Katika karne ya 19, ardhi ya Tanganyika ilijumuisha jamii na makabila mbalimbali, wakiishi maisha ya jadi yaliyokuwa ya wakulima na wafugaji.
Yote haya yalifanyika kabla ya kile kilichoitwa: “Mashindano ya Kugawana Afrika,” (The Scramble for Africa).
Mwaka 1885, katika mkutano wa Berlin uliohusu kile kilichoitwa: “Mapatano ya Kugawana Afrika,” nchi za Ulaya ziligawana Bara la Afrika.
Katika kugawana huko, Tanganyika ilichukuliwa kuwa koloni la Ujerumani. Wajerumani walipoanza kuitawala Tanganyika walianza kubadilisha maisha ya watu wa ndani kwa msukumo wa kilimo cha pamoja, wakachukua ardhi, wakata kodi na wakaanzisha kazi za shuruti,jambo lililokera na kuteka mioyo Watanganyika.
Wajerumani waliweka utawala wa moja kwa moja. Hawakuheshimu Serikali za mtaa au makabila, bali waliteka ngazi ya uongozi, wakawafukuza viongozi wa asili waliopinga ukoloni.
Kwa mfano, waliweka vikwazo vikali, mateso na mauaji ya viongozi waliojitoa kupinga ukoloni walikutana na mkono wa chuma.
Hapo ndipo moto wa upinzani ulipoanza kuwashwa na tamaa ya uhuru ikawaka, kisha mapambano yakaanza.
Baada ya kero za muda mrefu za Wajerumani dhidi ya wazawa, baadhi ya makabila na viongozi wa jadi walisimama, wengine wakaanzisha vita dhidi ya Wajerumani.
Chifu Mkwawa wa kabila la Wahehe ni mfano mkongwe. Wakati wa vita dhidi ya Wahehe, miaka ya mapambano ilikuwa 1891 hadi 1898.
Wajerumani walikabiliana na upinzani mkali wa Wahehe, Mkwawa alipigania uhuru wa watu wake kwa miaka kadhaa.
Ingawa vita ya Wahehe dhidi ya Wajerumani ilikuwa ndiyo kubwa kwa wakati huo, haikuwa vita pekee dhidi ya wakoloni.
Kulikuwa na mapigano madogo madogo ya makabila kadhaa, kila mtu aliyeweza kujitetea alijitokeza. Ukombozi ukawa ndoto inayowaka mioyoni mwa watu wengi.
Lakini nguvu ya wakoloni wa Ujerumani ilikuwa kubwa, mizinga, silaha za kisasa kwa wakati huo, manyanyaso na mateso, kwa hiyo upinzani mara nyingi ulidhoofika bila mafanikio makubwa.
Hata hivyo, wimbi la upinzani lilianza kuipa Tanganyika sura ya kishujaa.
Vita ya Maji Maji (1905–1907)
Vita ya Maji Maji ilikuwa ‘mwamba’ mkubwa wa upinzani dhidi ya wakoloni.
Kutokana na kuongezeka kwa ukandamizaji, kodi kubwa, kazi za kushurutishwa, kukamatwa kwa ardhi nzuri, hasira ikazidi kukua.
Hali hiyo ilifika kwenye upeo wake mwaka 1905. Hapa ndipo ilipoanza vita ya Maji Maji ambayo kumbukumbu za kihistoria zinaonesha kuwa ilianza na kudumu kati ya Julai 1905 na Julai 1907.
Chimbuko la vita hivyo ni Kijiji cha Nandete, Mkoa wa Lindi na iliongozwa na Kinjeketile Ngwale aliyewaaminisha wenzake kuwa maji yanaweza kuzuia risasi.
Watu 250,000 hadi 300,000 walipoteza maisha wakati wakipambana na Wajerumani.
Jina Maji Maji lilitokana na imani ya Watanganyika wapambanaji waliopigana dhidi ya Wajerumani, waliamini kuwa, ‘maji ya uzima’ waliyopatiwa na watawa wa jadi yangekuwa kama ngao ya kiroho, kwamba yangegeuza risasi ya Wajerumani kuwa maji, hivyo ishindwe kumdhuru mtu.
Hali hii ilitoa matumaini, ujasiri, roho ya kujiunga na vita, hata kama silaha ilikuwa duni. Wengi walioingiwa na imani hiyo walijiunga katika mapambano hayo.
Mapambano yalienea kwa maeneo mengi. Watu kutoka jamii mbalimbali waliingia kwenye mapambano, upinzani ulikuwa mkubwa, umoja ulikuwa wa kipekee. Huu ulikuwa wito wa kufufua heshima, ardhi, utu wa mtu dhidi ya ukandamizaji mkubwa wa Wajerumani.
Lakini nguvu ya kikoloni ya Wajerumani ilikuwa kubwa kwa jeshi, silaha, mizinga na mbinu za kisasa kwa wakati huo. Kutokana na hali hiyo, mapigano yalishindwa kuleta mabadiliko ya haraka.
