Tatizo Simba ipo hapa, yapewa ujanja kujiokoa mapema

NINI tatizo Simba? Ndilo swali linalozunguka katika vichwa vya mashabiki wa timu hiyo kutokana kukumbana na kipigo cha nne msimu huu ndani ya mechi 12 za mashindano.

Juzi, Jumapili, ilikuwa siku mbaya kwa wana Simba kufuatia kufumuliwa mabao 2-0 na Azam FC ikiwa ni siku chache tangu ipoteze mechi mbili mfululizo za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Tofauti na msimu uliopita ambapo ndani ya mechi 12 za kwanza Simba ilipoteza mechi mbili, moja ikiwa ya Ngao ya Jamii na nyingine ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga kwa bao 1-0, na kushinda mechi nane dhidi ya Coastal Union (1-0), Tabora United (sasa TRA United) kwa mabao 3-0, Fountain Gate (4-0), Al Ahly  Tripol (3-1), Azam (2-0),  Dodoma Jiji (1-0), Tanzania Prisons (1-0) na Namungo kwa mabao 3-0.

Kipindi hicho sare zikiwa mbili katika mechi ya kwanza dhidi ya Al Ahly Tripoli (0-0) na nyingine ni dhidi ya Coastal Union kwa mabao 2-2 ilikuwa ni mechi ya ligi ile ya kwanza waliyoshinda ilikuwa Ngao ya Jamii.

Msimu huu hali inaonekana kuwa tofauti, wameshuka kwa asilimia 16.7, kivipi? Msimu uliopita ndani ya mechi 12 za kwanza katika mashindano yote, Simba ilikuwa na ushindi kwa asilimia 66.7 na msimu huu ni sawa na asilimia 50.

Ndani ya kipindi hicho kifupi tayari timu hiyo imefanya mabadiliko matatu ya benchi la ufundi, awali ilianza msimu ikiwa chini ya Fadlu Davids uliokuwa msimu wa pili kwake, lakini kwa makubaliano ya pande mbili aliachana na miamba hiyo baada ya mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa katika hatua za awali dhidi ya Gaborone United ambapo Simba ilishinda kwa bao 1-0 ugenini Botswana.

Timu hiyo ikawa chini ya  kocha Seleman Matola katika mechi moja ya Ligi dhidi ya Fountain Gate na kushinda kwa mabao 3-0, ndipo viongozi wakafanya mpango wa kuongeza nguvu katika benchi hilo kwa kumuomba aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ kwa ajili ya mechi ya marudiano dhidi ya Gaborone.

Sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, ilitosha kwa Simba kutinga raundi pili kuwania nafasi ya kutinga makundi ya michuano ya kimataifa na viongozi wa Wekundu hao wa Msimbazi baada ya siku chache  wakamalizana na Dimitar Pantev aliyekuwa kocha wa Gaborone.

Ndani ya siku 61, kocha huyo aliyetambulishwa kama meneja aliiongoza timu hiyo kutinga makundi kufuatia ushindi wa 3-0 dhidi  Nsingizini Hotspurs ya Eswatini.

Pantev akapata ushindi wa kwanza katika Ligi dhidi ya JKT Tanzania kwa mabao 2-1 kabla ya kupoteza mechi mbili mfululizo za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ya kwanza akiwa nyumbani dhidi ya Petro Luanda kwa bao 1-0 na nyingine akiwa Bamako, Mali dhidi ya Stade Malien kwa mabao 2-1.

Vipigo hivyo viliwafanya mabosi wa Simba kukaa chini ya kocha huyo raia wa Bulgaria na kusitisha mkataba wake kisha ikatangaza kikosi hicho kitakuwa chini ya Matola ambaye naye ameonja kipigo chake cha kwanza dhidi ya Azam. Ndani ya mechi 12 za msimu huu, Simba imefunga jumla ya mabao 17 katika mashindano yote pungufu ya matatu na msimu jana ambapo walifunga mabao 20, kikosi hicho kimeruhusu mabao manane zaidi kwa matatu na idadi ambayo iliruhusu msimu uliopita katika mechi hizo.

