TANZANIA Prisons imesema licha ya matokeo kuwa magumu, lakini inaridhishwa na kiwango bora cha wachezaji na namna wanavyojituma uwanjani, huku benchi la ufundi likianza kusaka nyota wawili wa kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji kumaliza tatizo la mabao.
Prisons haijawa na matokeo mazuri sana kutokana na pointi saba ilizokusanya katika mechi saba, huku ikiruhusu mabao matano na kufunga matatu tu, ikiwa nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Zedekia Otieno amesema mbali na matokeo waliyonayo, lakini anafurahishwa na juhudi binafsi za wachezaji wake uwanjani na makosa yanayoonekana atayafanyia kazi.
Amesema wakati ligi ikisimama, huku dirisha dogo likifunguliwa siku chache zijazo, ataangalia sehemu ya kuongeza nguvu kwa wachezaji wawili ambao si wanakuja kukaa benchi bali kuleta mabadiliko.
“Tumekuwa na tatizo la kutumia nafasi tunazopata, lakini tusiangalie tu upande wa matokeo bali namna timu inavyocheza, tunaenda dirisha dogo tunaweza kuongeza wawili ambao watakuja kubadili kitu hasa eneo la mbele,” amesema Otieno.
Kwa upande wake kipa wa timu hiyo, Mussa Mbisa amesema bado wanayo nafasi ya kufanya vizuri licha ya matokeo waliyoanza nayo na kukuri ligi imeanza kwa ugumu kwa kila timu kuonyesha ushindani.
Kuhusu makosa yanayoonekana kwa mchezaji mmoja mmoja, kipa huyo wa zamani wa Mwadui na Coastal Union, amesema hilo ni jukumu la kocha kuyafanyia kazi na kutoa matumaini Prisons kumaliza nafasi nzuri Prisons.
“Ligi ni ngumu kila timu inaonesha upinzani, Prisons bado tunaweza kufanya vizuri ukiachana na matokeo tuliyoanza nayo, sehemu yenye makosa kocha atafanyia kazi na tutamaliza ligi nafasi nzuri,” amesema Mbisa.