NI swali ambalo baadhi ya watu wamekuwa wakijuliza sababu zinazowafanya wasanii wa muziki, waigizaji na wanamitindo kupenda mchezo wa kikapu.
Jibu lilikuwa halipatikani ikizingatiwa kuna michezo mingine kama soka, kriketi, tenisi, vinyoya na magongo ambayo hushindwa kwenda kuangalia ikichezwa viwanjani.
Lakini, mbali na kupenda mchezo huo, wasanii hao wamekuwa pia wakionekana katika viwanja vya mpira wa kikapu kushuhudia ligi za kikapu zikichezwa.
Inaonyesha sababu zinazofanya wasanii waupende mchezo wa kikapu ni kutokana na kuendana na mitindo ya mavazi ya vijana wengi wakiwemo wanamuziki na wanamichezo wengine.
Hivyo siyo ajabu kuwakuta wasanii wa muziki na waigizaji wa filamu na wanamitindo wa mavazi wakifuatilia mpira wa kikapu iwe ni kwa kwenda uwanjani au kuangalia hata kwenye mitandao ya kijamii.
Kikapu ni mchezo ulioanzia Marekani, taifa ambalo ni kubwa kiuchumi duniani, huku burudani ikiwa ni sehemu kubwa inayolitangaza taifa hilo katika uhamasishaji zaidi vijana kwenye nchi nyingine duniani. Baadhi ya wasani wanaoonekana viwanjani katika Ligi ya Kikap Dar es Salaam ni Chid Benzi, Emmanuel Mkono, Young Lunya, Ally Kiba, Mheshimiwa Temba na Baba Levo.
Akizungumzia hilo la wasanii kupenda kikapu, kocha wa Game Time Squard, Bainas anasema wamekuwa wakipenda mchezo wa kikapu na ni kutokana na mchezo huo kuonekana kuwa ni utamaduni wao.
“Mchezo huo ulioanzia Marekani wasani wengi wamekuwa wakicheza mchezo huo, na jezi wanazovaa mitaani ni za mchezo wa kikapu,” anasema.
Issa Hassan, mdau wa kikapu kwa upande wake, anasema wasanii wamekuwa wakipenda mchezo huo jinsi wachezaji wanavyofunga na pia kuruka na kudanki.
“Mchezaji anavyofunga upande mmoja na mwingine anafunga upande wa pili wasanii wanaona ni burudani walizozoea,” anasema Hassan.
Baadhi ya wasanii waliocheza BDL ni pamoja na Mheshimiwa Temba aliyeichezea timu ya JKT na katika kilele cha mafanikio aliwahi kuwa mchezaji bora 2017.
Msanii mwingine ni Emanuel Mkono ajulikanaye kwa jina la kimuziki la ‘Nahreel’ aliyewahi kuichezea Mchenga katika Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam.