Hali ilivyo mitaani leo Siku ya Uhuru

Dar/mkoani. Watanzania mwaka huu wamesherehekea maadhimisho ya miaka 64 ya Uhuru wa Tanganyika wakiwa majumbani pamoja na familia zao, hali ambayo ni tofauti na desturi ya wengi kutumia siku hiyo kupumzika kwenye maeneo ya burudani au kushiriki matukio ya hadhara.

Mabadiliko hayo yalichochewa na taarifa za kuwepo maandamano yasiyo na ukomo ikiwa ni mwendelezo wa maandamano ya Oktoba 29, wakati wa uchaguzi yaliyosababisha vurugu ikiwano watu kupoteza maisha, wengine kujeruhiwa na maliza za umma na zile za binafsi kuharibiwa.

Waandaaji wa maandamano ambao hawafahamiki waliitisha tena maandamano yasiyo na ukomo ya Desemba 9 siku ambayo Tanzania inaadhimisha miaka 64 ya Uhuru.

Kufuatia hali hiyo Serikali Ilitoa agizo la kuwataka wananchi wote wasio na dharura kusalia nyumbani ili kuhakikisha usalama wa umma.

Pia, salamu za heri kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan, zilizowasilishwa na Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba, ziliwahimiza Watanzania kutumia siku ya Uhuru kwa kukaa nyumbani na familia zao kwa wale ambao hawana sababu za lazima kutoka nje.

Aidha, tangazo la Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, kwamba watu wanaolazimika kutoka nje wabebe vitambulisho na wawe tayari kuulizwa maswali ya uthibitisho, liliongeza umakini na kuwafanya wengi wachague kubaki majumbani ili kuepuka usumbufu.

Pia, uwepo wa askari polisi na wanajeshi katika baadhi ya mitaa nao uliongeza hisia za tahadhari na kuimarisha uamuzi wa wananchi kusalia ndani.

Hata hivyo, kwa wale waliolazimika kusafiri kutokana na dharura, hali haikuwa rahisi.

 Usafiri wa umma ulipungua kwa kiasi kikubwa kutokana na watoa huduma wengi kutii agizo la Serikali

 hali iliyosababisha  adha kwa watu waliolazimika kutafuta usafiri wa kwenda hospitali, kazini au kwenye shughuli zao muhimu.

 Upungufu huo ulisababisha pia baadhi ya madereva wa bajaji na bodaboda kupandisha nauli mara dufu, jambo lililoleta malalamiko kutoka kwa wananchi waliokuwa na dharura.

Hali hii ilijengeka zaidi kutokana na hofu ya uwezekano wa maandamano ya Desemba 9, ambayo yaliongeza wasiwasi kuhusu usalama wa maeneo ya mijini na kusababisha

 maadhimisho ya mwaka huu kupita bila shamra shamra za watu kujumuika katika maeneo ya burudani kama baa na kumbi za muziki, tofauti na ilivyozoeleka miaka iliyopita.

Hali ilivyo eneo la Kariakoo makutano ya Barabara ya Lumumba na Mtaa wa Mkunguni kuelekea Barabara ya Bibititi kukiwa hakuna wafanyabiashara wala watu wanaopita leo Jumanne Desemba 9, 2025 saa 04:15 asubuhi, jijini Dar es Salaam ikiwa ni Sikukuu ya Uhuru wa Tanganyika.

Hali ya utulivu imetawala katika Manispaa ya Moshi leo, huku katika eneo la Soko la Mbuyuni maduka mengi yakiwa yamefungwa, 

Kwa kawaida mji wa Moshi huwa na pilika pilika nyingi kuanzia asubuhi hadi jioni, kwa muda wa asubuhi, mitaa iliyozoeleka kuwa na shughuli za kibiashara, misongamano ya watu na magari, leo imeonekana kuwa katika ukimya.

Hali ilivyo eneo la Mlimani City eneo hili ambalo limezoeleka kuwa na pilikapilika za magari na watembea kwa miguu lakini leo hakuna wafanyabiashara wala watu wanaopita tofauti na siku za nyuma, hii ni  leo Jumanne Desemba 9, 2025 saa 5 :17 asubuhi jijini Dar es Salaam ikiwa ni Sikukuu ya Uhuru wa Tanganyika.

Hali ilivyo Mtaa wa Loliondo Manispaa ya Kibaha Mkoa wa Pwani ambapo maduka mengi hayajafunguliwa leo Jumanne Desemba 9,2025 tangu saa kumi na mbili asubuhi hadi saa nne asubuhi ambapo eneo hilo ndilo wananchi wamekuwa wakifurika kila siku kupata mahitaji muhimu. 

Hali ya utulivu imetanda katika baadhi ya maeneo jijini Mbeya tofauti na ilivyokuwa jana Desemba 8, 2025.

Leo Jumanne Desemba 9, Watanzania wanaadhimisha Siku ya Uhuru wa Tanganyika ikiwa ni miaka 64, hata hivyo Serikali imewataka wananchi wasio na ulazima wa kutoka kubaki nyumbani.

Mwananchi imepita baadhi ya maeneo jijini Mbeya likiwamo Soweto ambako saa 5:00 asubuhi baadhi ya maduka yamefungwa, huku kukiwa hakuna watu mtaani.

Jana Desemba 8, katika Soko la Soweto kulishuhudiwa umati wa wananchi wakifanya ununuzi wa bidhaa.

Kutokana na utulivu uliotanda, huduma ya usafiri ukiwamo wa bajaji na daladala umekuwa changamoto, huku bodaboda wakionekana kwa nadra barabarani.

Mfanyabiashara, Suleiman Hashim amesema siku saba nyuma wananchi walinunua mahitaji, hivyo leo Desemba 9 ameamua kufunga biashara.

“Huenda ununuzi uliofanyika ni kwa sababu tulisikia Desemba 9 kutakuwa na maandamano, ndio maana hali ilikuwa vile,” amesema.

Hali ya utulivu imeshuhudiwa katika Barabara ya Sam Nujoma , ambapo watu wachache watembea kwa miguu na wenye vyombo vya usafiri wameonekana katika barabara hiyo tofauti na siku zote.

Wafanyabiashara na wasafirishaji katika eneo la Segerea wakiwa wamefunga maduka yao na kusimamisha huduma za usafiri leo Desemba 9, 2025.

Mwananchi imeshuhudiwa hali ya utulivu katika maeneo kadhaa ya mitaa ya eneo hilo.

Katika Kituo cha Mabasi cha Segerea Mwisho, hapakuonekana mfanyabiashara wala gari inayotoa huduma ya usafiri.

Hali ya utulivu imeshuhudiwa katika barabara za mitaa ya Tandale, ambapo watu wachache watembea kwa miguu na wenye vyombo vya usafiri wameonekana katika barabara hiyo tofauti na siku zote.

Kwa kawaida maeneo ya Tandale na viunga vyake huwa na hekaheka nyingi ikiwamo watembea kwa miguu, wauza vitafunwa pembeni ya barabara na mitaa, waendesha bodaboda na bajaji. Lakini leo ni tofauti kwani watu ni wachache na vyombo vya usafiri pia vichache na hata bodaboda ambazo huegesha pembezoni mwa barabara kwenye migundi (vituo vya bodaboda) hazipo zinapita moja moja.

Maeneo ya Magomeni yamekuwa na utulivu tofauti na siku nyingine, ikiwemo siku ya jana Jumatatu ambapo mara nyingi kunakuwa na pilikapilika za watu na shughuli mbalimbali.

Leo, Jumanne Desemba 9,2025 mitaa tofauti imeonekana kuwa tulivu, huku wakazi wengi wakibaki kwenye makazi yao.

Kuanzia Magomeni Usalama, Kota hadi Tanesco, hali imeripotiwa kuwa shwari na hakuna maduka wala magenge au huduma nyingine zinazopatikana au kufunguliwa.

Ukimya umetawala kiasi cha kufananisha mazingira na siku ya msiba, lakini hiyo ndiyo hali ya Jumanne mtu yupo nyumbani kwake.

Akizungumzia hali hiyo, Abdulrahman Maulid amesema kuwa wananchi wametii maelekezo ya Serikali kukaa nyumbani wakiadhimisha Siku ya Uhuru wa Tanganyika na wengi walikuwa wamejiandaa mapema kwa kununua mahitaji muhimu, tofauti na ilivyokuwa Oktoba 29.

“Safari hii sijaona mtu anayeangaika kutafuta mahitaji, kwa sababu maandalizi yalishafanyika. Kingine mtandao upo haujakatwa kama siku ile  (Oktoba 29) hivyo mtu hawezi kuwa ‘bored’,”

Hata hivyo, Mwananchi imeshuhudia mitaa mingine mtu mmoja mmoja wakitembea, huku baadhi ya maduka yakifunguliwa kwa muda kutoa huduma kisha yanafungwa.