Unguja. Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Suleiman Masoud Makame, amesema hajaridhishwa na mpangilio wa miundombinu, matumizi ya ardhi na namna shughuli zinavyoendeshwa katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na Mifugo (Zarili).
Amesema mazingira ya sasa ya taasisi hiyo hayako katika hali inayoweza kuonesha ufanisi, ubunifu au uendelevu unaotarajiwa kutoka kituo cha utafiti chenye wajibu mkubwa kwa sekta ya kilimo na mifugo.
Waziri Makame amebainisha kuwa mwonekano wa Zarili hauakisi malengo ya msingi ya kuongoza, kutoa mafunzo na kusimamia tafiti za kuongeza uzalishaji kwa wakulima na wafugaji.
Ameongeza kuwa taasisi hiyo inapaswa kuwa mfano wa kitaalamu na kitovu cha maarifa, hivyo amesisitiza haja ya maboresho ya haraka ili kuiweka katika viwango vinavyolingana na matarajio ya serikali na wananchi.
Makame ametoa kauli hiyo leo, Desemba 8, 2025, wakati akikagua idara mbalimbali za wizara hiyo kisiwani Pemba, akiwa katika tathmini ya utekelezaji wa shughuli za kilimo, mifugo na utafiti zinazotekelezwa katika vituo vilivyo chini ya wizara yake.
Amesema mpangilio wa mazingira ya Zarili hauoneshi taswira ya kituo cha kitaalamu chenye uwezo wa kutoa mafunzo kwa wakulima na wafugaji, wala hauakisi dhana ya uzalishaji bora inayopaswa kuwa mfano kwa jamii.
Makame ameongeza kuwa taasisi hiyo inapaswa kuwa kitovu cha uzalishaji na chanzo cha maarifa kwa wakulima na wafugaji, sambamba na kufanya tafiti zenye mchango wa kuongeza tija na uzalishaji kwa wananchi wa kisiwa hicho.
“Taasisi hii inatakiwa kubadili mfumo wa utendaji kazi kwa kuandaa mpango madhubuti wa matumizi ya eneo utakaotafsiri lengo ya wizara katika nyanja za uzalishaji, utafiti na mafunzo hivyo sijaridhishwa na hali ya eneo hili lilivyo,” amesema.
Aidha, ameitaka menejimenti ya Zarili kuandaa utaratibu madhubuti wa utoaji elimu utakaowafikia wakulima na wafugaji, akisisitiza kuwa matokeo ya utafiti hayawezi kubaki kwenye vitabu na maabara pekee.
Katika hatua nyingine, ameagiza kuharakishwa kwa ujenzi wa kisima ndani ya eneo la taasisi hiyo, kufuatia taarifa za kuwepo changamoto zinazoathiri upatikanaji wa maji kwa shughuli za utafiti.
Naye Naibu Waziri wa wizara hiyo, Dk Salum Soud Hamed, amewaelekeza wataalamu wa wizara na taasisi kuchukua hatua za haraka kutatua changamoto hizo ndani ya wiki moja, akibainisha kuwa maji ni rasilimali ya msingi katika shughuli zote za utafiti, na kukosekana kwake kunadhoofisha matokeo ya tafiti pamoja na utoaji wa huduma.
“Hatutavumilia ucheleweshaji wowote katika utekelezaji wa maelekezo hayo, kwani dhima ya Serikali ni kuhakikisha taasisi zote zinazohusika na utafiti zinakuwa na mazingira bora ya kiutendaji,” amesema.