Hasira za ‘Kamchape’ Kigoma zilivyosababisha mauaji baa

Kigoma. Ni ugomvi uliotokea ndani na nje ya Baa ya Utulivu iliyopo Kijiji cha Rungwe Mpya katika Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma na kusababisha mauaji ya Alfred Mikano, lakini kiini cha ugomvi kinatokana na kazi za kundi la Kamchape.

Kamchape ni timu ya waganga wa jadi ambapo kiongozi wao anaaminika kutoka Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), amekuwa akiendesha ramli na kutafuta wachawi na timu ya Watanzania katika ukanda wa mwambao wa Ziwa Tanganyika.

Kulingana na ushahidi uliotolewa kortini, marehemu alikuwa mjumbe wa kamati ya kamchape jambo lililosababisha mshitakiwa Sekeye Zakaria (43) kupata hasira za kundi hilo hivyo kujenga chuki na kuamua kumtafuta Mikano ili kumtia adabu.

Ni kutokana na ushahidi huo uliotolewa mbele ya Jaji John Nkwabi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Desemba 8,2025 mahakama hiyo ilimtia hatiani Sekeye Zakaria na kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Ilielezwa na mashahidi kuwa Mei 23, 2024 katika baa hiyo ya Utulivu, kulitokea ugomvi uliomhusisha Sekeye na mdogo wake aitwaye Yaledi Zakaria, ambaye alitoroka na hajatiwa mbaroni na polisi hadi hukumu inatoka, dhidi ya Mikano.

Kutokana na ugomvi huo, mmiliki wa baa alimjulisha mtoto wa Mikano juu ya tukio hilo ambaye alifika eneo la tukio na kumpeleka hospitali ya Kabanga, lakini kutokana na hali aliyokuwa nayo, alipewa rufaa kwenda hospitali ya Bugando.

Hata hivyo, wakiwa wamefika Wilaya ya Sengerema wakielekea Bugando, hali yake ilibadilika na kulazimika kulazwa kwa dharura hospitali ya Wilaya ya Sengerema ambapo alilazwa hapo hadi Mei 29, 2024 alipofariki dunia kwa kipigo hicho.

Ndipo Sekeye alipotiwa nguvuni na kushtakiwa kwa mauaji ambapo Jamhuri ukiongozwa na wakili wa Serikali mwandamizi, Edna Makala akisaidiana na wakili wa Serikali Clement Masua, uliita mashahidi 5 na kuwasilisha kielelezo kimoja.

Upande wa mashitaka uliegemea zaidi ushahidi wa shahidi wa pili wa Jamhuri, Abubakar Maseluko ambaye alidai kushuhudia ugomvi kati ya ndugu hao wawili na marehemu ambaye alikuwa ni mteja wake na ulitokea saa 2:30 usiku.

Alieleza kuwa akiwa katika baa yake hiyo, alikuwa na wateja ambao aliwataja kuwa ni Sekeye Zakaria, Alfred Mikano, Yared Zakaria na raia wa Burundi pia.

Wakati akiendelea kuhudumia wateja, alisikia kelele za ugomvi kati ya Mikano na ndugu hao wawili na kwamba Mikano alikuwa ni mmoja wa wanakamati ya Kamchape, jambo lililokuwa limemtia hasira Sekeye na kujenga chuki naye.

Shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa wateja wake hao walipigana ndani ya baa wakati Sekeye akipigana na Mikano, lakini walivutana hadi nje ya baa ambapo Sekeye na mdogo wake walishirikiana kumpiga Mikano hadi akapoteza fahamu.

Hapo ndipo shahidi wa kwanza wa Jamhuri, Egoni Mikano ambaye ni mtoto wa marehemu alipofika na kumchukua baba yake aliyekuwa na hali mbaya ya kiafya, ambapo baba yake alimweleza kuwa walimpiga ni Yaled Zakaria na Sekeye Zakaria.

Akishirikiana na mama yake, walimpeleka hospitali na kupewa rufaa kwenda Hospitali ya Bugando, lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya ndipo akalazwa katika hospitali ya wilaya ya Sengerema ambapo alifariki dunia Mei 29,2024.

Uchunguzi wa mwili wake ulifanywa na shahidi wa 3, Dk Jaffary Makombe wa hospitali ya Kasulu ambapo alibaini sababu za kifo ni kuvunjika kwa uti wa mgongo eneo la shingo na kusababisha kifo kwa kuwa sehemu hiyo ina mishipa ya fahamu.

Shahidi wa 4 ni mgambo, MG.231399 Pius Mbilizi ambaye ndiye aliyemkamata mshitakiwa wakati huo akiwa amezingirwa na wananchi katika eneo la shule ya sekondari wakati shahidi wa 5, Sajini Suleman ndiye alichunguza tukio hilo.

Kulingana na shahidi huyo, Yared Zakaria alifanikiwa kutoroka kabla ya kutiwa nguvuni na vyombo vya Dola na gadi sasa bado hawajaweza kumkamata.

Akiongozwa na wakili Mary Milali kutoa utetezi wake, Sekeye Zakaria alidai kuwa siku ya tukio saa 12:00 jioni, alikuwa katika eneo lake la biashara pamoja na mkewe, ambapo alipokea simu kutoka kwa shemeji yake akiomba tenga.

Shemeji yake huyo aliyetajwa kwa jina moja tu la Beatus aliyekuwa shahidi wake wa pili, alifika nyumbani kwa mshitakiwa na alipofika walizungumza, kula miwa na kuangalia televisheni hadi 4:30 usiku ambapo alimpa matenga mawili akaondoka.

