Tafakuri ya fursa na changamoto kwa Watanzania

Uhai wa Tanganyika (sasa Tanzania) kama Taifa huru, umetimiza miaka 64, umri ambao ndani yake kuna mkusanyiko wa mafanikio, mitihani na dhoruba.

Ndani ya miaka hiyo, Tanganyika ilijenga misingi yake kwa maono ya pamoja na mfumo wa usawa, utu, amani na mshikamano.

Katika kipindi hicho, Taifa limepiga hatua kadhaa mbele kimaendeleo na kiuchumi, hata hivyo licha ya mafanikio hayo, limekabiliwa na changamoto lukuki ikiwemo kuporomoka kwa demokrasia ya vyama vingi.

Safari ya uhuru wa Tanganyika, imepitia hatua nyingi zenye uzito wa kihistoria. Miaka michache baada ya uhuru, mwaka 1964, Tanganyika iliamua kuungana na Zanzibar na kuzaliwa Taifa jipya la Tanzania.

Muungano huo uliibeba dhamira ya kuunganisha watu wa pande mbili zenye historia, tamaduni na mifumo ya utawala tofauti, lakini zenye imani ya kujenga Taifa moja lenye nguvu zaidi ya sauti ya kila upande peke yake.

Miongo iliyofuata ikaweka msingi wa utawala na uongozi ulioimarishwa na Katiba ya mwaka 1977, ambayo hadi sasa imebeba mizani ya madaraka, imeweka mipaka ya mamlaka ya dola na imekuwa mwongozo wa safari ya kisiasa ya Taifa.

Mabadiliko hayo hayakutokea katika mazingira mepesi. Mabadiliko ya kisiasa ya mwaka 1992, Tanzania ilirejea katika mfumo wa siasa za vyama vingi, baada ya miongo takriban mitano.

Hiyo ilitazamwa kama ishara ya Taifa linalokua, linalokubali maoni tofauti na linaloamini ushindani wa hoja kama sehemu ya ukuaji wa demokrasia.

Mabadiliko hayo yalifungua milango ya uhuru zaidi wa mawazo, pia yakaleta changamoto za namna ya kusimamia ushindani wa kisiasa bila kuruhusu misuguano ichafue tunu za amani na utulivu.

Ndani ya miaka 64, Tanzania imejijengea hadhi ya kipekee barani Afrika, nchi iliyosimama mbali na migogoro ya kijamii na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozikumba baadhi ya nchi jirani.

Katika kipindi hicho, Tanzania imejitwalia hadhi ya kuwa kisiwa cha amani. Hata hivyo, kadiri siku zinavyoenda, ukweli kwamba amani ni jambo linalopaswa kulindwa unazidi kudhihirika.

Matukio ya Oktoba 29, yametia doa historia ya amani nchini, yakionyesha namna sintofahamu za kisiasa zinavyoweza kuwa tishio kama Taifa halitasimama pamoja kukemea, kuelimisha, na kuweka mifumo imara ya mawasiliano ya kisiasa na kijamii.

Kwa upande mwingine, mizengwe inayohusishwa na rushwa na ufisadi imeendelea kuwa mzigo kwa nchi. Rushwa imekuwa ikipunguza kasi ya maendeleo, ikizidisha gharama za maisha na kuathiri huduma za kijamii huku pengo kati la wenye nacho na wasio nacho likiongezeka.

Vita dhidi ya rushwa imekuwa ikipigwa, lakini changamoto za mienendo hiyo zimeonyesha Taifa linahitaji zaidi ya kaulimbiu, linahitaji maboresho ya mifumo, uwajibikaji thabiti na ushiriki wa wananchi katika kusimamia haki na uwazi.

Akizungumzia miaka 64 ya uhuru, mtaalamu wa siasa, Said Majjid anasema Tanzania ya leo ina fursa nyingi zilizojengwa na misingi ya kihistoria na jiografia yake.

“Tunayo ardhi yenye rutuba, rasilimali nyingi kuanzia madini, maji, gesi asilia, mbuga za wanyama, hifadhi za kipekee kama Serengeti na Ngorongoro na nafasi ya kiuchumi inayotokana na kupakana na nchi nane,” anasema.

Anasema ni Taifa lililo katikati ya Afrika Mashariki na Kusini, eneo linaloweza kuwa kitovu cha biashara ya kikanda endapo uwekezaji wa kutosha katika miundombinu utaendelea.

