Mgunda awabana mastaa Namungo | Mwanaspoti

KOCHA Mkuu wa Namungo, Juma Mgunda amesema anatambua ugumu wa kuwaachia wachezaji katikati ya mashindano na kuwabana akiwapa programu maalumu ili waitumie wakiwa mapumziko kusudi wakirudi wawe timamu kimwili.

Mapumziko hayo ni maalumu ya kupisha timu za taifa kuwakilisha nchi zao katika fainali za Afcon 2025 zinazotarajiwa kufanyika Morocco kuanzia Desemba 21 hadi Januari 18 mwakani.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mgunda alisema mara baada ya kuibuka na ushindi katika mechi iliyopigwa na jua kali dhidi ya Mbeya City alikaa kikao na wachezaji ili kuzungumza ni namna gani wanaenda kupumzika na mipango  ya wanarudi vipi.

“Hakuna kazi ngumu kama kupumzika katikati ya mashindano, ni lazima kutokana na ratiba ya Fifa ila kwa wachezaji wetu ni mtihani, kwani wanarudi tunaanza moja na ili kukwepa changamoto hiyo nimetoa programu kwa wachezaji,” alisema Mgunda na kuongeza:

“Nitakuwa naifuatilia kwa kuwasiliana nao, lengo ni kutaka kurudi na kuendana na kasi ilivyo sasa, ligi ni ngumu mipango na mbinu bora ndizo zinaamua matokeo na wachezaji hawatakiwi kubweteka walipo.”

Mgunda aliongeza,  ushindani uliopo katika ligi hauna ukongwe ila  ni ubora ndiyo unaamua matokeo,  ndiyo maana matokeo yamekuwa ya kushangaza kwa timu ambazo hazina mipango mizuri.

“Tutarudi Januari baada ya michuano ya Afcon kumalizika katikati ya Januari mwakani, naamini wachezaji watafanya kile nilichowaelekeza ili tutakaporejea tuendelee tulipoishia,” alisema nyota huyo wa zamani wa Coastal Union na Taifa Stars aliyewahi kuzinoa pia Coastal, Simba na Taifa Stars.