WPL mzigo umerudi, mechi tatu kupigwa

MZIGO wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) umerudi tena kwa mechi tatu kutarajiwa kuchezwa kesho Jumatatu Desemba 8, 2025, ikiwamo ile ya watetezi wa taji JKT Queens itakayokuwa inakula kiporo dhidi ya Bunda Queens.

Mechi nyingine za kesho katika ligi hiyo ni Alliance Girls dhidi ya Fountain Gate Princess, kikiwa pia ni kiporo, huku Tausi ikiikaribisha Mashujaa Queens.

Hadi sasa Simba Queens iko kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi sita baada ya kucheza mechi mbili dhidi ya Bilo Queens ikishinda kwa mabao 4-0, kisha ikaichapa Bunda Queens 3-0.

Mabingwa watetezi JKT Queens wataanza karata yao ya kwanza dhidi ya Bunda Queens mechi itakakayopigwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Tausi ikiwa mara ya kwanza kucheza WPL itaikaribisha Mashujaa ambayo huu ni msimu wa tatu na Alliance itakuwa nyumbani Nyamagana jijini Mwanza.

WP 01

JKT Queens iliyotoka kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake na kutolewa makundi, inapewa nafasi kubwa kuianza ligi kwa kishindo licha ya kwa kwamba Bunda nayo sio ya kubezwa.

Hii itakuwa mechi ya tano kwa Bunda kukutana na mabingwa hao wa CECAFA tangu ilipopanda daraja mwaka 2023, JKT Queens ikishinda mechi tatu na sare moja.

Msimu huo JKT ilishinda mabao 4-0 ugenini kisha 2-1 nyumbani, msimu uliopita maafande hao wakapata sare ya 1-1 ugenini kisha wakashinda mabao 3-0 nyumbani.

WP 02

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha wa JKT Queens, Abdallah Kessy amesema wamejipanga vizuri na anaamini maelekezo aliyowapatia wachezaji watakwenda kufanyia kazi ndani ya dakika 90.

“Ni mechi ya ufunguzi kwetu hivyo ni lazima tupambane kwa jasho na damu kuhakikisha tunapata ushindi kwani ni mechi yetu ya kwanza licha ya ugumu wa timu kama Bunda inayocheza mpira mzuri,” amesema Kessy.