Dar es Salaam. Wakati Tanzania Bara ikisherehekea miaka 64 ya uhuru wake, Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza msamaha kwa wafungwa 1,036 baadhi akiwapunguzia adhabu na wengine kuachiwa huru.
Kati ya wafungwa hao waliopata msamaha huo wa Rais, 22 wameachiwa huru, huku 1,014 wakipunguziwa adhabu zao na watakabaki gerezani kutumikia sehemu ya vifungo vilivyobaki.
Idadi ya wafungwa walioachiwa huru leo, Desemba 9, 2025 inafanana na ile ya waliochiwa katika msamaha wa Rais wakati wa sherehe za uhuru za mwaka jana.
Msamaha huo wa Rais kwa wafungwa, hutolewa Desemba 9, kila mwaka. Mkuu wa nchi chini ya ibara ya 45(1)(a)-(d) ya Katiba ya Tanzania, amepewa mamlaka ya kutoa msamaha kwa wafungwa.
Taarifa ya msamaha huo, imetolewa leo Jumanne, Desemba 9, 2025 na Wizara ya Mambo ya Ndani na kutiwa saini na Waziri wa wizara hiyo, George Simbachawene.
Katika taarifa hiyo, Simbachawene amesema ni matarajio ya Serikali kuwa wafungwa walioachiwa huru watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee gerezani.
Makundi yaliyonufaika na msamaha huo, kwa mujibu wa taarifa hiyo ni waliohukumiwa kifungo cha kuanzia miaka miwili na kuendelea na ambao tayari wametumikia robo ya adhabu zao gerezani.
Wafungwa hao kwa mujibu wa masharti ya Katiba, wamepunguziwa moja ya sita ya adhabu zao wanazozitumikia sasa baada ya punguzo la kawaida la moja ya tatu linalotolewa chini ya Kifungu cha 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58.
Wengine walionufaika ni wafungwa wenye magonjwa ya kudumu au sugu ambao wapo kwenye hatua ya mwisho na wafungwa wazee wenye umri wa miaka 70 au zaidi.
“Wengine ni wafungwa wa kike walioingia na ujauzito gerezani au wenye watoto wanaonyonya au wasionyonya waliohukumiwa kifungo cha mwaka mmoja na kuendelea, wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili wasio na uwezo wa kufanya kazi,” imeeleza taarifa hiyo.
Pia, wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kuwekwa kizuizini na wawe wamekaa gerezani kuanzia miaka 10 au zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wafungwa wanaotumikia vifungo vya nje na wale waliowahi kukiuka masharti chini ya Sheria ya Bodi za Parole Sura ya 400 na kurudishwa gerezani kutumikia adhabu zao, Sheria ya Huduma kwa Jamii Sura ya 291 na Kanuni za Kifungo cha Nje, hawatahusika na msamaha huo.
Wengine wasiohusika na msamaha huo ni, wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo gerezani kwa makosa ya uhujumu uchumi, matumizi mabaya ya madaraka, utakatishaji wa fedha, rushwa na usafirishaji au kujihusisha kwa namna yoyote ile na dawa za kulevya ikiwemo bangi.
Pia, wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo gerezani kwa makosa ya kujamiiana, utekaji au wizi wa watoto, kupoka, kuwapa mimba wanafunzi au makosa yoyote yanayohusiana na ukatili dhidi ya watoto na biashara haramu ya binadamu.
“Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo gerezani kwa makosa ya unyang’anyi, unyang’anyi wa kutumia nguvu, unyang’anyi wa kutumia silaha, kumiliki silaha, risasi, milipuko au kujaribu kutenda makosa hayo hawahusiki na msamaha huu,” imeeleza taarifa hiyo.
Imeeleza wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo gerezani kwa makosa ya kukutwa na viungo vya binadamu na kujihusisha na nyara za Serikali au ujangili.
Wengine wasiohusika ni waliofungwa kwa kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali au kusaidia kutendeka kwa makosa hayo, kujaribu kuua, kujiua au kuua watoto wachanga, makosa ya ugaidi, uharamia na makosa ya kimtandao.
Pia, wamo wafungwa wanaotumikia kifungo cha pili au warudiaji, waliowahi kupata msamaha wa Rais, waliotenda makosa ya kinidhamu gerezani na hayajatimiza miaka mitatu, wafungwa wa madeni, waliopatikana na hatia ya mauaji au kuhukumiwa adhabu ya kifo na wanaotumikia kifungo cha maisha gerezani.