Licha ya kuondokewa na baadhi ya wachezaji kama Fabrice Ngoma, Leonel Ateba, Fondoh Che Malone, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na wengine, lakini wachezaji waliosalia ambao msimu uliopita wakiobeba timu wameonekana kuiangusha Simba msimu huu.

Jean Charles Ahoua, Syeven Mukwala na Elie Mpanzu waliofunika msimu uliopita wakionekana kupungua makali, lakini hata kukosekana kwa kipa Moussa Camara na Abdulrazak walio majeruhi ni anguko jingine la Simba.

Kuondoka kwa kocha Fadlu Davids kisha kuletwa kwa Pantev aliyedumu siku 61 ni janga jingine linaloonekana kuwavuruga wachezaji ambao sasa wanasubiri kocha mpya.

 Fadlu akionekana kuanza kujenga timu wakiwamo aliowasajili kabla ya kuondoka na kuja Pantev aliyekuwa akitengeneza kikosi kipya baadhi ya wachezaji wakikosa nafasi tofauti na zamani, huku kikosi cha kwanza kikiwa hakijapatikana akaondolewa. Pia sintofahamu inayodaiwa kuwepo upande na uongozi na kukosekana kwa mtaalamu wa kusoma mpinzani kupitia video (Video Analyst) ni kitu kinachodaiwa kuivuruga Simba, licha ya mzigo wa lawama kuangushwa kwa makocha tu

Wachezaji hawajitumi na kuwa na utulivu, kitu kinachodaiwa inachangiwa na kukosa wa kuwahamasisha na kuwajenga kisaikolojia ili kuibeba timu uwanjani.

Kocha wa zamani wa Simba, Dylan Kerr ambaye kwa sasa yupo Marekani ameifanyia tathimini Simba katika mechi mbili ilizopoteza katika michuano ya kimataifa na kueleza kinachoitesa. “Kuna namna timu inakatika na wachezaji wanaonekana kujisahau hasa wakati wa kulinda pia kuna tatizo la kutumia nafasi tazama marudio ya mechi Simba ilipoteza sana nafasi za wazi,” alisema kocha huyo.

Kwa upande wake, John Tegete, kocha kitaaluma na meneja wa zamani wa Uwanja wa CCM Kirumba, anaiangalia Simba kwa mtazamo mpana zaidi, akisema lililoonekana ni mabadiliko mengi kwa muda mfupi.

“Huwezi kutengeneza utulivu wa timu ikiwa benchi la ufundi linabadilishwa mara kwa mara,” alisema. “Wachezaji wanahitaji kuelewa mfumo mmoja, kanuni moja na sauti moja ya mwalimu. Ukibadilisha mara kwa mara, unaunda pengo la kimfumo linaloathiri matokeo moja kwa moja.”

Katika kipindi hiki ambacho Simba ipo kwenye mchakato wa kusaka kocha mpya, jambo la kwanza linalopaswa kupewa uzito ni kurejesha utulivu ndani ya kikosi. Mabadiliko ya benchi la ufundi yanaweza kuwa yamechangia kwa namna moja hasa upande wa  saikolojia kwa baadhi ya wachezaji, jambo ambalo linaweza kuathiri utendaji wao uwanjani. 

Mazungumzo ya mara kwa mara na uongozi, kuondoa presha zisizo za lazima na kujenga morali ndilo daraja la kuifanya timu iimarike hata kabla ya mwalimu mpya kutua.

Pili, Simba inapaswa kufanya tathmini ya kiufundi (technical audit) ili kubaini maeneo yaliyoteleza. Ni muhimu kuelewa wachezaji gani wanaendana na mfumo unaotakiwa, yupi anahitaji msaada zaidi na ni sehemu gani ya uwanja imekuwa ikisababisha udhaifu. 

Tathmini ya aina hii humsaidia kocha mpya anapoingia, kwani badala ya kuanza upya, anapata ramani ya kile kinachohitajika kufanyiwa maboresho.

Mwisho, Simba inapaswa kuweka mkakati wenye mwelekeo wa muda mrefu, badala ya kukimbiza matokeo ya haraka. Kocha mpya atahitaji muda, mazingira sahihi na mpango endelevu. 

Maboresho ya sasa yakifanyika kwa utulivu, basi ujio wa kocha mpya unaweza kuwa mwanzo wa mabadiliko makubwa tofauti na sasa.