Mshitakiwa alipinga vikali ushahidi wa shahidi wa kwanza wa Jamhuri akisema ni wa uongo wala hakushiriki kumuua Mikano kwa kuwa hakuwepo eneo la tukio na kusisitiza kuwa yeye sio mnywaji wa pombe kama ushahidi ulivyotolewa.

Alipinga pia ushahidi wa shahidi wa pili aliyeeleza ugomvi ulitokea katika baa yake akisema ni eneo lenye shughuli nyingi kwa vile ni eneo la soko na kuhoji aliwezaje kufanya tukio hilo kwa dakika 15 wakati uongozi wa kijiji ulikuwapo eneo hilo.

Alidai kuwa kuna mkanganyiko miongomi mwa mashahidi ambapo mtoto wa marehemu alidai baba yake hakuwa mlevi wakati Abubakar alieleza kuwa alikuwa ni mlevi na kueleza kuwa mkanganyiko huo unaonyesha ni ushahidi wa uongo.

Alifafanua kuwa mdogo wake, Yared Zakaria ambaye ni mshukiwa kwamba walishirikiana kufanya mauaji, alisafiri kwenda Dar es Salaa tangu mwaka 2021 na hajawahi kurudi hivyo ushahidi unaomhusha na mauaji ni usaliti na uongo.

Beatus katika ushahidi wake, alieleza kuwa Mei 23,2024 alikuwa amevuna nyanya kutoka katika bustani yake lakini hakuwa na matenga ya kutosha hivyo akayaomba kutoka kwa mshitakiwa na alikwenda kuyachukua nyumbani kwake.

Baada ya kula miwa, chakula cha jioni na kuangalia televisheni, alipewa matenga mawili na mshitakiwa na aliondoka nyumbani kwake saa 4:30 usiku na kwamba alikuja kushangaa kupewa taarifa kuwa Sekeye anahusishwa na mauaji hayo.

Katika hukumu yake aliyoitoa jana Jumatatu, Desemba 8, 2025, Jaji Nkwabi alisema hakuna ubishi kuwa Alfred Mikano ni marehemu na kifo chake sio cha asili na kwamba ni wajibu wa mahakama kupima kama mshitakiwa ndiye aliyemuua marehemu.

Jaji alisema wakati upande wa mashitaka unasisitiza na unathibitisha kwa vigezo vyote kuwa ni mshitakiwa akishirikiana na mdogo wake alimuua Mikano, upande wa utetezi kuwa mshitakiwa ametambuliwa kimakosa kwani alikuwa nyumbani.

Mshitakiwa alienda mbali na kudai yeye si mnywaji wa bia hivyo hicho kinachoitwa ni kutambuliwa na shahidi wa pili ambaye alidai ni mteja na rafiki yake hivyo ushahidi wake huo umefanyika kimakosa (mistaken identification).

“Lakini katika kesi hii, mshitakiwa alitumia muda kunywa pombe katika baa ya shahidi wa pili na hii ni kusema shahidi huyo alimhudumia mshitakiwa. Kulikuwa na mwanga uliotokana na taa za jua, hakuna na sababu ya kumtaja,”alisema.

Jaji alisema ni mtazamo wake kuwa utetezi wa mshitakiwa kuwa hakuwa eneo la tukio bali nyumbani hauna mashiko kwani ulitolewa nje ya utaratibu wa kisheria, wala shahidi wa pili hakuhojiwa juu ya hilo na alikuwa ndani ya eneo la kijiji.

“Mshitakiwa alikuwa ndani ya mipaka ya kijiji hicho hicho hivyo hii haimfanyi asiweze kutenda kosa lakini alitoa utetezi ambao hauna mantiki alipodai ndugu yake alisafiri kwenda Dar es Salaam na hajawahi kurudi,”alieleza Jaji Nkwabi.

Kuhusu madai ya mshitakiwa kuwa mashahidi wa Jamhuri walitoa ushahidi wa kujikanganya kuhusu muda wa tukio, Jaji alisema hakubaliani na hoja hiyo kwani sio rahisi kwa sababu katika mazingira hayo, sio rahisi kuangalia saa.

“Shahidi wa pili hakuhojiwa kuhusu ugomvi kuchukua dakika 15 katika baa yake na kwamba viongozi wa kijiji walikuwepo hivyo haiwezi kuibuliwa katika hatua ya utetezi. Mkanganyiko uliopo ni mdogo na haujaenda katika mzizi wa kesi.”

Jaji alisema baada ya kupitia ushahidi wa upande wa mashitaka kwa ujumla wake na utetezi wa mshitakiwa, anaona Jamhuri imethibitisha mashitaka hayo pasipo kuacha mashaka kuwa ni mshitakiwa ndiye aliyesababisha kifo cha Mikano.

Kuhusu uwepo wa nia ovu ya kumuua Mikano, Jaji alisema sehemu ambayo walimpiga marehemu (shingoni) na idadi ya mapigo waliyompiga na kutoroka eneo la tukio bila kutoa msaada kumpleka hospitali, alidhamiria kufanya mauaji.

“Lakini pia ile kuwa na chuki dhidi ya marehemu ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati ya Kamchape iliyosababisha mtuhumiwa huyo kupata hasira za kundi la watu wa Kamchape ni moja ya sababu kuonyesha nia ovu ya kutenda kosa,” amesema.

Ni kwa msingi huo, mahakama imezingatia mshitakiwa na mdogo wake walitoroka eneo la tukio, walishirikiana kumpiga marehemu, eneo walilomshambulia, idadi ya mapigo waliyoyafanya na nguvu waliyoitua inaonyesha uwepo wa nia ovu.

Jaji akahitimisha kwa kusema upande wa mashitaka umeweza kuthibitisha shitaka la mauaji pasipo kuacha mashaka kuwa ni Sekeye ndiye aliyemuua Mikano hivyo anamtia hatiani na kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.