Kicheko bei ya petroli, dizeli zashuka Zanzibar

Unguja. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura), imetangaza kushuka kwa bei za mafuta huku mafuta ya taa yakisalia kwenye bei yake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari leo Jumanne Desemba 9, 2025 na kuthibitishwa na Meneja wa kitengo cha uhusiano Zura, Mbaraka Hassan Haji, bei hizo zitaanza kutumika rasmi leo.

Amesema, kwa mwezi huu (Desemba) lita moja ya petroli itauzwa kwa Sh2,815 kutoka Sh2,868 ya mwezi uliopita (Novemba) sawa na punguzo la Sh53.

Pia, bei ya dizeli itakuwa Sh2,944 kutoka Sh3,004 ya Novemba sawa na punguzo la Sh60 na bei ya mafuta ya taa imesalia kwenye bei ya Sh3,000 kama ilivyokuwa  Novemba.

Amesema, lita moja ya mafuta ya ndege itauzwa kwa Sh2,376 kutoka Sh2,405 sawa na punguzo la Sh29.

“Sababu za kupungua kwa bei za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya ndege kwa mwezi huu  ni kupungua bei za ununuzi katika soko la dunia pamoja na kupungua kwa gharama za uagizaji wa mafuta kutoka soko la dunia hadi Zanzibar,” amesema. 

Mamlaka hiyo, imewasisitiza wananchi kununua mafuta katika vituo rasmi vilivyosajiliwa, pamoja na kudai risiti za kielektroniki, ili kuimarisha uwazi, usimamizi na urahisi wa kupata huduma endapo changamoto yoyote itajitokeza.

Hivi karibuni wakati akifanya mahojiano maalumu na Mwananchi, Mkurugenzi Mkuu Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC), Akif Ali Khamis alisema shirika hilo linaendelea na ujenzi wa bohari yenye uwezo wa kuhifadhi mafuta lita 60 millioni kwa lengo la kudhibiti bei za mafuta.

Alisema, bohari tatu zilizopo Mtoni zina uwezo wa kuhifadhi mafuta lita 15 millioni ambazo hazitoshelezi kwa mahitaji ya jamii, ndio maana hakuna bei maalumu ya mafuta.

Wakizungumza kuhusu punguzo la bei za mafuta, wananchi kisiwani hapa wamesema suluhisho pekee ni kujengwa bohari ya mafuta, kwani hakuna bei maalumu za ununuzi wa mafuta.

Khalid Jecha mkazi wa Kikwajuni amesema amefurahishwa na kupungua kwa bei ya mafuta kwa mwezi huu ila Serikali ijitahidi kuweka bei maalumu kila mwezi.

Kwa upande wake, Khalifa Mansour Shariff amesema kushuka kwa bei za mafuta ni jambo la faraja kwao kwani wataendelea kufanya shughuli bila ya usumbufu.