Mapigano yalifupishwa kwa ukatili mkubwa, maelfu ya watu waliuawa, mazao yakaharibika, kijiji kimoja baada ya kingine kiliporwa na mateso makubwa yalitokea. Wimbi la Maji Maji likashindwa.
Lakini ingawa mapambano ya Watanganyika hao yalishindwa, ‘Maasi’ ya Maji Maji yalikuwa kama nguzo ya uhuru. Yaliashiria kuwa watu wa Tanganyika hawatanyamaza milele.
Yalionesha kwamba hawakuwa tayari kukubali utawala wa kikoloni bila vita. Hapo nipo zama mpya ya mapambano ya kisasa ya ukombozi.
Baada ya mapambano haya, Wajerumani walibadilisha mikakati yao. Wakapunguza vitendo vya kushurutisha kazi, wakapunguza kazi za mabwana, wakawa na sera ya kilimo kwa wakulima wa Kiafrika badala ya kuanzisha mashamba makubwa ya wakoloni. Hii ilikuwa kama ushindi mdogo wa kweli wa wananchi.
Ingawa Wajerumani walipata upinzani mkali kutoka kwa Watanganyika duni wa wakati huo, walidumu kama watawala wa Tanganyika hadi Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia (1914 hadi 1918).
Lakini mgogoro wa vita hiyo ulipokuja, Tanganyika ikapigwa na mawimbi ya vita kwa sababu mwishoni mwa vita hiyo Wajerumani walishindwa.
Mwaka uliofuata wa 1919, kwa mkataba wa amani wa vita (The Treaty of Versailles), makoloni ya Wajerumani, Tanganyika ikiwamo yakawekwa mikononi mwa mataifa washindi.
Tanganyika ikakabidhiwa mikononi mwa Waingereza kama mkoloni mpya, lakini hiyo ikawa ni rasmi chini ya udhamini wa Shirikisho la Mataifa (League of Nations). Wajerumani waliangushwa, na mwanzo mpya ukawa Tanganyika chini ya Waingereza.
Tangu mwaka 1920, Taifa hili liliitwa rasmi, Tanganyika Territory. Waingereza, tofauti na Wajerumani, walitumia utawala wa kutawala kwa njia isiyo ya moja kwa moja.
Waliweka makabila na machifu wa asili kama wasimamizi wa ngazi za chini na wao wenyewe walichukua mamlaka ya juu.
Hii ilileta mfumo tofauti wa utawala. Hata hivyo, waliendeleza unyonyaji, kilimo cha zao la biashara kwa masilahi ya mkoloni, waliendelea kutoza kodi na ukandamizaji wa kiuchumi ukaendelea.
Ingawa mambo ya kiuchumi na kijamii yalianza kuchukua mwelekeo tofauti, ukoloni ukabaki dhahiri; umaskini, ukosefu wa fursa na unyonyaji wa kiuchumi uliendelea.
Kuibuka kwa fikra za Uhuru
Katika utawala wa Waingereza, baada ya vita ya Pili ya Dunia (1939-1945), hali ya dunia ilipobadilika, mataifa ya Ulaya walijitokeza wakikosoa ukoloni, Waafrika waliweza kusimama kidete kuhakikisha wanapata haki zao.
Wengi waliopata elimu; walimu, wasomi na washauri wa jamii wakaanza kujiuliza, “kwanini tunaendelea kubeba mizigo na mateso ya ukoloni?”
Hapa ndipo fikra ya uhuru ilianza kukua na wito wa haki, usawa, utu na mustakabali wa Tanganyika lipoamka.
Katika muktadha huu, kuibuka kwa Tanganyika African National Union (Tanu), chama cha kisiasa ambacho kilitetea haki za Watanganyika kilikuwa nguzo muhimu.
Tanu ikawa jukwaa la umoja, matumaini na mwanga wa uhuru. Hali hii iligusa mioyo ya wengi kuanzia vijana, walimu, wafanyakazi na hata wakulima. Wengi wakaanza kuona uhuru kama ndoto ya kweli inayowezekana.
Katika miaka ya mwisho ya utawala wa ukoloni, Waingereza waliona kuwa hawana njia ya kudumu ya kukandamiza hisia za watu.
Viongozi wa Tanganyika, waliosoma, waasisi wa Tanu, walifanya mikutano, mijadala na maandamano wakipinga ukoloni. Hali ya kisiasa ikabadilika.
Mei 1961, Waingereza wakakubali mchakato wa utekelezaji wa Serikali ya Tanganyika kujitawala.
Tanganyika ikapewa utawala wa ndani, na kiongozi wa Tanu, Julius Nyerere, akawa waziri mkuu wa kwanza wa Tanganyika. Hii ilikuwa hatua kubwa kuelekea uhuru kamili.
Katika mkutano uliofanyika Dar es Salaam, Serikali ya Waingereza, kupitia mwakilishi wake ikakubali kuwaondoa wakoloni rasmi na Tanganyika ikaachwa huru.
Hii ilifanyika Desemba 9, 1961, siku ambayo ardhi ya Tanganyika, yenye maumivu, mateso, kushurutishwa, upinzani na kila aina ya unyonyaji, ikawa Taifa huru.
