na kampeni ya kuhamasisha utunzaji maji na hata wale wanaojenga waweke mifumo ya kuvuna na kuhifadhi maji, huku wakishirikiana na sekta nyingine.

Jana Jumapili, Desemba 7, 2025 Waziri Aweso alipiga marufuku matumizi ya maji yanayotoka Mto Ruvu kwa shughuli nyingine zisizo za kibinadamu, akisisitiza kwa sasa maji hayo yatatumika kwa matumizi ya binadamu pekee hadi hali ya upatikanaji itakapokuwa sawa baada ya mvua kunyesha.