Majjid anasema amani ndiyo turufu pekee ya mafanikio katika kuzitumia fursa zilizopo, kwani Tanzania kwa jiografia yake ni kivutio kwa wawekezaji na watafiti, ndio maana imeendelea kupewa nafasi muhimu katika majadiliano ya kikanda na kimataifa.

Anaeleza nafasi ya vijana ambao sasa ni zaidi ya nusu ya idadi ya Watanzania imekuwa fursa lakini changamoto kwa upande mwingine.

“Kundi hili lina nguvu, mawazo na ubunifu ambao kama utaunganishwa vizuri kupitia mifumo ya elimu, mafunzo ya ufundi, teknolojia na upatikanaji wa mikopo midogo, unaweza kuwa chachu ya uchumi wa karne hii,” anasema.

Anasisitiza bila kutengeneza mazingira rafiki ya ajira na ujasiriamali, kundi hilo linaweza kugeuka kuwa chanzo cha mivutano ya kijamii.

Dk Anord Tweve, mtaalamu wa mabadiliko ya tabianchi, anasema ni vigumu kutathmini miaka 64 ya uhuru wa nchi bila kuangazia jinsi taifa linavyopambana na mabadiliko ya tabianchi.

Anasema mvua zisizotabirika, ukame unaozidi kuongezeka na mafuriko ya mara kwa mara ni changamoto zinazoathiri moja kwa moja sekta za kilimo, mifugo na usalama wa chakula.

“Kwa nchi ambayo zaidi ya asilimia 65 ya wananchi wake wanategemea kilimo, mabadiliko haya yanahitaji sera madhubuti, utafiti na uwekezaji wa kisasa,” anaeleza.

Mchambuzi wa siasa, Profesa Samone Mjema anasema miaka 64 ya uhuru imeifikisha Tanzania hatua ya ukomavu ambayo inahitaji uamuzi mkubwa kuhusu mustakabali wake.

Anasema Taifa linapaswa kuangalia upya mifumo ya utawala, kuimarisha muungano kwa kuzingatia changamoto zilizojitokeza na kuunda katiba inayokidhi mazingira ya sasa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

“Kizazi kipya kina matarajio tofauti, dunia imebadilika, hivyo hata misingi ya utawala lazima iendane na kasi hiyo,” anasisitiza Profesa Mjema.

Kwa upande wake, mchambuzi wa siasa na jamii, Dk Patrick Mcharo anaona Tanzania inahitaji kujenga mtiririko mpya wa mawasiliano baina ya Serikali, vyama vya siasa na wananchi, ili kuondoa nafasi ya sintofahamu zinazoweza kuchochea taharuki kama zile za Oktoba 29.

Kwa mtazamo wake, nchi imefika hatua ambayo amani lazima iwe mradi wa kitaifa unaosimamiwa kimfumo, sio jambo la kubahatisha.

Anashauri kuimarishwa kwa vyombo vya usuluhishi, majadiliano ya kisiasa ya mara kwa mara na kuwekwa wazi taarifa za umma ili kupunguza mianya ya upotoshaji.

Kwa upande wake, mtaalamu wa maendeleo ya kiuchumi kutoka katika moja ya taasisi za kimataifa, Hellen Ngwasi anaamini Tanzania imebeba hazina ambayo endapo itawekewa mikakati thabiti, italifanya Taifa kuongeza pato lake maradufu ndani ya miaka 10 ijayo.

Anaeleza miradi ya kimkakati kama Reli ya Kisasa (SGR), upanuzi wa bandari, uwekezaji katika utalii na uchumi wa gesi vinaonyesha dira sahihi.

Hata hivyo, anasisitiza vita dhidi ya rushwa lazima iwe ya kimfumo na inayoshirikisha taasisi binafsi, ili mazingira ya uwekezaji yawe na uaminifu.

Anaeleza miaka 64 ya uhuru ni mwanya wa kuonyesha nchi ilikotoka, ilipo na inakokwenda. Ni kipindi kinachoonyesha Taifa lililohimili mawimbi ya kihistoria na bado likasimama imara.

“Ni hadithi inayohitaji maboresho ya kila kizazi, lakini ikiwa na kanuni moja kuwa, Tanzania inaweza kuwa bora zaidi ya ilivyo leo, kama itaendelea kuwekeza katika umoja, misingi ya haki, uwajibikaji na matumizi sahihi ya fursa ilizopewa na historia na jiografia yake,” anasema Hellen.