Wanawake 22 wapandikizwa mimba Muhimbili

Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imesema jumla ya wanawake 22 wapo katika hatua mbalimbali za upandikizaji mimba Vitro Fertilization (IVF) hospitalini hapo.

Hatua hiyo inakuja miezi 16 ikiwa imetimia, tangu Muhimbili kuanzisha rasmi kitengo cha upandikizaji mimba.

Kwa mara ya kwanza, Muhimbili ilianza upandikizaji wa vijusi kwenye tumbo la mama wiki ya kwanza ya  Mei mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dk Delila Kimambo jana Jumatatu, Desemba 8, 2025 wakati akitoa hotuba yake  kwenye kikao kazi kati ya Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa na watumishi wa sekta ya afya kilichofanyika hospitalini hapo.

“Tangu kuanzishwa kwa huduma hii Septemba 2024, wanawake 22 wapo katika hatua mbalimbali za matibabu. Waziri, tunajivunia kuwa kwa sasa huduma hizi zinatolewa kwa asilimia 100 na wataalamu wazawa,” alisema.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo Muhimbili mpaka kufikia mwishoni mwa Mei kati ya wenza 2,000 waliofika kuhitaji upandikizaji  na walioonekana hawawezi kusaidika zaidi ya kupandikiza walifikia 120.

Mkuu wa kitengo cha IVF Muhimbili, Dk Matilda Ngarina alipofanya mahojiano maalumu na Mwananchi mapema Aprili 2025 alisema wanawake 11 walifanikiwa kuvuka katika hatua za awali.

Idadi hiyo alisema ni kati ya wenza 31 walioanza hatua za awali za uvunaji wa mayai na mbegu za kiume, kisha kuunganishwa maabara na kufanikiwa kutengeneza kijusi, kabla ya upandikizaji vijusi hivyo katika tumbo la mama.

Amesema mpaka sasa wametoa huduma kwa makundi matatu, ambapo walianza kundi la kwanza lenye wenza watano Desemba 2024, kundi la pili lenye wenza 13 Februari 2025 na kundi la tatu lenye wenza 13 mapema mwezi huu.

“Kundi la kwanza lilikuwa na wagonjwa watano, kati yao watatu ndiyo waliweza kukidhi vigezo mpaka hatua ya mwisho ya kunyonywa mayai na kutengenezwa kijusi baada ya muunganiko  wa yai la mama na mbegu ya baba na kutengeneza kijusi ambacho tumekifreeze (kugandisha) maabara.”

“Kundi la pili tulikuwa na kinamama 13 kati ya hao wanane ndiyo walikwenda vizuri mpaka mwisho na kuweza kutengeneza vijusi ambavyo vipo frozen.

“Sasa hivi tuna kinamama 13 ambao wameanza matibabu ya kuja kunyonywa mayai na katika kundi hili ndiyo kwa mara ya kwanza kumeanza kutumia mbegu kutoka kwa donors ‘wachangiaji’ huko nyuma tulikuwa tunatumia wenza wao,” alisema Dk Ngarina.

Alisema kwa sasa katika upandikizaji, wanasayansi wanashauri kitu kinaitwa ‘freeze all’ alimaanisha kugandisha kwanza ‘kijusi’, akisema zamani baada ya mbegu na yai kurutubishwa maabara baada ya siku tatu mama alipandikizwa.

Lakini sasa wakabaini ukimpandikiza hapohapo, kunakuwa hakuna matokeo mazuri ikilinganishwa na kuhifadhiwa kwa muda, mwili wa mama ukapumzika.

Alisema kazi ya kupandikiza ni  kubwa, tofauti na wengi hudhani mama atafika na kuvunwa mayai na kupandikizwa.

“Ni shughuli ndefu ya maandalizi, lazima mwili ukae sawa ijulikane shida ni nini, tuamue kwamba utapewa huduma namna gani ya kuuandaa mwili,  tuanze kukuchoma zile sindano, twende chumba cha upasuaji tuvune yale mayai, tuyarutubishe na kuyaunganisha na mbegu, halafu yaachwe yaatamie yatengeneze kijusi.

“Vijusi navyo vinakuwa na hatua au ubora mbalimbali, tunavipa ubora kusema hiki bora, bora kidogo na hiki hakifai, kwa hiyo unaweza ukaanza vizuri  mpaka unafika mwisho kuja kutengeneza kijusi unakuta kijusi hakifai kabisa,” alisema Dk Ngarina na kuongeza;

“Ndiyo maana unaona tunaanza na wengi, lakini wengine wanatenegeza kijusi ambacho hakina mfumo mzuri, kwa hiyo ile hatua ya ya kumwandaa mama mpaka aje atengeneze kijusi huwa tunataka atengeneze mayai mengi, ili usije ukarudia tena kuja kumchoma yale masindano huwa yana stress sana, hiyo huwa inafanya mwili wake unabadilika.”

Kwa mujibu wa Dk Ngarina mama akivunwa mayai hata kizazi huwa kikubwa kule anakolala mtoto, kwa hiyo hushauriwa mama akishanyonywa mayai kumuacha mwili wake kwanza urudi kawaida, kabla ya kumwandaa kwa ajili ya kumpandikiza.

Alisema kwa makundi ya awali yenye wanawake 31, 11 kati yao vijusi vipo vizuri kwa sasa wanawaandaa kupandikiza baada ya kuacha miili yao ikae vizuri na pia kulikuwa kuna hatua za kuangalia nyumba ya uzazi kwa ndani.

Alisema baada ya kunyonya mayai kabla ya kuja kupandikiza, lazima kuangalia nyumba ya uzazi ina hali gani kuhakikisha hakuna uvimbe, ghasia yoyote ambayo itazuia mimba isishike, kwahiyo wameshawafanyia vipimo na vizazi vyao vimeshatulia vizuri na wao wenyewe wako tayari kubeba mimba.

Sh1 bilioni fedha ambazo Muhimbili imelipa kununua vifaa vya upandikizaji mimba vilivyotoka nchini India kwenye kampuni ya Shibane.

Sh14 milioni, gharama za kuwezesha mtu kufanyiwa upandikizaji wa mimba katika hospitali hiyo, gharama inayodaiwa kuchangiwa na kutegemea vifaa na dawa kutoka nje ya nchi.