Upungufu wa wataalamu, vitendeakazi changaoto Wizara ya Kilimo

Unguja. Wakati Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar ikiendelea na ziara Pemba, imebaini inakabiliwa na changamoto ya wataalamu wa kilimo na vitendeakazi.

Kutokana na hilo, wizara imeahidi kutafuta njia bunifu za kutumia ili kusaidiana na wataalamu na vitendeakazi vilivyopo kwa lengo la kuongeza ufanisi bila kuongeza gharama.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Desemba 9, 2025 na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Dk Salum Soud Hamed, akiwa ziarani kutembelea taasisi na vituo ndani ya wizara katika Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Dk Salum amesema kutokana na upungufu wa wataalamu ndani ya wizara, ipo haja ya kupanga upya maeneo ya kilimo kwa kuanzisha mpangilio maalumu wa upandaji miti ya matunda na kuimarisha vitalu vya uzalishaji miche ili kuzuia wadudu wasiharibu mbegu.

“Naipongeza menejimenti ya wizara kwa kuandaa ziara ambayo imetoa mwanga juu ya mafanikio na maeneo yanayohitaji kuimarishwa. Serikali itatafuta njia bunifu za kutumia wataalamu waliopo kwenye idara tofauti ili kuongeza ufanisi,” amesema.

Kwa upande wake, Waziri wa wizara hiyo, Suleiman Masoud Makame, amesema wamedhamiria kufanya mageuzi ya sekta ya kilimo kwa kuimarisha maeneo ya uzalishaji ili kuwa na uhakika wa chakula nchini.

Amesema ziara hiyo imelenga kuyatambua maeneo yanayomilikiwa na wizara, kuyapima kimafanikio, kubaini changamoto zilizopo na kuhakikisha utekelezaji wa majukumu unakwenda sambamba na malengo ya Serikali.

“Katika maeneo yote tuliyotembelea yapo mafanikio lakini tunahitaji kufanya kazi kubwa ya kuimarisha sekta hizi. Serikali haiwezi kuwa na ardhi ambayo haitumiki wakati ina mahitaji makubwa,” amesema.

Vilevile, ameeleza kuwa changamoto nyingi zinahitaji hatua za haraka kwani maeneo mengi yanayomilikiwa na wizara hayatumiki ipasavyo, jambo linalochangia uvamizi na kurudisha nyuma juhudi za Serikali.

Msimamizi Idara ya Kilimo, Mbarouk Ali Mgau, amesema zipo changamoto zinazowakabili, zikiwamo upungufu wa wafanyakazi na vitendea kazi, ambazo  zinazokwamisha kasi ya maendeleo.

Hata hivyo, amesema zipo hatua zimeanza kuchukuliwa ili kuleta mafanikio ndani ya sekta.

Amewapongeza viongozi kwa kuamua kutembelea maeneo yao ya kazi, ikiwa ni mara ya kwanza tangu walipoteuliwa kushika nyadhifa hizo.

Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Saleh Mohamed Juma, amewataka watendaji kuimarisha nidhamu ya kazi, kuwahi kazini na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.